24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kimondo chazua taharuki Kagera

RENATHA KIPAKA (BUKOBA) na AGATHA CHARLES (DAR)


MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti, amewataka wakazi wa mkoa huo kuwa watulivu kuhusiana na sauti kubwa iliyosikika juz usiku ikiwa imeambatana na mwanga mkali katika anga na sehemu kubwa ya mkoa huo.

Akizungumza mjini Bukoba jana, Brigedia Jenerali Gaguti alisema kwa sasa watalaamu wa masuala ya anga wameanza kufanyia uchunguzi jambo hilo ili kujiridhisha juu ya kilichotokea na watakapokamilisha wananchi watajulishwa.

Akisimulia tukio hilo, mkuu huyo wa mkoa alisema kati ya saa 3:20 na 3:45 usiku juzi akiwa nje nyumbani kwake aliona kitu ambacho aanadhani ni nyota kubwa iliyoanguka kutoka angani.

“Naweza kusema karibu wakazi wengi wa Bukoba wameona jambo hilo, wapo ambao walipata shaka wakidhani ni tetemeko la ardhi, binafsi nimeshuhudia naweza kusema nilichokiona inaweza kuwa ni nyota kubwa kutoka angani na kuelekea upande wa Magharibi wa Ziwa Victoria.

“Usiku huo hali ya hewa ilikuwa na dalili za mvua hivyo tukio hilo linaweza kuwa na uhusiano wa nyota na mvua, tusubiri watalaam wa mambo haya wafanye uchunguzi tutawafahamiasha, kama ni nyota au nini na ilianguka au kuzama ziwani,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Dickison Mwombeki mkazi wa Kimbungu wilayani Muleba alisema alistushwa na muungurumo mkubwa uliosababisha yeye na majirani zake kukaa nje kwa muda mrefu kwa hofu ya kurejea kwa tetemeko lingine la ardhi.

“Nilidhani ni tetemeko…, lakini sikuona ardhi ikitikisika hapo nikafikiria labda ni bomu limepigwa sehemu au vita, sikuwa na amani tulikaa nje ya nyumba zetu hadi saa 8 usiku baada ya kuwasiliana na baadhi ya watu ambao wengine walidai pengine ni kimondo kilidondoka kutoka angani,” alisema.

Naye Anisia Ntangeki mkazi wa Katoma Manispaa ya Bukoba alidai tukio hilo lilitokea wakati yeye na familia yake wakiwa wanakula ambapo aliona mwanga mkali mithiri ya radi ukitokea ndani.

Anisia alidai kwa mawazo yake alidhani walikuwa wamevamiwa lakini baada ya kutoka nje aliona kitu hicho chenye mwanga mkali kilikuwa angani na kusikia mngurumo mkubwa ambao uliwafanya kutafuta eneo salama kujificha kwa hofu ya usalama wao.

Kimondo ni nini

Mtanzania lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Jiologia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Elisante Mshiu ambaye alifafanua zaidi nini maana ya kimondo.

Dk. Mshiu alisema. “Kimondo ni sehemu ya mabaki baada ya kuundwa mfumo wa jua na yanakuwa anga la juu yakiwa yameshikiliwa katika mfumo wa jua na yanakuwa yanatembea,” alisema.

Alisema kimondo kinaweza kuanguka kinapofikia nguvu ya uvutano na dunia.

Mtaalam huyo Jiologia alifafanua kuwa kasi ya kimondo kinapofikia hatua ya kuanguka kasi yake huwa ni kubwa na kiashiria cha moto hutokea baada ya msuguano wa hewa na kimondo.

“Kasi ni kubwa na kiashiria ni moto, msuguano wa hewa na kimondo husababisha moto. Kasi ya kudondoka chini hutegemea umbali wa anga la juu” alisema Dk. Mshiu.

Aidha kuhusu athari za kimondo kinapoanguka duniani, alieleza kuwa hutegemea na ukubwa kwani huweza hata kuangukia nyumba au eneo jingine lolote na kusababisha uharibifu.

Dk. Mshiu alisema miaka milioni 65 iliyopita kulikuwa na mjusi mkubwa (dinosaur) ambaye alitoweka kutokana na vimondo kuanguka duniani.

“Inategemea ukubwa, miaka milioni 65 iliyopita dinosaur waliishi na kutoweka kutokana na vimondo, kipindi hicho vimondo vilikuwa vikubwa lakini vya sasa ni vidogo.

“Kikiwa kikubwa kama nyumba kikadondokea nyumba athari yake ni kubwa. Lakini siku hizi vinaanguka nje ya maeneo ya watu labda kutokana na uchache wake,” alifafanua Dk. Mshiu.

Dk. Mshiu alisema vimondo vichache vinajulikana lakini vinaanguka mara kwa mara usiku na mchana.

Moja kati ya vimondo vinavyojulikana duniani ni kile cha Mbozi ambacho kipo mkoani Mbeya.

Katika mtandao wa Wikipedia, Kimondo cha Mbozi kinaelezwa kuwa ni kati ya vimondo vizito 10 vinavyojulikana duniani.

Kimondo hicho kina urefu wa mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22 huku kikikadiriwa kuwa na uzito wa takribani tani 16. Kimondo hicho kiligunduliwa mwaka 1930.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles