27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichotokea Sudan, Algeria kinanukia Morocco

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UTAFITI wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), unasema sehemu kubwa ya wananchi wa Morocco wako njiani kuyaacha makazi yao, shauku kubwa ikiwa ni kwenda barani Ulaya kusaka maisha mazuri, ambayo wanaamini hawawezi kuyapata wakiwa ndani ya taifa lao.

Hii huwa ni shauku ya vijana wengi wa Kiafrika, ambapo mhasibu mstaafu mkazi wa mjini Casablanca, Abdallah al-Barnouni, anaiita ni tama ya vijana wengi kutaka maisha mazuri ndani ya muda mfupi, huku wakiwa hawana mipango ya kuwafikisha huko.

“Kizazi cha sasa, watoto wa leo, wanataka kufanikiwa haraka. Wanataka wapate kila kitu ndani ya muda mfupi. Wanataka gari zuri, nyumba na kazi nzuri, yaani wanataka kuishi maisha mazuri,” anasema Al-Barnouni.

Hata hivyo, hiyo haiondoi ukweli kwamba bado wananchi wengi wa Morocco wanataka kuona mabadiliko ya kisiasa ndani ya taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika, jambo linaloibua shaka kuwa huenda likajikuta ikiingia katika machafuko kama ilivyokuwa kwa Sudan na Algeria.

Kwamba, Morocco haitofautiani na kilichotokea Misri, Libya, Tunisia na Yemen, mataifa ambayo pia viongozi wake waling’olewa Ikulu kutokana na hasira za wananchi waliokuwa wamechoshwa na mwenendo mbovu wa kisiasa uliochangia maisha magumu kwa walio wengi.

Saleh al-Mansouri, mmoja kati ya wananchi wa Morocco aliyeishi Ujerumani kwa miaka mingi, kabla ya kurejea nchini kwake, analizungumzia hilo katika mahojiano yake na BBC akisema:

“Watu wanakwenda huko (Ulaya) kwa ajili ya vitu ambavyo hawavipati hapa. Hapo ni suala la kiuchumi. Hapo unazungumzia mavazi na maisha mazuri kwa ujumla. Lakini pia, vipo vitu visivyoshikika.

“Hapa Morocco mamlaka hazijali wananchi. Ni kukosekana kwa hali ya kujaliwa ndicho kinachowafanya watu wakimbie.”

Kukazia hoja ya Al-Mansouri, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa nusu ya wananchi wa Morocco wanaotajwa kuwa ni milioni zaidi ya 35, wako kwenye harakati za kuondoka nchini humo.

Tukirejea kwa Sudan na Algeria, hali ilikuwa hivyo kabla ya maandamano makubwa yaliyozing’oa serikali zilizokuwa madarakani, ambapo wananchi walikuwa wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi.

Kwa Sudan, wananchi walishinikiza na kisha kufanikiwa kumtoa madarakani aliyekuwa rais wao wa muda mrefu, Omar al-Bashir, wakati wenzao wa Algeria walimng’oa Ikulu Abdelaziz Bouteflika.

Kama inavyotokea Morocco kwa sasa, maandamano ya wananchi yalikuja baada ya malalamiko na manung’uniko ya muda mrefu, wengi wakionesha hasira dhidi ya viongozi wao hao.

Mathalan, robo tatu ya wananchi wa Sudan wanasema wazi nchi yao ilikuwa ikiongozwa kidikteta na si kwa kufuata misingi ya demokrasia, wakati wale wa Algeria hawakuficha hofu yao juu ya chaguzi, wakisema hazikuwa zikiendeshwa kwa haki.

Hivi sasa nchini Morocco, wananchi walio wengi wameonesha kiu ya kuona mabadiliko ya kisiasa yakifanyika. Kwa mujibu wa ripoti ya BBC hayo ni maoni ya nusu ya idadi ya wale waliyotumika katika utafiti wake wa hivi karibuni.

Wananchi wa Morocco wakipambana na polisi katika maandamano yaliyofanyika Aprili, mwaka huu

Kwa upande wake mwandishi wa habari, ambaye pia ni mwanaharakati anayekinzana na mamlaka za Morocco, Abdellatif Fadouach, anasema: “Ndiyo, vijana wengi wanafikiria kuondoka, wameonesha kukata tamaa.”

Hali inatajwa kuwa mbaya zaidi kwa vijana, ambao kwa mujibu wa takwimu, ni asilimia 45 ya wananchi wa Morocco. Hivyo, kinachofanyika ni kuzorotesha shughuli za uchumi ndani ya taifa hilo.

Ni kupitia takwimu hizo, ndipo inapoelezwa pia kwamba asilimia 70 ya watu wenye umri chini ya miaka 30 hawafikirii chochote zaidi ya kufungasha virago vyao na kutimkia kwingineko kutafuta maisha mazuri.

Kuonesha ni kwa kiasi gani hali ya kisiasa nchini humo ni ya kutilia shaka, ni asilimia 18 pekee ya watu wenye umri wa miaka 18 hadi 29 ndiyo wanaoizungumzia vizuri serikali ya Morocco.

Inaelezwa kuwa serikali ya Mfalme Mohammed VI imebakiza mvuto kwa wazee kwani nusu ya wale wenye umri wa miaka 60 ndiyo wanaojipambanua kumuunga mkono kiongozi huyo.

Inaeleweka wazi kwamba bado walio wengi hawafurahishwi na kitendo cha kiongozi huyo, kujilimbikizia mamlaka makubwa, hasa baada ya marekebisho ya Katiba ya nchi hiyo.

Kinachoonekana kuwakera zaidi vijana wa Morocco si tu uhaba wa nafasi za ajira, lakini pia umekuwapo upendeleo wa fursa, wakitoa mfano wa upatikanaji wa leseni za uvuvi, ambazo zimekuwa zikigawiwa kwa wanasiasa na watu wa karibu wa familia ya kifalme.

Kuonesha hasira zao, wananchi wa Morocco waliingia mitaani mwaka 2016 na kisha kufanya hivyo tena mwaka juzi, wakilaani vitendo vya rushwa na uhaba wa ajira.

Maelfu ya wananchi waliandamana na mamia kujikuta wakiishia mikononi wa vyombo vya dola. Aidha, haijasahaulika kuwa yalikuwapo maandamano mengine Aprili, mwaka huu, wananchi walipopaza sauti zao kugomea uamuzi wa mahakama kuwahukumu viongozi wa upinzani vifungo vya gerezani.

Mmoja kati ya waliokuwa wamekumbwa na rungu hilo la mahakama ni mwandishi wa habari, Hamid el Mahdaoui, ambaye alitakiwa kwenda kukitumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kile kilichokuwa kimeelezwa kuwa alimpa silaha mmoja kati ya waandamanaji.

Haijasahaulika kuwa ni kipindi hicho ndipo yalipoibuka maandamano makubwa ya walimu waliokuwa wakilalamikia mishahara yao, ambapo serikali ya Morocco iliingilia kati na kuahidi kulishughulikia.

“Muda wowote kuanzia sasa, Morocco inaweza kushuhudia kile kilichotokea Algeria, Sudan, Syria, Misri, Libya au Tunisia,” anasema mwandishi Fadouach.

Ingawa maandamano hayo yalifanyika katika baadhi ya maeneo, wafuatiliaji wa siasa watakumbuka kuwa ilikuwa hivyo pia kwa mataifa yote ya Kiarabu yalioingia katika machafuko, nikitolea mfano Sudan na Algeria.

“Ni ngumu sana kutabiri itakavyokuwa,” anasema Abderrahim Smougueni, mwandishi wa habari wa jarida la kila wiki nchini Morocco liitwalo TelQuel Arabi. “Kuna hali ya wananchi kutokuwa na furaha na kuvurugwa na serikali na waziri mkuu (Saadeddine Othmani).

“Watu walikuwa wakitarajia kuona serikali ikipambana na rushwa. Badala yake, wanaongeza kodi kwa watu wa kipato cha kati, hivyo kulivunja nguvu kundi hilo muhimu.”

Lakini sasa, kinachoitofautisha Morocco na Sudan ni jeshi. Kule Sudan, ni chombo cha dola ndicho kilichoingilia kati na kumng’oa Bashir, ikiwa ni baada ya maandamano ya muda mrefu yaliyochangia wananchi wengi wasio na hatia kupoteza maisha, ukiacha waliolazimika kuyakimbia makazi yao.

Akisisitiza kuwa huenda yaliyoikuta Sudan yakachelewa kama si kutotokea kabisa nchini Morocco, Smougueni anasema: “Ukija kwa Morocco, hali ni tofauti kidogo kwani huku jeshi halina sauti mbele ya mfalme Mohammed VI.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles