27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kilakala: Hakuna wa kumwondoa JPM

FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa upinzani wa kuiondoa CCM madarakani bado haujazaliwa na kwamba chama hicho kitapata ushindi wa asilimia 100 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24.

Kilakala alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati akifanya mahojiano kwenye kipindi cha ‘Zungumza’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha Clouds Plus.

Alisema kuwa kwa kazi inayofanywa na CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dk. John Magufuli ni ngumu kuwashawishi wananchi kutokuichagua.

“Sasa hivi kilichopo ni kwamba hakuna mpinzani ambaye anashindana na CCM, badala yake watasalia kuwa nafasi ya pili tu, kwani malengo yao ni kutaka kupata ruzuku tu kwa kuwa wanapata idadi ya wabunge.

“Upinzani kwa miaka hii ya sasa, 100 au 200 ndiyo wafikirie kuchukua dola, lakini siyo sasa hivi, sababu chama chetu kina mtandao mkubwa wa viongozi unaoanzia chini, huku ukishirikisha wananchi katika suala zima la maendeleo, hivyo mbadala wa CCM Tanzania bado haupo,” alisema Kilakala.

Aliongeza kuwa wapinzani wa kweli lazima watatokea CCM kwa kuwa wapinzani wa sasa bado hawajaandaa mtu wa kuja kuwa kiongozi wa Serikali.

“Mfano uchaguzi wa mwaka 2015 naweza kusema kuwa ni kama CCM wenyewe tulikuwa tunashindana, kwa sababu mpinzani mkuu wa pili alikuwa ni Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu aliyelelewa na kukulia ndani ya CCM.

“Hivyo unaweza kuona kuwa wapinzani wenyewe bado hawajizatiti vya kutosha katika kuandaa na kutengeneza viongozi jambo ambalo kwetu lipo kuanzia uwepo wa UVCCM,” alisema Kilakala.

Katika hatua nyingine, Kilakala alisema kuwa chama hicho kimefanya mambo mengi makubwa ambayo daima yataendelea kukipa ushindi ikilinganishwa na upinzani.

“Chama chetu kimepewa ridhaa na wananchi ambapo ukiangalia kwa kiasi kikubwa mambo mengi yamefanyika ipasavyo kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema.

WABUNGE WA UPINZANI      

Akizungumzia kauli za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  za kuwakosoa wabunge wa upinzani kila kukicha wa majimbo ya Kawe, Kibamba na Ubungo, alisema wamekuwa hawatimizi majukumu yao ipasavyo.

“Wabunge jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kuwa wanawasilisha kero za wananchi wao, ikiwa na maana kwamba jambo linalohusu Kawe, Ubungo au Kibamba kwa sasa yanazungumzwa na mkuu wa mkoa au wilaya jambo ambalo linatafsri kuwa wabunge hao hawasikilizi kero za wananchi wao.

“Hivyo wananchi wanahitaji watu watakaowatumikia na ndiyo maana utaona kuwa jitihada za mkuu wa mkoa katika kuhakikisha kuwa majimbo hayo yanapata maendeleo zimezaa matunda na tayari Serikali imetenga fedha kusaidia Wilaya ya Ubungo, hivyo niseme tu kwamba wapinzani wa kuitoa CCM bado hawajazaliwa,” alisema Kilakala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles