31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kigwangalla aivunja Bodi ya Utalii

Loveness Bernard, Dar es Salaam

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kutokana na kushindwa kutekeleza maagizo ya wizara kwa wakati.

Akizungumza Dar es Salaam jana alipotembelea bodi hiyo, Kigwangalla, alisema amefanya uamuzi huo kutokana na kutokutekelezwa maagizo yake aliyotoa kwa TTB mwaka mmoja uliopita.

“Kuanzia leo (jana) naivunja bodi ya wakurugenzi isipokuwa mwenyekiti wake tu, nawapa muda watendaji kutekeleza maagizo yangu,” alisema Kigwangalla.

Pia alihoji suala la kuwekwa mabango yanayotangaza utalii katika sehemu mbalimbali za Dar es Salaam ikiwamo katika eneo la ofisi za bodi hiyo na kuweka majarida ya utalii katika ndege za Tanzania.

“Niliwaagiza muweke majarida katika ndege zetu na mabango sehemu mbalimbali yanayotangaza utalii, juzi nikitoka jimboni nilipanda ndege na baadhi ya abiria walinifuata na kuniuliza kwanini hatuna majarida yanayotangaza vivutio vyetu,” alisema Kigwangalla.

Katika hatua nyingine, aliitaka TTB kutumia watu maarufu kama vile Judith Wambura maarufu kama Lady Jay Dee, Ali Kiba, Barnaba, MwanaFa, Millard Ayo, Mbwana Samatta, Diamond Platinumz na wengine wenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii kutangaza utalii kwa kuwapa safari katika vivutio mbalimbali.

Pia aliitaka bodi hiyo kuwatumia wapiga picha waliopo nchini kwa kuwapa safari za mbugani ili wapate picha za matukio mbalimbali kwa ajili ya chaneli ya utalii.

“Chaneli yetu tangu imeanza kuruka ina wiki chache tu lakini tunarudia mikanda ile ile kwa maana hatuna footage za kutosha imefikia kipindi mtumie hawa wapiga picha kwa kuwapa ziara na footage mzipate kwa ajili ya chaneli yetu,” alisema.

Akijibu baadhi ya hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa TTB, Godfrey Meena, alisema majarida yanayotangaza utalii yameshachapishwa pamoja na flashi na yote bado yako bandarini yanasubiri kulipiwa ushuru.

“Majarida tumeyachukua jana na tunatarajia kuyasambaza haraka na kuna flashi zipo bandarini zinasubiri kulipiwa ushuru kwa sababu zilitengenezwa nje kutokana na oda ilikuwa kubwa, hakuna kampuni nchini iliyoweza kukidhi mahitaji yetu ikatulazimu kuagiza nje,” alisema.

Pia alisema baadhi ya taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili ikiwamo Ngorongoro, Tanapa, Tawa na TFS hazijawasilisha michango yao kwa ajili ya uanzishwaji chaneli hiyo.

“Ni TTB tu tumetoa mchango wetu kwa ajili ya uanzishwaji wa studio, tumenunua samani na kompyuta yenye server kubwa, changamoto ni kwamba wenzetu bado hawajawasilisha michango yao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles