24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kigwangalla aja na mbinu mpya dhidi ya Ukimwi

Na UPENDO MOSHA – HaI

SERIKALI imeanza mkakati wa kuhamasisha watu mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwamo wanasiasa pamoja na wasanii ili kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla aliyasema hayo jana, wakati akizindua kampeni ya upandaji wa Mlima Kilimanjaro  ambayo inashirikisha watu 80 kutoka nchi mbalimbali duniani, ikiwa na lengo la kuchangisha fedha za mapambano  dhidi ya Ukimwi, ambayo imendaliwa na Mgodi wa Madini ya Dhahabu wa Geita (GGM).

Kigwangalla alisema Wizara ya Maliasili na Utalii itaanda utaratibu wa kuhamasisha makundi ya watu mbalimbali, wakiwamo wasanii na watu mashuhuri ili wapande mlima huo.

Alisema takwimu za maambukizi mapya, hususani katika kundi la vijana, yanatisha na kwamba zinahitajika jitihada za makusudi kudhibiti ugonjwa huo.

“Hali ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi inatisha, lazima kama vijana tuwe mstari wa mbele kupambana na hali hii… nimepanga kupanda mlima huu na watu mashuhuri, wakiwamo wanasiasa na wasanii,” alisema.

Alisema mbali na kampeni hiyo, wizara yake imekuwa ikihamasisha utalii wa ndani na kukuza uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk. Leonard Maboko, alisema kila siku watu zaidi ya 200 huambukizwa virusi vya ugonjwa huo, kati yao asilimia 80 ni vijana kuanzia miaka 15-24.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Richard Jordinson, alisema tangu kampeni hiyo kuanzishwa, wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 13 na kwamba mwaka huu nchi zaidi ya 72 zimeshiriki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Ukimwi, Dawa za Kulevya na TB, Oscar Mkasa, alisema kamati hiyo inaendelea kuishauri Serikali kwa lengo la kupata vyanzo vya uhakika vya fedha kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles