27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KINANA ARUSHA KOMBORA KWA MAALIM SEIF

seif

Na Muhammed Khamis (UoI)-ZANZIBAR

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amerusha kombora zito kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, huku akimwita mgombea wa urais wa kudumu aliyekata tamaa.

Pamoja na hayo, Kinana amewataka Wazanzibari kuachana na maneno ya mitaani kwani Uchaguzi Mkuu ulishamalizika na Dk. Ali Mohamed Shein ameshaapishwa kuwa rais kwa mujibu wa sheria.

Kauli hiyo aliitoa jana katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Dimani zilizofanyika Maungani, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Alisema CCM itaendelea kuchaguliwa na wananchi kwa sababu inatimiza wajibu wa kuwatumikia wananchi, kutimiza matakwa na sera kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Kinana alishangazwa na CUF kushindwa kutanua wigo wa demokrasia ndani ya chama hicho na kuendelea kumshikilia mgombea urais mmoja wa kudumu kwa zaidi ya miongo minne.

“Kuna mgombea mmoja hapa Zanzibar ameanza kugombea urais tokea akiwa na miaka 30 na sasa ana miaka 80, toka akiwa bado kijana mbichi, sasa amekuwa kikongwe na kupinda mgongo ila bado ana tamaa ya kuwania urais.

“Demokrasia ndani ya chama chetu ni ya aina yake na kwamba kukubalika kwetu mbele ya wananchi kunatokana na misimamo yetu inayotetea masilahi ya umma. Hata demokrasia yetu ndani ya CCM kamwe haifanani na vyama vingine,” alisema Kinana huku akishangiliwa.

Kinana alisema CCM ina umoja imara na katu hazuiwi mwanachama kuwania nafasi ya uongozi na haina sifa ya kuwa na wagombea wa kudumu kama ilivyo CUF ambayo tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi sasa, Katibu Mkuu wake Maalim Seif amekuwa mgombea wa kudumu.

Alisema ushiriki wa wana CCM 25 ndani ya chama kuwania nafasi ya uteuzi wa ubunge Jimbo la Dimani ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa demkorasi, na mgombea aliyepatikana anaungwa mkono na wanachama wote.

Alieleza kuwa vikao vya CCM vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC) vilikutana na kupitisha jina la mgombea aliyeshinda kura za maoni, huku CUF ikiwa kimya, ikishindwa hata kufanya vikao vyake kwa mujibu wa katiba ya chama chao.

Akizumgumzia kupwaya kwa dhana na misingi ya demokrasia ndani ya CUF, Kinana alisema hivi sasa chama hicho kina wenyeviti watatu, ambao mmoja ni wa muda, mwingine wa mpito na aliyebaki ni wa zamani

Aidha Kinana aliwashangaa wanachama wa CUF ambao wanakubali kudanganywa kirahisi kila siku na kuaminishwa ipo siku mgombea wao wa urais aliyeshindwa uchaguzi atatangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Rais wa Zanzibar.

“Tuliambiwa hapa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafutwa, watakuja watu toka UN, mara tukaelezwa wangekuja   Jumuiya ya Ulaya, wakaambiwa washone nguo mpya kusherehekea ushindi, huku siku zikitaradadi hakuna kinachotokea,” alisema.

Kinana alisema viongozi wa CUF hawana uwezo wowote wa kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo kwani walibahatika kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini bado hakuna walichofanya.

“Kama ni mkate CUF walipata nusu na CCM nusu, wakashika wizara makini za Biashara na Viwanda, Katiba na Sheria, Habari na Utamaduni, Mawasiliano na Miundombinu, lakini kutokana na wao kuwa dhaifu, hawakumudu hata kujenga kiwanda kidogo,” alisema.

Kinana aliwaomba wananchi wa Dimani kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Juma Ali Juma kwa sababu ni makini, mchapakazi na mwepesi wa kuwatumikia wananchi.

Akihutubia katika mkutamo huo wa uzinduzi wa kampeni, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Idd, aliwaeleza wananchi wa Dimani kuwa si sifa ya wagombea wa CUF kuwatumikia wananchi na mfano mzuri ni katika majimbo ya Pemba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles