30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KINGUNGE NGOMBALE MWIRU: SHUJAA WA MAISHA BORA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


FEBRUARI 5 ya kila mwaka, Chama Cha Mapinduzi (CCM) husherehekea siku ya kuzaliwa kwake, lakini sherehe za mwaka huu ziLIgubikwa na majonzi kufuatia kifo cha mpiganaji wake, Kingunge Ngombale Mwiru.

Mwanasiasa huyo aliyezaliwa mwaka 1932 alifariki dunia Februari 2 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa baada ya kushambuliwa na mbwa wake Desemba 22, mwaka jana.

Habari za kifo chake si tu zilikuwa za kushtua lakini pia ziligusa hisia za watu wengi ndani na nje ya nchi.

Kwanza kifo chake kimetokea ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu alipofariki mkewe Peras ambapo Kingunge alilazimika kutoka wodini na kwenda kumzika kisha alirudishwa tena hospitali.

Taarifa za kifo chake zilisambaa katika vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi na katika mitandao ya kijamii hasa kutokana na harakati za mwanasiasa huyo mahiri nchini.

Kingunge alikuwa shujaa wakati wa uhai wake kwani historia inaonesha wakati nchi za Afrika zilipokuwa zikipigania Uhuru, yeye pia alishiriki katika harakati hizo akiwa mmoja wa vijana wa TANU walioshinikiza kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika.

Ushujaa wake huo unathibitishwa na magwiji wa siasa waliojitokeza kumzika mwanasiasa huyo ambao wengi walimwelezea kama mtu muhimu nchini ambaye hajapata kutokea.

Shujaa wa vitendo

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama Vya Siasa, John Shibuda, alisema Kingunge alikuwa shujaa wa vitendo vilivyosanifu na aliyejenga mwelekeo hai wa siasa za Tanzania na ukombozi wa Bara la Afrika.

“Ametuachia ufadhili wa maono na uzalendo, alikuwa shujaa wa kuishi na imani zake za uzalendo hazikubinuliwa na imani yoyote ile,” alisema Shibuda.

Mjenzi wa hoja

Aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali za Awamu Nne za kwanza, Stephen Wasira, alisema Kingunge alikuwa ni kiongozi aliyeamini kwamba hoja zinajibiwa kwa hoja.

Wasira alikuwa miongoni mwa viongozi walioruhusiwa kutoa salamu za mwisho kwa Hayati Kingunge wakati wa ibada fupi iliyofanyika nyumbani kwake.

“Nilipokuwa Waziri wa Serikali za Mitaa mwaka 1987 nilibahatika kufanya kazi na Kingunge nikiwa chini yake, wakati huo alikuwa na ofisi mbili, Dar es Salaam na Dodoma.

“Aliamini katika nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu hivyo, pale ambapo ulikuwa humwelewi alijitahidi kujenga hoja.

“Ni mwanaharakati lakini ni mshiriki mkubwa katika ujenzi wa Tanzania, tunasikitika kumkosa lakini hatuna cha kufanya tunamshukuru Mungu kwa yote,” alisema Wasira.

Ushindi wa CCM

Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe, alisema ushindi wote ambao CCM imekuwa ikipata katika chaguzi mbalimbali kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na mwanasiasa huyo.

“Ametuachia  vitabu vingi sana, kila ukiangalia Ilani za uchaguzi, Ilani za chama, miongozo ya CCM kwa sababu alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa karibu miaka yote anatoa ushauri.

“Yeye ndiye alikuwa anaandika na kuasisi Ilani za CCM na ushindi wote uliokuwa unapatikana, alijikita katika masuala ya siasa hivyo kwa sisi watu wa Mkoa wa Lindi tumepoteza lulu ambayo ilikuwa inatoa ushauri kwa vijana wote hasa walioingia katika medani ya siasa…yeye ndiye alikuwa Kungwi wetu na hakujali anamshauri nani,” alisema Membe.

Alisema ili kumuenzi ni vyema kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kutokuoneana, kuzushiana kwa sababu Mzee Kingunge alikuwa mkweli na alitekeleza kile alichokiamini.

“Itatuchukua muda kupata shoka la aina hii ambalo linaacha kila kitu kwa ajili ya kulitumikia Taifa ndani ya chama na ndani ya Serikali.

“Alichotuachia katika miaka 41 ya CCM ni kujenga demokrasia ndani ya Serikali na ndani ya chama, ukitaka kwenda kinyume na Mzee Kingunge kataa suala la demokrasia, hawezi kuwa rafiki yako,” alisema.

Alishawishi

Makamu Mwenyekiti wa CCM(Bara), Philip Mangula, alisema Kinguge aliamini katika nguvu ya hoja na si kwa kulazimisha.

“Kingunge alishawishi hivyo, viongozi wote tuige mfano huu wa kushawishi badala ya kulazimisha,” alisema Mangula.

Mshauri mwema

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema kwa muda mfupi waliofanya naye kazi waligundua kuwa alikuwa kiongozi mwenye ushauri mwema, mwenye kupenda kujenga mshikamano.

“Ni kiongozi ambaye kile anachokiamini alikuwa akikipigania bila kujali atapoteza nini upande wa pili, aliheshimu sana muda kama mlikuwa na ahadi mkutane saa tisa atafika muda huo, ni kiongozi wa tofauti sana.

“Tunaomba viongozi wa vyama vyote tuige kwa viongozi kama hawa ambao ni nadra sana katika Taifa kuwa nao, hawana chuki, hawana visasi kwa watu, wanapenda kusikiliza mawazo ya wadogo, wakubwa lakini wana misimamo ya kuleta umoja na mshikamano na si kulitawanya Taifa na kutengeneza madaraja ya viongozi,” alisema Mbowe.

Gwiji la Siasa

Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, alisema itachukua muda kumpata mwanasiasa kama Kingunge ambaye hakuwa mnafiki.

“Ni gwiji la siasa, alijitambua na huwa haropoki, alikuwa akitumia kichwa chake, ameondoka na yale ambayo itatuchukua muda kumpata mwanasiasa kama yeye,” alisema Simba.

Alikuwa na msimamo

Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine Afrika, msimamo pekee unaokubalika kwa tawala dhalimu ni ule unaoendana na mtazamo wao, lakini kwa Kingunge alikuwa haogopi kutoa msimamo wake bila kujali utawafurahisha ama hautawafurahishi wakubwa.

Hili linathibitishwa na Mwandishi wa Habari Mkongwe, Jenerali Ulimwengu.

“Alikuwa haogopi kutoa msimamo wake kama unawafurahisha ama hauwafurahishi wakubwa, alieleza misimamo yake hata kama Mwalimu Nyerere hakuifurahia.

“Nakumbuka mwaka 1978 aliwahi kufukuzwa katika jengo la Karimjee akiwa yuko ndani ya Serikali…tumuenzi kwa kuwa wakweli, kupunguza unafiki na woga,” alisema Ulimwengu.

Ulimwengu anaitaja sifa nyingine aliyokuwa nayo hayati Kingunge kuwa ni uwezo mkubwa wa kuchambua masuala na kuyaeleza kwa lugha fasaha inayoeleweka na kila mtu.

“Alikuwa na fikra pevu, alisoma na akajifunza kuwa mchambuzi wa masuala ya Kifalsafa, kisiasa na uongozi wa jamii,” alisema.

Naye Mbunge wa zamani wa Kahama Vijijini, James Lembeli, alisema ni vigumu kumwelezea Kingunge kwa sababu aliyaishi maneno yake.

“Vitendo vyake viliendana na maneno yake, sidhani kama kuna kiongozi mwingine ukiacha Mwalimu Julius Nyerere, Mwalimu alikufa maskini na huyu mzee nadhani amekufa maskini.

“Hakuwa na visasi wala kinyongo hata kwa wale waliomtukana, waliombeza na ndiyo maana amezikwa na umati mkubwa wa watu.

“Watu wa vyama vyote wamekuja…viongozi tuliobaki tutumie historia kuturejesha kwenye mstari,” alisema Lembeli.

Rais Magufuli

Rais Dk. John Magufuli alisema Kingunge alichangia katika juhudi za kupigania Uhuru wa Tanzania na baada ya uhuru akawa mtumishi mtiifu wa chama cha Tanu na baadaye CCM.

“Ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka.

“Ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu,” alisema Rais Dk. Magufuli katika salamu zake baada ya kifo cha mwanasiasa huyo.

Changamoto kwa wanasiasa

Kutokana na kifo cha Kingunge ni wazi kuwa kuna changamoto kwa wanasiasa na viongozi kuweza kuyaenzi mazuri ya mwanasiasa huyo.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), alisema Kingunge alikuwa na msimamo, uwezo wa kuthubutu na uzalendo hivyo ni vyema wanasiasa vijana wakaiga mfano huo.

“Jambo kubwa la kujifunza kwa Kingunge ni kuwa na msimamo na kutoogopa kutofautiana na wenzako hata kama ni wakubwa namna gani hasa pale ambapo wanafanya jambo ambalo huliamini,” alisema Nnauye.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad alisema; “Ni vizuri kuyaenzi yale aliyoyasimamia Mzee wetu, alikuwa anachukia uonevu dhidi ya mtu na mtu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF), alisema wamepata pengo kubwa ambalo halitazibika.

“Tumepata pengo ambalo halitazibika, tukiitaja Kilwa ama tukitaja siasa za Tanzania tunamuona Kingunge,” alisema Ngombale.

Mazishi yake

Safari ya mwisho ya mwanasiasa huyo ilihitimishwa juzi baada ya kuhifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, alisema Kingunge ni miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa nchini uliosababisha nchi kupata heshima.

“Kingunge ameacha historia kubwa katika nyaraka mbalimbali za Serikali, ni miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa nchini hadi tukapata heshima kubwa.

“Waliopewa dhamana katika nafasi mbalimbali tujifunze kuweka mbele uzalendo ili kumuenzi Kingunge,” alisema Jafo.

Mazishi yake pia yalihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, marais wastaafu, Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Ally Hassan Mwinyi.

Wengine ni Mama Maria Nyerere, Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mawaziri wakuu wastaafu, Joseph Warioba, Dk. Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa, Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chande, Jaji Mstaafu, Mark Bomani na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma.

Vile vile walikuwapo, Balozi Paul Rupia, Balozi Job Lusinde, Spika wa Bunge Mstaafu, Pius Msekwa, Mwanasiasa Mkongwe nchini, Dk. Crisant Mzindakaya, Prof. Issa Shivji, Prof. Mwesiga Baregu na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku.

Akihubiri katika ibada ya maziko, Katekista George Wilbard wa Parokia ya Chuo Kikuu, alisema ili kumuenzi mwanasiasa huyo ni vyema kuishi katika yale aliyoyaamini.

“Ikiwa tunaamini kwamba Yesu alikufa vivyo hivyo wao waliolala katika Yesu Mungu atawaleta pamoja nao. Maneno haya yadhihirike kwetu tunapomuaga Kingunge, tuna huzuni, tumempoteza na hatutamuona tena.

“Tukitaka kumuenzi ni kuishi yale aliyoyaishi na kuyafanya kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamuombea,” alisema Katekista Wilbard.

Waasifu wa Kingunge

Msemaji wa familia, Balozi Ali Mchumo, alisema Kingunge alizaliwa Mei 30 mwaka 1932 huko Kipatimo Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi, lakini alikulia jijini Dar es Salaam.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mchikichini kisha akajiunga na Shule ya Sekondari African Special na baadaye Shule ya Wavulana ya Tabora.

Alisema licha ya Kingunge kuwa na ufaulu ambao ungemwezesha kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda lakini alikataa kwenda huko na kutaka kwenda kusomea sheria nchini India.

“Wakati akisubiri kwenda huko aliajiriwa na Idara ya Public Waste (Wizara ya Ujenzi sasa) kama karani, mwaka 1954 Chama cha TANU kilizaliwa na wiki moja baadaye alijiunga na chama hicho.

“Ili aelekeze nguvu zake zote katika kupigania Uhuru aliamua kujiuzulu nafasi yake ya ukarani mwaka 1956 na kutumika kama Katibu wa TANU,” alisema Balozi Mchumo.

Balozi Mchumo alisema mwaka 1957, Kingunge alikuwa Katibu wa TANU wa Wilaya ya Rufiji.

Historia inaonesha wakati nchi za Afrika zilipokuwa zikipigania uhuru, Kingunge alishiriki katika harakati hizo akiwa mmoja wa vijana wa TANU walioshinikiza kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika.

Pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Pan African Movement ambapo alishika nafasi hiyo kwa muda mfupi kisha alirudi nchini na kuwa Kamisaa wa Siasa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Katika maisha yake toka ujana wake amelitumikia Taifa mpaka katika ngazi za juu kabisa.

Alishika nafasi mbalimbali nchini zikiwamo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mbeya, Tanga, Mbunge Jimbo la Kilwa, Mjumbe wa Kamati Kuu CCM na Waziri katika wizara mbalimbali kwa nyakati tofauti.

Alikuwa Mshauri wa Rais katika masuala ya siasa hadi mwaka 2010 na pia alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba akiwakilisha kundi la Tiba Asili.

Alikuwa Mwafrika wa Pili kuwa mkuu wa Chuo cha Kivukoni ambacho sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambacho kilikuwa mahsusi kwa ajili ya kupika viongozi.

Alijitoa CCM Oktoba 2015 baada ya kutofurahishwa na utaratibu uliotumika kumteua mgombea urais wa CCM mjini Dodoma Julai mwaka huo.

Hata hivyo hakujiunga na chama kingine cha siasa.

Mbali na Kingunge kutokuwapo katika maisha haya ya kawaida, ataendelea kukumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Atabaki kuwa nuru ya kuwaangazia viongozi wengine katika safari ndefu waliyonayo ya kulijenga Taifa hili ambalo lilikuwa ndiyo ndoto zake.

Mungu amlaze mahali pema peponi, Amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles