25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

KILA SIKU NNE ZA MWEZI WATOTO WA KIKE HUACHA KWENDA SHULENI

Na Lilian Justice, Morogoro


SIKU nne za kila mwezi watoto wa kike huwa hawahudhurii masomo shuleni kutokana na kukosa vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi, maji safi na salama na hata chumba maalumu kwa ajili ya kujisitiri.

Hii imetokana na wadau ama serikali kushindwa kuweka bayana suala la watoto wa kike kuwekewa mfumo mzuri  wa upatikanaji wa huduma muhimu hususani anapokuwa kwenye hedhi.

Shule nyingi nchini, hasa zilizopo vijijini wanafunzi wa kike hushindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa taulo maalumu za kujisitiri (PADS), vyoo vilivyotenganishwa  na vya wavulana, milango yenye komeo, ukosefu wa maji safi, chumba maalumu kwa ajili ya kubadilishia  pedi jambo ambalo linamfanya mtoto wa kike akiwa kwenye hedhi kuona aibu kuhudhuria masomo na hivyo kuamua kubaki nyumbani.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UNESCO) inaeleza kuwa kati ya msichana mmoja hadi kumi waishio ukanda wa Sahara  hushindwa kuhudhuria masomo  pindi wanapokuwa kwenye hedhi.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkambarani, Bernadetha Malisa  anasema suala hili kwa kiasi kikubwa huchangia wanafunzi kufeli kwa sababu kila mwezi ni lazima wakache masomo kwa kuhofia kujichafua wakiwa darasani.

‘’Kama tungekuwa na fungu la kuwanunulia vifaa vya kujisitiri, nina imani mahudhurio yangekuwa mazuri na matokeo ya kuhitimu kidato cha nne au la saba yangeongezeka zaidi,” anasema Malisa.

Anasema wazazi/walezi huwa wanawafundisha watoto wao kujisitiri kwa kutumia njia za asili, ambazo si salama kiafya.

Anasema endapo serikali itatenga bajeti  kwa ajili ya vifaa vya kujisitiri kwa watoto wa kike shuleni kama ilivyo kwa elimu bure, suala la utoro kwao lisingekuwapo na hata mimba za utotoni huenda zingekwisha.

“Uongozi wa shule tunajitahidi kuandika andiko maalumu  kwa wadau wa elimu na mashirika mbalimbali ili kutuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo na chumba maalumu kwa ajili  kujisitiri,” anasema Malisa.

Naye Mwalimu Ajuta Lawrence, kutoka Kituo cha Taarifa na maarifa Kijiji cha Mkambarani kinachoratibiwa  na Mtandao wa Jinsia Tanzania  (TGNP), anasema jamii bado haina uelewa kuhusu matumizi ya vitambaa laini vya kujisitiri wakati wa hedhi, na hivyo kuendelea kutumia vitambaa  chakavu vya asili maarufu kwa jina la SODO.

‘’Jamii imeendelea kutumia vitambaa chakavu vinavyotokana na kanga ama nepi za watoto zilizochakaa, badala ya kutumia pedi za kisasa kujisitiri,” anasema Lawrence.

Anasema vitambaa hivyo mara nyingi huwa wanavianika chini ya godoro ili ndugu zake wadogo wasione kwani wakiona pengine wanaweza kuhoji ama kuvichezea.

‘’Wanalazimika kuvificha na kuvianika chini ya godoro ili visionekane, lakini tatizo ni kwamba haviwezi kukauka vizuri hivyo kuna hatari kubwa kwa mlengwa kupata muwasho au fangasi,” anasema.

Hata hivyo, anasema  kituo cha taarifa na maarifa  kimefanikiwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike shuleni kuhusu jinsi ya kujitambua na kujisitiri kwa kutumia vifaa ama taulo za kisasa wakiwa kwenye hedhi.

Anasema licha ya kutoa elimu hiyo, mwitikio bado ni mdogo kwa wazazi kubadilika kifikra na kuachana  na kutumia njia za kizamani katika kujihifadhi, pia kuwapa elimu watoto wa kike kutambua haki zao na kujiamini.

Anasema bado wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya kujifunzia kwa njia ya vitendo, hivyo wanalazimika kufundisha kwa nadharia pekee.

Naye mmoja wa wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Mkambarani, Salma Mohamed anasema mama yake amekuwa akimfundisha na kumpa matambara kwa ajili ya kujihifadhi akiwa hedhi.

Anasema hajui kama kuna njia nyingine ya kujisistiri zaidi ya hiyo na wala hajawahi kusikia ama kuona vifaa vingine vya kisasa vya kujihifadhi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkambarani, Mohamed Mzee anasema ili kuwaondolea watoto wa kike changamoto hiyo, tayari wameshapitisha maazimio kupitia kikao cha baraza la madiwani ili kuweza kufanya tathimini za shule zilizopo na kuona ni namna gani  watatenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa hivyo shuleni.

‘’Tulikaa kikao cha baraza na kujadili suala hili kwa kina, sasa hivi tunafanya tathimini ambapo mwezi huu tutakuwa na jibu kamili kuhusu suala la kutenga bajeti ili kuwasitiri watoto wetu wa kike,” anasema.

Anasema kuwa suala la upatikanaji wa vifaa vya kujisitiri ni jukumu la watu wote yaani wananchi, wadau mbalimbali, mashirika na serikali kwa ujumla kuhakikisha upatikaji wa vifaa hivyo unakuwa ni endelevu.

Kwa upande wake Ofisa Programu Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP, Deo Temba anasema ili kutekeleza bajeti inayolenga usawa wa jinsia hasa kwa wasichana wanaoishi vijijini, ni lazima vifaa vya  vya kujisitiri vipatikane bure na bila kutozwa kodi.

Temba anasema kuwa Mtandao wa TGNP umekuwa ukifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa vifaa hivyo vinapatikana kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo hutoa bure.

‘’Nchi za Kenya, Zambia, Uganda na Afrika Kusini  wanatoa pedi kwa watoto wa kike shuleni, hivyo na sisi Tanzania tukiweka mikakati ya pamoja tunaweza kufikia lengo hilo,” anasema Temba.

Anasema ili serikali iweze kufikia malengo hayo, inapaswa  kuweka midahalo na kuwakutanisha wadau mbambali  wa maendeleo na mashirika binafsi ama taasisi ili kuona ni jinsi gani watakavyoweka  mikakati ya pamoja na kutenga bajeti itakayowezesha upatikanaji wa vijaa hivyo shuleni hususani vijiini.

‘’Baada ya kukutana na wadau, serikali inaweza pia kutenga fungu maalumu kwa ajili ya kila shule kuwapo na chumba maalumu kwa watoto wa kike kubadili pindi wanapokuwa kwenye hedhi, na fedha kidogo itakayobakia waweze kusaidiwa wanafunzi wavulana  wasiojiweza’’ anasema ofisa huyo.

Wakati sasa umefika kwa serikali kupitia wizara husika kuhakikisha  inatenga bajeti maalumu kwa watoto wa kike kupata elimu iliyo bora kwa vitendo na katika vipengele vyote  kwa kuhakikisha upatikanaji wa vitambaa laini shuleni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles