29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kila la heri Samatta

samatha+px*Watanzania wamuombea, makocha, wadau wazungumza

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MACHO na masikio ya Watanzania leo yataelekezwa jijini Abuja, Nigeria ili kufahamu kitakachojiri kwenye hukumu ya makocha 54 wa timu za taifa Afrika,  ambao watahusika katika kumchagua mchezaji bora anayechezea ligi ya ndani Afrika.

Kinyang’anyiro hicho kinahusisha wachezaji watatu ambao ni Mtanzania, Mbwana Samata na Mkongo, Robert Kidiaba wanaochezea Klabu ya TP Mazembe, Baghdad Boundjah wa Algeria anayekipiga Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Kila mmoja katika orodha hiyo ana sifa yake iliyomfanya kupata nafasi ya kuingia katika tuzo hiyo ambayo Samatta anaonekana kuwazidi wengine.

Moja ya ubora ambao unatajwa kuwepo kwa Samatta ni kuwa mfungaji bora wa Afrika msimu uliopita na kuisaidia klabu yake ya TP Mazembe kuwa bingwa Afrika.

Mshambuliaji huyo machachari akiwa katika kiwango bora cha ufungaji wa mabao wastani wa 0.55, amekuwa ni mwiba wa mabao kwa wapinzani akiwa katika klabu yake ya TP Mazembe msimu uliopita katika ligi kuu ya nchi hiyo.

Pia Samatta aliweza kulifufua jina la TP Mazembe lililoonekana kufifia katika medali ya soka, kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara kushiriki na kufanya vizuri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Samatta akiwa katika ubora huo, mpinzani wake Boundjah aliwahi kuwa  mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tunisia msimu wa 2013/14, huku msimu wa 2014-15  akifanikiwa kucheza  michezo 23 na kupata mabao 11.

Hatua hiyo ni baada ya kutolewa kwa mkopo katika timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, akitokea Qatari katika timu ya Al Sadd kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika ligi hiyo.

Kila mshiriki katika kinyang’anyiro hicho anajua ubora wa Samatta, licha ya kwamba anaonekana si mwenye thamani nje ya Bara la Afrika lakini akawa wa kuigwa ndani ya ardhi ya bara hili.

Kwa sababu hiyo huwezi kumsikia bosi wa TP Mazembe, Moizze Katumbi akimzungumzia Robert Kidiaba, wakati anajua mlinda mlango wake huyo umri ulishamtupa mkono muda mrefu hata huo ushiriki wake ni kama anawakilisha tu kutokana na CAF kuthamini mchango wake katika soka la Afrika.

Akizungumzia juu ya mchezaji huyo, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, alisema hakuna kikwazo kitakachomkwamisha mchezaji huyo kutokana na sifa na ubora wake.

“Samatta ameisaidia klabu yake kuwa bingwa Afrika na amekuwa mfungaji bora wa Afrika, hivyo katika orodha ya wachezaji anaoshindana nao hakuna mwenye sifa kama zake, wasiwasi wangu labda kwa kuwa Kidiaba anatoka nchi inayozungumza Kifaransa na wengine Kiingereza.

“Kama atashindwa labda itatokana na ubaguzi wa maeneo na asili ya utawala wa wachezaji hao, lakini si ubora wa mchezaji huyo,” alisisitiza Mkwasa.

Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans van der Pluijm, amempa Samatta asilimia kubwa ya kushinda tuzo hiyo kutokana na kigezo cha kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na timu yake ya TP Mazembe.

Alisema straika huyo anastahili tuzo hiyo kutokana na uwezo mkubwa alioonyesha  akiwa na Taifa Stars, ambao kwa hakika utasaidia kumuongezea nafasi ya ushindi dhidi ya wapinzani wake.

“Kwa kuwa tuzo hii inawahusisha wachezaji wa ndani, Samatta anaweza kuwashinda wenzake kutokana na mafanikio aliyopata lakini kama ingekuwa ni tuzo ya wachezaji wa Afrika kwa ujumla nafikiri angeshinda yule anayecheza kwenye klabu kubwa barani Ulaya,” alisema Pluijm.

Naye Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, alisema Samatta ana nafasi kubwa ya kushinda kutokana na umri wake kuwa mdogo na unamruhusu kuwa mchezaji bora wa Afrika na hata duniani kwa baadaye na pia ni mmoja wa wachezaji waliotoa mchango mkubwa kufanikisha ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa TP Mazembe.

Alisema waandaaji wa tuzo hizo Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), linaweza kutaka kuweka historia kwa kumfanya awe mshambuliaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo kutoka Afrika Mashariki.

“Mbali na Samatta kuwa na mchango mkubwa kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na kuwa tegemeo, pia amekuwa ni mchezaji wa kwanza kutakiwa na timu za Ulaya katika usajili wa majira ya baridi kutoka Afrika,” alisema Mwakalebela.

MTANZANIA pia lilizungumza na  Kocha wa Simba, Dylan Kerr ambaye alisema kikubwa kitakachombeba Samatta ni ubora alionao zaidi ya wengine.

“Ukizungumzia ubora, Samatta ni lazima ashinde tuzo hiyo hakuna mjadala, msimu uliopita ameisaidia sana timu yake kufika hapo ilipo,” alisema Kerr.

Kocha wa timu ya JKT Ruvu, Abdallah Kibadeni, alisema anamuombea kwa Mungu mchezaji huyo wa kimataifa kutoka hapa Tanzania ashinde tuzo hiyo, kwani kiwango chake cha uchezaji ni sifa tosha inayoweza kumpa ushindi.

Mkongwe huyo amewataka vijana Watanzania, kuhakikisha wanaiga mfano wa mchezaji huyo anayewania tuzo ya mchezaji bora wa ndani Afrika.

“Nafarijika sana kumuona Samatta akiwania tuzo, hata kama atashindwa kuchukua lakini amejaribu na amelitangaza Taifa letu la Tanzania, mchezaji huyu ana sifa nyingi sana na nzuri, hana majivuno amekuwa akizingatia mafundisho ya walimu mara nyingi anapokuja hapa nchini huwa nakutana naye kufanya mazungumzo mbalimbali, anakubali ushauri wowote  na anaheshimu walimu, hajawahi kuonyesha dharau hata siku moja ndiyo maana hata kiwango chake uwanjani  kinazidi kuimarika zaidi na zaidi,” alisema Kibadeni.

Kennedy Mwisabula, aliliambia MTANZANIA kuwa matarajio yake makubwa ni kuona Samatta anachukua tuzo hiyo, ingawa ushindani utakuwa ni mkubwa.

Mwaisabula alisema Samatta ni mchezaji mzuri na tegemeo kwa taifa la Tanzania, juhudi zake ambazo amekuwa akizionyesha uwanjani ni kigezo tosha.

“Wasiwawi wangu yule mchezaji mwingine anayetoka naye timu moja Robert Kidiaba, ila Samatta yupo vizuri ingekuwa mimi ni mtoaji wa tuzo basi angeshinda, ila huwezi jua wenzetu kule wanaweza kusema umri wake ni mdogo ukilinganisha na hao wapinzani wake ambao wamekuwa wakiwania tuzo mara nyingi,” alisema Mwaisabula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles