27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

KILA LA HERI WATANZANIA WOTE KUFIKISHA MIAKA 55 YA UHURU

uhurupicha

LEO Watanzania wanasherehekea kutimiza miaka 55 tangu nchi hii ing’oe ukoloni kutoka kwa Waingereza Desemba 9, 1961.

Maadhimisho ya mwaka huu kitaifa yanafanyika jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Uhuru.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam Jumanne wiki hii na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ilisema shughuli za maadhimisho hayo zitaanza saa 12 asubuhi na kutoa wito kwa wakazi wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi.

Mbali na makomandoo wa JWTZ, Rais Dk.  Magufuli atakagua gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama; pia kutakuwa na gwaride la kimya kimya, burudani za vikundi vya ngoma na kadhalika.

Siku ya leo ni maalumu kuwakumbuka waasisi walioleta Uhuru wa nchi hii na kuwaomba Watanzania wote kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Magufuli katika kuimarisha uchumi wa viwanda na maendeleo ya nchi.

Tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana, hii itakuwa mara ya pili kwa uongozi wake kushuhudia maadhimisho ya siku ya Uhuru.

Hata hivyo, mwaka jana Rais Magufuli alifuta gwaride na sherehe zote za Uhuru, badala yake aliagiza siku hiyo itumike kwa kufanya usafi nchi nzima; na fedha ambazo zilikuwa zitumike kwa sherehe hiyo alizielekeza kwenye matumizi mengine.

Kwamba fedha Sh bilioni nne zilizokuwa zimetengwa kwa sherehe hizo aliagiza zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco iliyopo Dar es salaam kwa kuongeza njia za barabara za lami.

Baadhi ya watu wanazitazama sherehe za mwaka huu kuwa na sura tofauti kutokana na mwenendo wa Rais Dk. Magufuli wa kimaamuzi na kiutendaji.

Kwamba anaweza kuonyesha tofauti kwa  kuvaa magwanda ya jeshi na kukagua gwaride la maadhimisho hayo, kama alivyowahi kufanya mkoani Arusha mapema mwaka huu wakati alipokuwa katika Chuo hicho cha Maofisa wa Kijeshi (TMA) kilichopo Monduli mkoani humo.

Pia baadhi ya watu wanajaribu kuangalia sherehe za mwaka huu kwa kuutazama uamuzi wake wa hivi karibuni wa kuwakamisheni maofisa wapya wa jeshi Ikulu, jijini Dar es Salaam, tofauti na ilivyozoeleka, ambapo shughuli hiyo hufanyikia katika chuo cha kijeshi Monduli.

Katika sherehe za maadhimisho ya leo, Watanzania watakuwa na shauku ya kumwona Rais Magufuli akiingia uwanjani hapo na kukagua gwaride kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana.

Aidha, inasadikiwa kwamba Rais Magufuli ataendeleza utamaduni ambao kwa mara ya kwanza aliuanzisha mtangulizi wake kwa kutoa hotuba katika sherehe hii.

Marais wa zamani Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa hawakuwa wanatoa hotuba katika sherehe hizi.

Tunasema vyovyote itakavyokuwa, tunawatakia Watanzania wote sikukuu njema ya kusherehekea miaka 55 ya Uhuru wa nchi yetu.

Tunaitakia mafanikio miaka mingi ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles