28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘Kila mwenye kipande cha ardhi kulipa’

NA AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM

SERIKALI imezindua Mpango wa  Kutambua na Kusajili kila Kipande cha Ardhi Mijini  wenye lengo la kuleta mapinduzi  makubwa ya  kiuchumi  kwa wananchi  na kuwawezesha kushiriki katika maendeleo.

Mpango huo ambao unategemewa kutekelezwa katika  mitaa ambayo haijapimwa  na haipo katika zoezi  la urasimishaji  katika halmashauri zote na mijini hautahusisha wakazi waliopo katika maeneo hatarishi ikiwemo mabondeni na maeneo yaliyopita gesi.

Akizungumza jijini jana  wakati wa uzinduzi wa mpango huo Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi  William Lukuvi , alisema  Mpango wa Kusajili na Kutambua Kipande cha Ardhi Mijini  ni moja kati ya mikakati ya serikali ya awamu ya tano kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wake.

Alisema ili nwananchi waweze kushiriki maendeleo hayo ,usalama wa miliki ya ardhi yao ni suala muhimu  ambapo  katika hilo leseni za makazi cha kutumia ardhi mijini hutolewa kama hatua za awali za umilikishaji katika maeneo yaliyojengwa kiholela wakati taratibu za mipango mingine juu ya eneo husika zinaendelea.

“Mpango huu wa kutambua kila kipande cha ardhi mijini ambao unaanzia mkoa wa Dar es Salaam utatekelezwa   nchi nzima,utekelezaji wake utagharamiwa  na serikali kwakushirikiana na mamlaka za upangaji ,”alisema Lukuvi.

Alisema ili kupunguza muda wa kutambua na kusajili wizara imeandaa mfumo wa kieletroniki ambao unatumia simu ya mkononi kwa ajili ya kutambua na kuchukua taarifa za wamiliki.

“Taarifa hizi zitatumika kuandaa daftari la wamiliki kwa kila mtaa na baadae wamiliki watahakiki taarifa zao na mwishoni watalipia gharama ndogo ya kuandaliwa  leseni ya makazi  kwa kiasi cha Shilingi elfu tano,”alisema Lukuvi.

Alisema faida za mpango huo  ni kwamba utakuwa ni hatua ya awali ya zoezi la kupanga,kupima  na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini  na kwamba taarifa zinazokusanywa zinaweza pia kutumiwa na taassisi mbalimbali ili kuwezesha kufanya tafiti kwa ajili ya mipango ya maendeleo yenye manufaa kitaifa.

Alisema faida nyingine za mfumo huo ni wananchi kutambuliwa  na kupatiwa nyaraka za awali za umiliki zitakazoongeza usalama wa miliki ili kuwezesha maendeleo endelevu katika ardhi kwa maslahi mapana ya kiuchumi.

“Pia utapunguza migogoro ya ardhi na  kurahisisha  usimamizi wa maendeleo katika ardhi kwakuzingatia sheria ya kuweka vigezo na masharti katika ujenzi  hivyo kudhibiti ukuaji holela wa miji na kuzuia uharibifu wa mazingira,”alisema Lukuvi.

 Alibainisha faida nyingine  ni kudhibiti umegaji holela na ugawanyaji wa viwanja  katika maeneo yasiyopangwa  na kupimwa mijini hivyo kuzuia misongamano wa ujenzi katika makazi.

Aliongeza kuwa faida nyingine ni kwamba serikali itanufaika  kwakuwa na taarifa za kila kipande cha ardhi  katika maeneo yaliyotangazwa kuiva kimji ambapo itakuwa ni nyenzo muhimu katika usimamizi wa utawala .

Mbali  na hilo Lukuvi aliwataka watendaji wa wizara hiyo kuacha ubinafsi na kuwapa fursa watalaam waliopo katika ofisi hiyo kufanya kazi za kitaaluma na si kuwaficha katika viteno ambavyo havina tija na visvyoendana na taaluma walizonazo.

Lukuvi alitoa kauli hiyo huku akimtolea mfano Dk.Eric Mwaikambo ambaye ni mtaalam  wa masuala ya upimaji ardhi,mhandisi wa mifumo ya kompyuta  na mbobezi wa menejimenti  ya taarifa za  jiografia ambaye kwa sasa amestaafu lakini kuipindi akiwa wizarani hapo alikuwa kama mmoja wa watumishi was too.

“Huyu baba alishastaafu  lakini kulingana na ujuzi alionao nilimuomba Katibu Mkuu amrusdishe kwa ajili ya kutuandalia huu mpango tuliozindua leo na ameuandaa bure lakini tungeita watu kutoka nje tungetumia zaidi ya milioni mia mbili,pamoja na utaalam wake wote huo lakini alipokuwa wizarani alikuwa ni mmoja wa watumishi wa stoo wakati mtu huyu elimu yake ni  PHD na katika kipindi chote hakuwahi kuruhuiswa hata kukaa karibu na waziri walimficha,hichi mlichokifanya kwa mzee huyu kumficha  ni dhambi hata kwa Mungu,”alisema Lukuvi.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliwataka wakazi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa wizara kwakuwa ma mpango huo utasaidia kupanga vizuri miji ikiwemo jiji la Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles