23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete adokeza siri Katiba Mpya

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM, DODOMA

HATIMAYE siri nzito kwenye mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa walio chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), imeanza kujulikana baada ya Rais Jakaya Kikwete jana kutoa taarifa rasmi ya awali kuwa mazungumzo kati yao yanakwenda vizuri na mwafaka wa mchakato wa Bunge la Katiba utapatikana kuanzia Jumatatu ijayo.

Kwa maneno yake, Rais Kikwete wakati akihutubia taifa kupitia kwa wazee wa Dodoma alisema: “Mazungumzo yamekwenda vizuri na tumepeana majukumu ya kufuatilia, tutakutana tena tarehe 8, kuyamaliza na kujua kinachoendelea.”

Wakati Rais Kikwete akihutubia taifa jana, wasaidizi wake na viongozi wa TCD walikuwa katika kikao kwa ajili ya kupata mwafaka wa mzozo uliojitokeza katika mchakato wa kukamilisha Katiba mpya.

Taarifa za uhakika kutoka katika vikao hivyo vya siri vinavyoendelea jijini Dar es Salaam, zinasema kwamba kukutana kwao ni kuhakikisha wanakubaliana na kutoka na kauli moja juu ya mwafaka wa Katiba mpya hapo Jumatatu watakapofanya kikao na Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema kuwa alikutana na vyama vinavyounda TCD, ambavyo ni CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, UPDP na UPDP kinachowakilisha vyama visivyo na wabunge Agosti 31.

“Cheyo (Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo) aliniomba kuonana nao na kwa kweli sikuwa na hiyana, nikakubali, nilikutana nao hapa Dodoma. Tulipeana kazi za kufanya, kila mmoja akafanye, tupeane taarifa, katika kikao kile mazungumzo yalienda vizuri, tarehe 8 tutakapokutana kwa mazungumzo tuone tutafikia wapi, tuombe mazungumzo haya yafanikiwe ili tuende mbele kwa pamoja,” alisema Rais Kikwete.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika Ikulu ndogo mjini Dodoma, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kililiambia MTANZANIA kuwa viongozi wa Ukawa walikwenda na pendekezo la kumtaka Rais Kikwete asitishe mkutano wa Bunge la Katiba ili kuruhusu mabadiliko ya Katiba ya sasa kwa ajili ya mambo yanayohusu uchaguzi mkuu wa mwakani.

Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa TCD, Cheyo, walitoa mapendekezo hayo kwa Rais Kikwete  ikiwamo kuitaka Serikali kupeleka marekebisho madogo yafanyike katika Katiba ya sasa kuruhusu mgombea binafsi na uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Mbali na hilo, pia walimwomba Rais Kikwete katika marekebisho hayo ya Katiba ya mwaka 1977 kuwapo kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) na matokeo ya urais yaruhusiwe kupingwa mahakamani.

Hata hivyo, taarifa hizo zilidai kuwa mjadala huo mkali ulihitimishwa na Rais Kikwete kuwataka wajumbe hao wa TCD kuhakikisha kuwa wanakaa pamoja na kuangalia namna bora ya kuliahirisha Bunge hilo kwani sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 haielezi namna ya Bunge hilo kuahirishwa.

Chanzo hicho kilisema kutokana mapendekezo hayo ya kila upande, wajumbe wanaounda TCD walitakiwa kwenda kujadiliana kwa kina namna bora ya kuliendea jambo hilo kama ilivyopendekezwa na Rais Kikwete.

Katika kikao hicho, TCD walilazimika kuunda kamati ndogo inayoongozwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia huku wajumbe wake wakiwa ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema  Dk. Willibrod Slaa.

Kamati hiyo itafanya kazi ya kuchambua mapendekezo mbalimbali ambapo itakutana tena Septemba 6-7, kabla ya Septemba 8 kukutana na rais.

Taarifa hizo kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza baada ya kikao hicho cha pamoja, Rais Kikwete atawasiliana na mamlaka husika kuangalia namna bora ya kusitisha vikao vya Bunge hilo ili kuruhusu mazingira ya kufanyika kwa Bunge la Jamhuri.

Hatua hiyo italifanya Bunge la Jamhuri kufanya marebisho hayo kwa ajili ya muundo wa Tume ya Uchaguzi na namna bora ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na baadaye Uchaguzi Mkuu mwakani.

EBOLA

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa Ebola, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa unadhibitiwa.

Alisema tayari wameunda kikosi kazi cha kupambana ikiwa ni pamoja na kufunga mitambo maalumu ya kuonyesha maradhi hayo.

Alisema pia hospitali za wilaya zimeagizwa kuunda kamati za afya ili kudhibiti maradhi hayo na mengine yanayoweza kusababisha maafa kwa wananchi.

“Tumesambaza vifaa katika kila hospitali ya wilaya kwa ajili ya maradhi hayo, viwanja vya ndege kikiwamo cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na vingine,” alisema.

Alisema tayari wamepeleka watumishi watatu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupata mafunzo ya ugonjwa huo.

ELIMU

Kwa upande wa elimu, Rais Kikwete alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuchangia gharama za chakula kwa wanafunzi ili waweze kupata elimu bora.

Alisema ikiwa wanafunzi watapata chakula wataweza kuwa na afya bora itakayowaruhusu kusoma kwa bidii, hivyo basi kila mwananchi anapaswa kuona umuhimu kuhusu suala hilo.

“Ikiwa kila familia itachangia gunia moja la mahindi kwa ajili ya kugawa chakula shuleni, wanafunzi wataweza kusoma kwa bidii, kwa sababu si gharama, bali ni kujitoa kwa ajili ya watoto wetu,” alisema Rais Kikwete.

Alisema Tanzania ni moja ya nchi ambayo imepiga hatua katika masuala ya elimu kwa kiwango kikubwa kwa sababu mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa wanafanikiwa katika malengo waliyokusudia.

“Kila mwaka tumekuwa tukijitahidi kuimarisha bajeti ya ya Wizara ya Elimu, lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2016-17 kila mwanafunzi anatumia kitabu chake darasani, anapata mlo na kusoma kwa bidii,” alisema.

Alisema jukumu la upatikanaji wa elimu bora linaanzia kwa mzazi, mwalimu na Serikali, hivyo basi wanapaswa kushirikiana ili kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa.

“Serikali itahakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanatimizwa kwa vitendo ili kuwapa nafasi wanafunzi kusoma kwa bidii,” alisema.

MAJI

Akizungumzia kuhusu suala la upatikanaji wa maji safi na salama, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini na vijijini.

Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa mijini wanapata maji safi na salama wakati asilimia 65 ya wananchi wa vijijini wanapata huduma hiyo.

Rais Kikwete alisema kutokana na hali hiyo, Serikali imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maji, ikiwamo ile inayofadhiliwa na nchi mbalimbali duniani.

Alisema baadhi ya miradi hiyo iko kwenye hatua ya ukamilikaji wakati mingine iko kwenye hatua ya utekelezaji, kinachotakiwa ni kushirikiana na wadau hao ili kuhakikisha wanafanikiwa.

“Ili tuweze kufanikiwa katika mipango hii, Watanzania wanapaswa kulinda vyanzo vya maji, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa watu wanaoharibu vyanzo hivyo kwenye mamlaka husika,” alisema.

UMEME

Akizungumzia kuhusu suala la upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi, Rais Kikwete alisema kuwa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) limejitahidi kuunganisha huduma hiyo wananchi kwa gharama nafuu.

“Sasa hivi wananchi wanaweza kuunganisha umeme kwa kiasi cha Sh 27,000 wakati zamani ilikuwa Sh 400,000, ukiangalia gharama hizo unaona tofauti kubwa, hayo ni maendeleo,” alisema.

Alisema kuwa awali malengo ya Serikali ifikapo mwaka 2015 kuwe na asilimia 30 ya watu waliounganishiwa umeme, lakini hadi mwaka huu tayari wamevuka malengo na kufikia asilimia 36.

Rais Kikwete alisema licha ya kuwapo kwa maendeleo hayo, lakini bado kuna changamoto zinazolikabili shirika hilo ikiwa ni pamoja na wananchi kushindwa kuunganisha umeme kwa gharama hiyo.

“Kuna baadhi ya wananchi wanashindwa kuunganisha umeme kwa gharama hizo, hali hiyo inaleta changamoto kubwa, licha ya Serikali kujitahidi,” alisema.

MIUNDOMBINU YA BARABARA

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa miradi ya barabara, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali imeweza kuunganisha mikoa, wilaya, kata na  vijiji kwa barabara zinazopitika.

“Kwa kweli tumejitahidi sana, tumeweza kuunganisha barabara kutoka mikoa kwa mikoa, halmashauri, kata na mitaa,” alisema.

Alisema katika bajeti yake, Serikali imetenga Sh bilioni 751 ili ziweze kutumika kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara.

Rais Kikwete alisema fedha hizo ambazo zimeingizwa moja kwa moja kwenye Mfuko wa Barabara zitatumika kwa ajili ya kuboresha miundombinu hiyo nchi nzima.

KILIMO

Akizungumzia kuhusu suala la kilimo, alisema kuwa maeneo mengi aliyopita wakati wa ziara yake alikumbana na migogoro ya wakulima na wafugaji.

Alisema kuongezeka kwa migogoro hiyo kunatokana na kutokuwapo kwa mipango bora ya matumizi ya ardhi, hali inayosababisha mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakulima.

“Nimeagiza watendaji wa mikoa kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji.

“Kwa sababu ardhi haikui, lakini mifugo inaongezeka, watu wanaongezeka na matumizi pia yanayongezeka, bila ya kuwapo kwa mipango bora ya ardhi migogoro haiwezi kuisha,” alisema.

Alisema malalamiko ya ukosefu wa pembejeo katika baadhi ya maeneo ni tatizo, lakini Serikali inahitaji kuhakikisha kuwa suala hilo linafikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Binafsi nampongeza Mh. Rais J Kikwete kwa uongozi wake mzuri na wenye busara nyingi mengi aliozungumzia hasa kuhusu barabara, elimu, umeme, kilimo na ardhi mengi tumeyaona yametekelezeka angalau kwa wastani. Lakini kuhusu katiba naweza kusema kwa namna au dhahiri yeye kama Rais ndiye aliyevuruga mchakato mzima baada ya kwenda bungeni na msimamo wake wa chama kuhitaji serikali mbili wakati rasimu imetaja serikali, ko hata hizi juhudi anazofanya kuongea na ukawa kuhusu katiba hazitasaidia kitu cha msingi yeye kama rais mkuu wa nchi ana mamlaka ya kuvunja bunge la katiba na kuunda kamati ndogo kujadili mambo yahusuyo uchaguzi wa mwakani ili kupunguza matumizi makubwa ya pesa kama ilivyo dodoma sasa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles