23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KINGUNGE, MAALIM SEIF WAMJADILI LOWASSA

 

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

UMEONANA na Lowassa hivi karibuni? Ni swali la mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Kombale Mwiru kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad aliyefika kumjulia hali Hospitali ya Taifa Muhimbili anakotibiwa.

Swali hilo la Kingunge kwa Maalim ambalo haikufahamika mara moja lilikuwa na maana gani, lilijibiwa kwa sauti ya upole na Maalim Seif: “Hapana sijamuona siku nyingi.”

Hata hivyo, Maalim Seif hakutaka kuendelea na msingi wa swali hilo kwake na badala yake aliendelea kumuuliza Kingunge kuhusu hali yake ya afya inavyoendelea.

Januari 8, mwaka huu Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, alifika hospitalini hapo akiwa ameambatana na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kumjulia hali mwanasiasa huyo.

KINGUNGE AMWELEZA SEIF YALIYOMPATA

Baada ya Kingunge kumuuliza swali Maalim Seif kuhusu kuonana kwake na Lowassa, alimweleza jinsi alivyong’atwa na mbwa wake ambao walimsababisha majeraha makubwa yaliyosababisha kufikishwa hospitali hapo kwa matibabu zaidi.

Akielezea jinsi alivyong’atwa na mbwa hao, alisema kuwa yeye anafuga, lakini hawamjui.

Akieleza sababu ya kutomjua, alisema huwa anatoka nyumbani majira ya saa 11 alfajiri na kurudi saa moja usiku jambo ambalo limechangia wasimfahamu hata harufu yake.

“Mara nyingi nauliza kama wameshapewa chakula na kama wamewafungia sawasawa au la, nikijibiwa ndiyo huwa naingia ndani,” alisema Kingunge.

Alisema siku ya tukio, mbwa wake hao watatu ambao walikuwa hawajafungiwa, walipomwona walimtoroka mlinzi na kwenda kumvamia.

Kingunge alisema mbwa hao baada ya kumvamia walianza kumuuma hali iliyomsababishia majeraha mbalimbali mwilini na maumivu makali.

Mazungumzo hayo kati ya Maalim Seif na Kingunge yalidumu kwa dakika tano.

SEIF AFICHUA UHUSIANO WAKE NA KINGUNGE

Baada ya mazungumzo yao, Maalim Seif, alitoka nje na kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza sababu zilizomfanya kufika hospitalini hapo kumjulia hali mwanasiasa huyo mkongwe nchini.

Alisema amefika kumjulia hali kutokana na majeraha makali aliyopata baada ya kuumwa na mbwa, lakini pia alimpa pole kutokana na kupatwa na msiba wa mke wake, Pares aliyefariki Januari 4 na kuzikwa Januari 11, mwaka huu katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Alisema Kingunge ni mwenzake na wametoka mbali tangu walipokuwa wote Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif alisema walikuwa pamoja kwenye Kamati Kuu ya CCM (CC) chini ya Mwenyekiti marehemu Mwalimu Julius Nyerere.

“Licha ya hilo, pia mimi na Kingunge ndio tuliunda sekretarieti ya kwanza wakati huo marehemu Rashid Kawawa akiwa Katibu Mkuu wa chama.

“Nimefanya naye kazi katika maeneo mbalimbali kwa muda mrefu, ni rafiki yangu, hivyo nilikuwa na wajibu wa kumwangalia sambamba na kumpa pole ya kufiwa na mkewe.

“Namwombea kwa Mungu aweze kumpa nguvu na maisha marefu, anyanyuke hapo alipolala aweze kurudi na kuendelea na shughuli zake za kila siku,’’ alisema Maalim Seif.

MUHULA WA URAIS Z’BAR

Katika hatua nyingine, Maalim Seif alisema mkakati wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutaka kubadili muhula wa urais ili uwe miaka saba kama ambavyo aliahidi Balozi Seif Ali Idd, autawezekana na wanajidanganya.

MGOGORO CUF

Alipotakiwa kuzungumzia mgogoro unaoendelea ndani ya chama chake kama unaweza kwisha na kukiimarisha kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, alisema hakuna mgogoro utakaodumu hadi wakati huo.

Alisema kwa sasa watashiriki chaguzi zote zinazofuata, huku akitamba katu chama hicho hakiwezi kufa kwani ni taasisi imara.

UCHAGUZI KINONDONI

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni, alisema yeye na chama chake wapo kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hivyo kwa sasa hawezi kusema jambo lolote hadi pale vikao vya pamoja vitakapoamua suala hilo.

UCHAGUZI MKUU 2020

Licha ya majibu hayo, MTANZANIA ilitaka kujua kama ana ndoto za kujitosa tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, na alijibu kwa kifupi kuwa chama kitaamua wakati ukifika.

LOWASSA ALIVYOIBUA MJADALA

Januari 9, mwaka huu, Lowassa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam, hatua ambayo ilizua mijadala mbalimbali, huku watu wakitafsiri kuwa huenda akarudi CCM, hasa baada ya kunukuliwa akimsifu rais kwa utendaji wake.

Wakati mjadala huo ukishika kasi, Januari 15, mwaka huu Lowassa, aliweka wazi mazungumzo yake na Rais Magufuli, na kusisitiza kuendelea na dhamira yake ya kusimamia mabadiliko kupitia Ukawa, licha ya kushawishiwa kurejea CCM.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Lowassa, alisema kwenda kwake Ikulu kulitokana na mwaliko alioupata kutoka kwa Rais Magufuli, akimtaka kukutana naye siku hiyo hiyo kwa mazungumzo jambo ambalo alilitekeleza.

“Ujumbe wa Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kwangu, ulikuwa ni kunishawishi kutaka nirejee CCM suala ambalo sikukubaliana nalo na milimweleza rais kwamba uamuzi wangu wa kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema haukuwa wa kubahatisha.

“Baada ya Rais Magufuli kunieleza ujumbe wake, nilitumia fursa hiyo kujadiliana naye juu ya masuala mbalimbali, likiwamo kutoheshimiwa kwa katiba na sheria kunakohusisha kupotea kwa watu, kuvamiwa na kutishwa na kushambuliwa kwa viongozi wa kisiasa wa upinzani, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, uminywaji wa demokrasia na hali ngumu ya uchumi kwa wananchi.

“Ni imani yangu kuwa rais atayazingatia haya na kufanyia kazi masuala haya kwa masilahi ya nchi yetu,” alisema Lowassa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles