26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KIPO KITU ZAIDI YA KUAMBIWA UNAPENDWA – 3

Na JOSEPH SHALUWA

NI mada ambayo inakufungua kutoka gizani na kukurudisha kwenye mstari. Marafiki, huko nyuma katika matoleo mawili yaliyotangulia tuliona mambo muhimu ya kufanya ili kuonyesha penzi la dhati kwa mwezi wako.

Lakini pia tuliona sifa za mwenzi ambaye hana nia ya dhati katika uhusiano. Tunajifunza haya kwa makusudi kabisa ili tuwe kwenye uhusiano mzuri, wenye nguvu na mapenzi motomoto.

Leo tunamalizia sehemu ya mwisho ya mada yetu, nikiwa na imani kuwa tutajifunza mengi ambayo yatakuwa dira katika uhusiano na wenzi wetu. Twende sasa kwenye vipengele vilivyosalia.

Matendo yazungumze

Kichwa chako kikishakuwa fiti, sasa unatakiwa kuanza mashambulizi ya kurejesha msisimko ndani kwa kuonyesha vitendo.

Kuna wanawake ambao hujisahau baada ya kuingia kwenye ndoa na kupata mtoto/watoto. Kutwa, kucha utakuta wapo makini na watoto wao. Wameshasahau kuwa wana waume ambao ndiyo sababu ya watoto hao.

Hilo ni tatizo. Utakuta mwanamke anajiachia hivyo, hajali kama ana mume. Anabaki mchafu, mumewe akirudi anamkuta yupo hovyohovyo, tena muda mwingi akiwa na mwanaye, hataki ukaribu na mume wake, huo msisimko utatokea wapi?

Sasa badilika, ishi kimahaba. Muda wa mumeo kurejea nyumbani, jitahidi kuwa msafi, ishi kama ulivyokuwa awali kabla hajakuoa. Usipokaa kimahaba, atavutika vipi?

Hili lipo hata kwa upande wa baadhi ya wanaume. Kwa kuwa ameshaoa kila kitu kinaisha. Hapangilii nguo vizuri, haendi saluni nk. Hilo ni tatizo. Kama alikupenda ukiwa mtanashati ni kazi yako kuhakikisha unadumisha utanashati wako.

Hata mnapokuwa mmelala chumbani, lala mkao wa kuonyesha ‘upo tayari kwa lolote’, maana kuna mwingine, akilala ni kama anakuambia wazi kuwa, ‘sina mpango na kitu chochote’. Kwa wanandoa siyo sahihi.

Maliza tatizo

Baada ya yote hayo, sasa unatakiwa kuanzisha mazungumzo. Usikubali kukaa na matatizo muda mrefu, mazungumzo ni jambo la msingi zaidi.

Kikubwa ni kutumia kauli nzuri, epuka maudhi kwa mwenzi wako ili mwisho wa siku muweze kumaliza tatizo bila kutofautiana zaidi. Nalisema hili, maana kuna wengine, wanataka kumaliza tatizo lakini ndani ya mazungumzo wanaruhusu kutokuelewana.

Boresha

Kukaa kwa amani na upendo ni jambo zuri, kwa sababu mtakuwa mmeshajifunza kwa yaliyopita, ni wakati wenu sasa  kuboresha uhusiano wenu. Hakikisha yale uliyoyafanyia kazi hapo juu unayaendeleza kila siku katika maisha yenu ya uhusiano.

Isiishie pale tu ulipokuwa ukihitaji kutafuta suluhu, badala yake sasa, hakikisha kila siku unazidisha ubunifu ili mwezi wako akuone mpya. Penzi linaboreshwa marafiki zangu. Kauli nzuri, matendo mazuri, kuheshimiana, kusikilizana ni kati ya mambo muhimu ambayo yamesisitizwa mara nyingi sana na wataalamu mbalimbali wa saikolojia ya uhusiano na ndoa.

Hata viongozi wa dini wakati wakifundisha ndoa wamekuwa mstari wa mbele kuwafundisha wandoa kuwa na mambo niliyoelekeza hapo juu. Kwa nini? Kwa sababu ndoa haiwezi kukamilika ikiwa kutapungua hayo niliyosema hapo juu.

NINI ZAIDI YA ‘NAKUPENDA?’

Onyesha kuna zaidi ya upendo kwa mwenzako kwa kumheshimu, kumpenda kwa dhati, kumsaidia anapokuwa na matatizo, kuunganisha familia na mengine yanayozidisha upendo.

Kusema tu nakupenda, hakuna maana umeingia moyoni mwa mwenzako. Wako wengi tu hukutana klabu usiku, wanaambiana wanapendana, usiku wanalala pamoja halafu asubuhi kila mtu anachukua hamsini zake.

Kuna kitu zaidi ya neno, nakupenda. Dhihirisha basi kwa matendo. Kusema tu I love you, wakati matendo yako yanatafsiri unamdharau mpenzi wako hakuna maana yoyote na mwisho wake kila siku utabaki ukilia mapenzi yanakutesa!

Kazi ni kwako rafiki yangu.

Jiandae kusoma kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitaingia mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles