31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kisena aondolewa mashtaka ya kutakatisha fedha

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MKURUGENZI wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena (46), mke wake Florencia Mshauri maarufu Florence Membe (43) na wenzao watatu, wameondolewa mashtaka ya kutakatisha fedha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilikubali kuondoa mashtaka hayo manne jana na washtakiwa kubaki na tuhuma za uhujumu uchumi, ikiwamo kusababisha hasara ya Sh bilioni 2.4 kwa Udart.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile kuwa upande wa mashtaka unawasilisha ombi kwa mahakama, la kuwabadilishia washtakiwa hati ya mashtaka.

Mahakama ilikubali ombi la upande wa mashtaka kuruhusu washtakiwa wasomewe hati mpya.

Katika hati mpya, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 15 kati ya 19 ikiwamo kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia Udart hasara ya Sh 2,414,326,260.70 baada ya kuondolewa mashtaka manne ya kutakatisha fedha.

Wankyo aliwataja washtakiwa wengine mbali na Kisena kuwa ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Chen Shi (32).

Ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 2012 hadi Mei 31, 2018 washtakiwa walitenda makosa hayo.

Kati ya Januari Mosi, 2011 na Mei 31, 2018 katika mahali tofauti wakiwa na watu wengine, ilidaiwa waliratibu shughuli za kihalifu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Inadaiwa kati ya Januari Mosi , 2015 na Desemba 31, 2017 katika eneo la Jangwani, washtakiwa hao wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil Gas Limited alijenga kituo cha mafuta kinachoitwa Zenon Oil and Gas katika karakana ya Kampuni ya Udart bila ya kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma na Nishati na Maji (Ewura).

Wankyo alidai kati ya Januari Mosi, 2015 na Desemba 31, 2017 katika eneo la Jangwani, Dar es Salaam washtakiwa wakiwa wakurugenzi wa kampuni hiyo kwa pamoja walianzisha biashara ya kuuza mafuta ya petroli katika eneo ambalo halijaruhusiwa.

Shtaka jingine inadaiwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa Robert, Kulwa, Charles na Florencia wakiwa na lengo la kuficha uhalisia, waliiba mafuta yenye thamani ya Sh 1,216,145,374 kwa kuyauza wakati wakijua mafuta hayo ni mali ya Udart.

Wankyo anadai kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 jijini Dar es Salaam kwa makusudi waliisababishia hasara Udart ya Sh 2,414,326,260.70.

“Washtakiwa wanadaiwa Juni 8, 2016 katika Benki ya NMB tawi la Bank House lililopo Ilala, Dar es Salaam, Robert na Chen walijipatia Sh milioni 594.9 mali ya mradi huo.

“Katika shtaka la mwisho, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 waliisababisha hasara ya Sh bilioni 2.4,” alidai Wankyo.

Hakimu alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi bila kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) au upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi haujakamilika na uliomba tarehe ya kutajwa na mahakama iliahirisha hadi Septemba 17. Washtakiwa walipelekwa mahabusu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles