24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kingunge kumnadi Lowassa leo

pic+kingungeNA FREDY AZZAH, LONGIDO

SIKU chache baada ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, kutangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo anatarajiwa kusimama kwenye jukwaa la vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) jijini Arusha kumnadi mgombea urais wa Chadema kupitia umoja huo, Edward Lowassa.

Meneja kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema, aliliambia gazeti hili kuwa mwanasiasa huyo atahutubia mkutano huo utakaoanza mchana.

“Kesho (leo), Kingunge atazungumza na Watanzania kuwaeleza kile anachokiamini, anataka mabadiliko, cha muhimu ni ujumbe wake,” alisema Mrema.

Alisema hadi sasa, Kingunge hajasema kama atajiunga na chama chochote kilicho kwenye umoja huo.
Kingunge aliyekuwa na kadi namba nane ya CCM, ni kati ya wanasiasa wa kwanza kukosoa mchakato uliotumiwa na chama hicho kikongwe kumpata mgombea wake wa urais.

Baada ya Lowassa kuenguliwa na katika kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM mwezi Julai, Katibu huyo wa zamani wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, alisema Kamati ya Maadili na Usalama iliteka
majukumu ya Kamati Kuu baada ya kuamua kuchuja majina ya makada waliojitokeza kuwania urais hadi kufikia watano.

Alisema jitihada hizo zilizofanywakwa kuvunja kanuni zililenga kumuengua Lowassa kuwania
kuingia Ikulu.
Kingunge, ambaye alijitokeza waziwazi kumpigia debe Lowassa, alisema kitendo cha kumuengua waziri mkuu huyo wa zamani kwa kuvunja kanuni, kimeacha kasoro kubwa ndani ya chama hicho tawala kwa sababu taratibu za
kupata viongozi zilikiukwa.

“Jitihada zote ambazo zimefanywa za kuvunja taratibu zilikuwa zinaelekezwa kwenye kumzuia Lowassa asipate haki. Badala ya yote nani kashinda? Kashinda Lowassa kwa sababu imeonekana wazi kuwa yeye ndio kipenzi cha Watanzania na hakuna kitu kikubwa kama kupendwa na watu,” alisema.

LOWASSA: KESHENI MKILINDA KURA

Katika hatua nyingine, mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, amewataka wafuasi wake kupiga kura na kukesha vituoni kuzilinda.

Lowassa aliyasema hayo jijini Arusha jana, alipopita eneo la Ngaramtoni, Jimbo la Arumeru Magharibi na kuzungumza na wananchi kabla ya kuendelea na ziara yake kwenye Jimbo la Longido na Namanga.

Kauli ya Lowassa ilitokana na kelele za wananchi waliokuwa wakiimba ‘rais, rais…’.
“Natamani hizo kelele zingenipeleka Ikulu, kitakachonipeleka Ikulu ni kura, nahitaji kura nyingi, hakikisheni mnapiga kura na kukesha vituoni mpaka mpate matokeo, wale wenzetu ni maarufu kwa kuiba kura,” alisema.

Alisema Mkoa wa Arusha una historia na Chama cha TANU pamoja na CCM, kwani ndipo lilipozaliwa Azimio la Arusha, lakini mwaka huu wataachana na chama hicho.

“Nimeona (CCM) wakipitapita Monduli na Arusha, nawaambia wasubiri tarehe 25, huu ndio mwaka wao wa kutoka madarakani… siku ikifika nendeni na vichinjio vyenu mkawakate,” alisema Lowassa.

Akizungumzia kero ya maji eneo hilo, alisema wakati akiwa Mbunge wa Monduli alichukua maji na kuyapeleka, huku akiwapa miundombinu viongozi wa Arumeru ili wapeleke maji kwa wananchi wao, lakini wakashindwa.

“Kulikuwa na pampu nne, mbili zikapeleka maji Monduli, mbili nikawapa viongozi wa Arumeru ili walete maji, tena niliwapa bure hizo pampu, sasa mimi nifanye nini zaidi ya hapo?” alisema. Alisema akipata madaraka atashughulikia
suala hilo na litakuwa historia.

Akiwa Longido, Lowassa alisema ameamua kuwania urais kwa sababu ana hasira na kumaliza umasikini, kwani siyo mpango wa Mungu watu wawe masikini.

“Nina usongo na umasikini, umasikini siyo mpango wa Mungu… nia yangu ni kuongoza taifa hili ili kuondokana na umasikini, nitaanza na elimu ambayo yote italipiwa na Serikali.

“Jambo la pili litakuwa kilimo, wakulima wataruhusiwa kuuza mazao popote na hawatakuwa na ushuru wowote kwenye mazao yao,” alisema.
Akiwa Namanga, alisema akiingia madarakani ataendeleza ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuhakikisha raia wa nchi hizo wanafaidi wote.

“Mimi na Serikali yangu, nikishinda tutaendeleza ushirikiano wa Afrika Mashariki, mpakani hapa siyo magari yanasimama simama, kazi ifanyike bila vikwazo, Namanga mtu akitaka kupita siyo asumbuliwe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles