31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘Kisukari, shinikizo la damu chanzo cha kuugua macho’

Amina Omari-Tanga

MAGONJWA  ya kisukari na shinikizo la dawa ndiyo yanayoongoza kwa kuchangia   tatizo la macho kwa wagonjwa wake.

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummiy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kambi ya kinywa na macho iliyoendeshwa na Taasisi ya Bilal Muslim   jijini Tanga.

Alisema   wagonjwa wenye kukabiliwa na magonjwa hayo ndiyo wamekuwa wanapata matatizo ya uoni hafifu na wakati mwingine huchelewa kupata tiba mapema.

Alisema   kama wagonjwa hao wangekuwa wanajua hali zao na kupata tiba mapema wangeweza kuepuka matatizo ya ugonjwa wa macho kwa wakati.

“Takwimu zinaonyesha kati ya watu 100, wanne wanakabiliwa na matatizo ya macho ambayo yangeweza kutibika kwa haraka lakini wengi wao wanachelewa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu,” alisema Ummy.

Alisema kuwapo kambi za matibabu ya bure kumesaidia kwa kiasi kikubwa kubaini ukubwa wa maradhi ambayo yanawakabili wananchi wa eneo husika na serikali kuwekeza nguvu katika eneo hilo.

Awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Bilal Muslim, Muhsin Shein aliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa maboresho waliyoyafanya katika sekta ya afya nchini.

“Zamani tulikuwa tukifanya kambi tulilazimika kubeba mzigo wa vifaa na wataalamu lakini kwa mwaka huu hospitali zimeboreshwa kwa kuwa na vifaa bora na vya kisasa,” alisema Shein.

Alisema  katika kambi hiyo wamelenga kuwahudumia wagonjwa 7000 kwa siku tatu lakini kwa siku ya kwanza pekee wamehudumia wagonjwa 3000, kati yao 1500 wamepatiwa miwani huku 56 wakifanyiwa upasuaji .

Akizungumzia afya ya kinywa, alisema   changamoto kubwa iliyokuwepo na utumiaji wa tumbaku uliokithiri hivyo husababisha  athari ya meno kuchafuka na kutoboka.

 Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Njau Senkodri, alisema   kutokana na kambi hiyo, wamebaini kuwa wanajukumu kubwa la kusogeza huduma za macho na kinywa karibu na wananchi.

Alisema   hivyo wana jukumu la kuhakikisha wanajiwekea malengo mahususi ya kufikisha huduma hiyo karibu na wananchi ili waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi na haraka.

“Niwaombe wananchi matibabu ni gharama hivyo  kuepuka hizo gharama jitahidini mjiunge katika Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa muweze kupata matibabu yenye uhakika,” alisema Dk. Senkodri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles