30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kishoka wa Tanesco atapeli wananchi milioni 24

Eliya Mbonea, Arusha



Mkandarasi hewa wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), anadaiwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 24.6 kutoka kwa wananchi 22 wa Kijiji cha Manyire, Kata ya Mlangarini wilayani Arumeru mkoani Arusha kama gharama ya kuwaunganishia nguzo 40 za kupitishia umeme.

Ofisa Usalama Tanesco Mkoa wa Arusha, Frank Shida, amesema hayo yamebainika katika oparesheni iliyolenga kukamata wateja haramu waliojiunganishia umeme kupitia vishoka.

Amemtaja mkandarasi huyo kwa jina moja la Kileo ambaye anadaiwa kusambaza nguzo umbali wa zaidi ya Kilometa moja huku nguzo hizo zikidaiwa kutokuwa na viwango vya shirika hilo.

Amesema mchanganuo wa fedha hizo ni Sh 861,000 gharama ya nguzo kwa kila mtu, Sh 40,000 za fomu kila mtu, kushimba mashimo Sh 15,000 kila mtu na Sh milioni 4.5 kutoka kwa Joramu Muganda na kufanya jumla ya Sh 24,652,000.

“Kijiji hiki kina nguzo zaidi ya 40 hizi si mali ya shirika ila waya uliotumika ni mali ya Tanesco. Mfano, hapo kwa Mugunda amejengewa laini kwenda kwake na nguzo zaidi ya 20.

“Niwaombe wananchi watumie njia sahihi za kuunganishiwa umeme kwa kwenda wenyewe ofisini ili kuepuka hasara wanayopata kwa kuwapa fedha nyingi vishoka,” amesema.

Aidha Mwakilishi wa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Hassan Limuli, amesema vitendo hivyo vinalisababishia hasara shirika na serikali.

“Laini hii iliungwa kinyemela kwenye eneo ambalo bado hatujafika. Lakini pia laini ya waya uliotumiwa ni ndogo kwa aina ya nguzo walizoweka huwa hatutumii waya huo.

“Hatuna uhakika nguzo zimetibiwa, zinaweza kuoza baada ya muda mfupi zikaanguka na kusababisha madhara kwa watu na mali. Dola ipo itamsaka muhusika na nyinyi hamtapoteza fedha zenu tazirudisha,” amesema Limuli.

Aidha Balozi wa nyumba 10, Florence Swai, akizungumzia tukio hilo amesema miezi miwili nyuma aliona watu wakichimba mashimo na kuweka nguzo.

“Niliwauliza muhusika wa nguzo hizo nikaambiwa Bethuel Themu, niliposkia hivyo nikajua hii ni kazi halali ya serikali, hii inadhihirisha kuna wasio waaminifu ndani ya shirika kwani hapa watu wa Tanesco, walikuja ila hatukujua na ilikuwa ngumu kuwapiga picha kwani hatukuwa na shaka,” amesema Swai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles