23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kinana, Makamba, Membe mtegoni

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe na makatibu wakuu wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, wamewekwa mtegoni.

Mtego kwa makada hao umewekwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa iliyoketi jana Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na CCM, Kamati Kuu imetoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hao na kuiwasilisha katika vikao husika.

“Kamati Kuu imepokea taarifa ya awali kutoka kwa Kamati ya Usalama na Maadili juu ya utekelezaji wa azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha Desemba 2019 jijini Mwanza, kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama watatu; Yusuf Makamba, Abdulrahman Kinana na Bernard Membe, ambao wote wameshafika mbele ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu inayoongozwa na mzee Philip Mangula, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

“Kamati Kuu imetoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hawa watatu na kuiwasilisha katika vikao husika,” ilisema taarifa hiyo.

Akitoa ufafanuzi wa suala hilo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema; “baada ya siku saba kamati ya mzee Mangula itatumia taratibu za ndani ya chama kuwasilisha kwenye vikao ili isomwe, ijadiliwe na maamuzi yafanyike.”

Baada ya kikao cha Kamati Kuu ambacho kinafanya kazi kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kikao kingine cha juu kwa taratibu za chama hicho ni cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kinafanya kazi kwa niaba ya Mkutano Mkuu wa CCM.

Kutokana na maagizo ya Kamati Kuu jana, huenda sasa uamuzi kuhusu makada hao watatu ukafanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo inaweza kupitisha maazimio kama ya kuwapa onyo, kuwafungia kwa muda ama hata kuwafuta uanachama.

Tofauti na makada wenzake wawili, Membe kabla ya kwenda kwenye kamati ndogo Dodoma alizungumza na kutoa ujumbe kwenye ukurasa wake wa twitter.

Pia Februari 6 baada ya kuhojiwa, alisema safari yake ya kuhojiwa na kamati hiyo ya maadili ilikuwa na manufaa makubwa kwake, kwa CCM na kwa taifa.

Mbunge huyo wa zamani wa Mtama, alisema amekuwa mtu mwenye furaha mara baada ya kuhojiwa, na anakwenda kula chakula kizuri yeye na mke wake katika hoteli ambayo haijulikani na kwamba mengine yatakuwa yakipatikana kidogo kidogo mara baada ya kushiba.

“Lakini niwaambie safari hii ya kuja Dodoma ilikuwa ni ya manufaa makubwa sana sana sana kwangu, kwa chama na kwa taifa letu, mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo nikishiba.

“Kwa hiyo sasa hivi mimi na mke wangu tunaenda kula chakula kitamu sana kwenye hoteli moja ambayo haijulikani, ‘and then’ baada ya hapo nitaanza safari ya kwenda Dar es Salaam,” alisema Membe.

Vilevile alisema amekuwa ni mtu mwenye furaha kwa sababu amepata nafasi ya kujadili masuala ya kitaifa na kimataifa na pia amepata nafasi ya kufafanua mambo pamoja na kutoa mawazo yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles