25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kisa cha binti aliyebakwa na kundi la wanaume kwenye basi

Untitled-1NDANI ya nyumba yenye geti katika vitongoji vya magharibi vya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, picha ya msichana Hanna Lalango inaonekana katika fremu ikiwa imezungukwa na shada la maua.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 alifariki dunia, Novemba mosi mwaka juzi, baada ya kupanda basi dogo la umma na kubakwa na kundi la wanaume.

Simulizi ya Hanna inafanana na ile iliyotokea nchini India miaka mitatu iliyopita, wakati msichana alipobakwa na kundi la wanaume ndani ya basi na kufia hospitalini kwa majeraha aliyopata.

Tukio hilo lililoteka vichwa vya habari duniani lilisababisha mlolongo wa maandamano makubwa katika taifa hilo kubwa kidemokrasia duniani na kutoa wito wa kukomesha unyanyasaji wanawake na adhabu kali kwa wahalifu.

Lakini nchini Ethiopia, taifa la pili barani Afrika kwa wingi wa watu mwitikio wa kifo cha Hanna haukuwapo kabisa.

Uchumi wa taifa hilo umekua kwa kasi katika miaka ya karibuni na nchi hiyo imepata maendeleo makubwa katika miradi ya afya na upunguzaji umasikini kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Lakini unyanyasaji wanawake umebakia juu na mara nyingi ni kama mwiko kulizungumzia, hali inayochangia kulifanya lishamiri.

Asilimia 80 ya Waethiopia wanaishi katika maeneo ya vijijini, ambako mila na desturi zinawaweka wanawake kama raia wa daraja la pili.

Katika majiji na miji, wanawake wa Ethiopia na wageni kwa pamoja hulalamika kunyanyaswa kijinsia mitaani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) ya mwaka 2013, Ethiopia iko katika nafasi ya 121 kati ya nchi 187 katika suala la usawa wa kijinsia.

Kesi ya Hanna haikujulikana hadi pale macho ya Blen Sahilu, mhadhiri kijana wa chuo kikuu na mwanaharakati wa haki za wanawake yalipotua katika stori fupi iliyozikwa kwenye kurasa za ndani za gazeti moja nchini humo.

“Nilijua kesi hii haikupewa uzito na imeandikwa kirahisi rahisi. Nilishtushwa mno… mara ya kwanza niliwaita marafiki zangu na kuwauliza, je, mlisikia kesi hii? lakini hakuna hata mmoja aliyeifahamu,” Blen anasema.

Blen akaanza kuendesha kampeni ya mwamko kupitia Vuguvugu la Njano, kundi la kiharakati analoliongoza katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa.

Wafuasi wake katika mitandao ya jamii walimuunganisha na familia ya Hanna na haukuchukua muda aliweka taarifa za kutosha kuwafanya watu zaidi wazisome.

Siku Hanna aliyotoweka ilianza kama siku nyingine yoyote.

“Asubuhi alifanya kazi za nyumbani kama kawaida: kuandaa kifungua kinywa na kufanya usafi wa nyumba,” anasema baba wa Hanna, Lalango Hayesso na kuongeza: “Kisha nikamwambia aende shule ili asije akachelewa.”

Hanna alikuwa mwanafunzi mzuri- hakuwa mzururaji bali makini na ambaye alimuahidi baba yake atakuwa daktari siku moja.

Lalango alimsubiri binti yake arudi nyumbani saa 10 jioni, lakini hakutokea. “Tulienda hadi kituo cha polisi kisha tuliomba mno. Hakukuwa na kitu kingine tulichoweza kufanya.”

Siku 11 baadaye, mwishowe Hanna aliibuka kwa kupiga simu. “Uko wapi?” aliuliza wakati baba yake alipopokea simu.

Baba alimuuliza bintiye swali hilo hilo. Hatimaye wanafamilia walimuona, akiwa ametapakaa damu na kutelekezwa nje ya kanisa moja na walimkimbiza hospitali.

Baada ya mlolongo wa kumhamisha kutoka hospitali moja hadi nyingine, safari ya maisha mafupi ya Hanna duniani ilikomea kwenye Hospitali ya Zewditu katikati ya Addis Ababa.

Madaktari walifanya kila linalowezekana lakini baada ya siku 22 za matibabu alifariki dunia kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.

“Alitufikia akiwa amechelewa sana,” anasema Dk. Abiye Gurmessa, mtaalamu wa upasuaji katika hospitali hiyo, ambaye timu yake ilifanya kazi usiku na mchana kutibu majereha makubwa katika sehemu za siri huku akisistiza kuwa eneo la jeraha lilikuwa kubwa mno na lilikuwa na maambukizo.”

Wakati siku zake za kuishi zikielekea ukingoni, Hanna aliiambia familia yake kuwa alipanda basi dogo la umma baada ya kutoka shule, na wanaume waliokuwa ndani ya basi hilo walimpeleka katika moja ya nyumba zao na kumbaka kwa siku kadhaa kabla ya kumtelekeza mitaani.

Uchunguzi wa polisi ulifanikiwa kuwanasa na kuwaleta baadhi ya watuhumiwa katika chumba cha hospitali.

Lalango alisema bintiye aliwatambua wahalifu watatu miongoni mwa waliombaka ambao walisaidia kupatikana kwa wengine wawili zaidi.

Watu watano kwa sasa wanashikiliwa na polisi wakati uchunguzi ukiendelea.

Iwapo binti yake angenusurika, Lalango alibainisha hangeitoa kesi hiyo hadharani kuhofia aibu na fedheha ambazo zingemkumba Hanna kipindi chote cha maisha yake.

Wanaharakati wa haki za binadamu wanauona utamaduni huo wa kufanya siri vitendo vya ubakaji kunafanya visiripotiwe na hivyo kuendelea kushamiri.

“Nimefanyia kazi masuala haya, hivyo nadhani nayajua. Lakini nimejifunza mengi kuhusu vitu vipya,” anasema Blen na kuongeza kuwa marafiki wa kiume huelezana namna walivyokuwa ujanani na jinsi ilivyo kawaida kwao kufanya vitendo hivyo. Kwamba kuna  matumizi ya maneno ya staha katika kuelezea hilo, hawaiti genge la ubakaji. Lakini wanajua kuwa si kitendo cha hiari.”

Kufuatia kesi ya Hanna, wanawake wengi wametoa mwito wa mabadiliko zaidi ya sera nchini humo.

Hata hivyo, Katiba ya Ethiopia yenyewe inasisitiza kuhusu haki za wanawake.

Sheria mpya ya familia ilipitishwa mwaka 2000 ikieleza umri wa ndoa kuwa miaka 18 na ilitoa fursa kubwa kwa wake kudhibiti mali kutokana na ndoa.

Aidha mwaka juzi, Ethiopia ilianzisha kampeni kwa kushirikiana na UN kupambana na unyanyasaji wanawake nchini humo.

Msemaji wa Serikali, Redwan Hussein alisema haoni umuhimu wa kubadili sera kufuatia kesi ya Hanna na kwamba serikali imedhamiria kukabiliana na vitendo hivyo.

“Elimu lazima iendelee, maendeleo lazima yaendelee na wanaofanya uhalifu lazima wafikishwe mahakamani, nadhani tuko katika mwelekeo sahihi,” alisema.

Lakini iwapo mabadiliko ya sera ni ya lazima, itakuwa ngumu kupata uthibitisho kutokana na ukosefu wa taarifa za kitafiti kuhusu unyanyasaji wa kijinsia nchini humo.

Tafiti za nyuma zilitoa picha yenye kuchosha lakini pia zikitumia sampuli ndogo mno na kuacha maswali mengi bila kujibiwa.

Blen alisema ana matumaini kesi ya Hanna itaibua ari ya kutaka tafiti zaidi. “Mkakati wa muda mrefu unapaswa uwe utafiti wa kitaifa badala ya eneo dogo,” alisema.

Lakini simulizi ya Hanna imefichua mwelekeo wa unyanyasaji wanawake wa Ethiopia.

Katika mkutano na wanahabari Novemba 24 mwaka jana kuhusu kesi hiyo, waliohudhuria walimwaga machozi wakati Lalango akieleza mkasa wa binti yake.

Wanawake waliohudhuria nao walieleza masaibu yaliyowapata wao au ndugu zao na walitoa mwito wa kuheshimiana baina ya wanaume na wanawake.

Na waliitaka serikali iwasilishe muswada wa sheria kali zaidi kuhusu usawa wa kijinsia.

Baba wa Hanna, amesema anahofia usalama wa binti zake wengine na mjukuu.

Lalango, ambaye ni Mkristo mcha Mungu amesema hana hofu na uwezekano wa athari za kisiasa kuhusiana na mkasa wa Hanna.

Amesema anachotumaini ni kuwa familia nyingine hazitakutana na maumivu kama iliyopata familia yake.

Kwa sasa amekuwa akiwalinda kwa karibu binti zake wengine wanne na mjukuu wake mdogo wa kike.

‘Katika utamaduni wetu, hakuna kitu kama hiki. Huenda huu ulikuwa ujumbe wa Mungu kuwaonya watu si Ethiopia tu, bali dunia nzima ili kisitokee tena kitu kama hiki” alimalizia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles