26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kibano kipya, wauzaji wanunuzi wa mkaa

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

KATIKA kukabiliana na uharibifu wa mazao ya misitu, Serikali imetangaza kanuni mpya kuongeza usimamizi wa sheria kwa wanunuzi na wauzaji wa mazao hayo ikiwamo mkaa na samani.

Kwa mujibu wa kanuni hizo zilizotangazwa Mei 24 kupitia Tangazo la Serikali namba 417, adhabu kwa atakayezikiuka ni faini ya Sh 500,000 hadi Sh milioni 12 au kifungo kati ya miezi sita hadi miaka mitano.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Arjanson Mloge, alisema Serikali inafanya hivyo kuzuia uharibifu wa misitu.

Alisema kuna maeneo ambayo yamesajiliwa na Serikali kwa ajili ya kuuza mkaa au mazao mengine ya misitu na kushauri watu wanunue kwenye maeneo hayo.

“Sisi tunakemea wale watu wanaonunua kutoka kwenye maeneo ambayo hayajasajiliwa. Hatuwakamati watu ili mradi tu wawe na risiti kutoka kwenye ‘selling centre’ (maeneo ya mauzo yaliyosajiliwa).

“Mama wa nyumbani mahali anapokwenda kununua pawe pamesajiliwa, hata hapa mjini ukiona mkaa uko mahali unauzwa ujue pamesajiliwa, kama hapajasajiliwa ninashauri watoe taarifa,” alisema.

Alifafanua kuwa hata magari yanayosafirisha mazao hayo hayatakamatwa kama yamenunua kwenye maneo yaliyosajiliwa.

Alisema kila wilaya imeainisha maeneo yanayofaa kuvunwa mkaa na kuna watu wameomba na kupitishwa na kamati za uvunaji za wilaya na kupangiwa kiasi cha magunia ya mkaa ya kuvuna.

“Kuna uharibifu wa misitu unasababishwa na watu ambao hawataki kufuata taratibu zetu, mfano hawa watu wa pikipiki, yaani wanasababisha uvunaji unakuwepo mahali popote pale kinyume cha mipango iliyowekwa na Serikali.

“Kuwepo kwa bodaboda zinachukua mkaa mahali popote, zinasababisha kila mtu anaingia msituni kitu ambacho ni kinyume na hatuwezi kusema wafanyakazi wa misitu watakuwepo mahali pote kwa wakati mmoja. Ndiyo maana tunatumia njia tofauti tofauti kuwaelimisha wananchi umuhimu wa rasilimali hii ya misitu,” alisema.

MAFUNDI SEREMALA

Alifafanua kuwa mafundi seremala huwa wanasajiliwa na kwamba mtu anayekwenda kununua samani anapaswa kuhakikisha anapatiwa risiti ya mtengenezaji husika kwani ndiye anayepokea malighafi ya msituni.

“Sisi hatutakuuliza kama umenunua kitanda chako au umenunua milango, tunachotaka uwe na risiti ya kule ulikonunulia ili tujue yule mtu anayetengeneza anapata wapi malighafi.

“Kitanda si mazao ya misitu ni kama vile umevaa gauni lako nije nikuulize risiti ya pamba iliyotengeneza gauni lako, lakini ukiwa na ile risiti ya kununulia gauni tutajua umelinunua kwa nani na tutakwenda kuangalia yule mtu kama ana leseni, ndiyo vitu ambavyo tunahimiza,” alisema.

ADHABU, MAKATAZO

Kwa mujibu wa kanuni hizo ambazo Mtanzania imeziona, katika uzalishaji mkaa atakayebainika kuzalisha kinyume cha sheria atawajibika kulipa faini Sh milioni 1 hadi Sh milioni 3 au kifungo miezi sita hadi mwaka mmoja au adhabu zote kwa pamoja.

Kulingana na kanuni hizo, ofisa aliyeidhinishwa anaweza kuingia wakati wowote katika majengo ya kuhifadhi, kuuza jumla au rejareja biashara ya magogo, mbao, miti au mkaa kwa ajili ya ukaguzi na ukimzuia unaweza kutozwa faini Sh milioni 1 hadi Sh milioni 2 au kifungo mwaka mmoja hadi miwili.

Atakayebainika kusafirisha magogo, mbao au mkaa kwa matumizi ya nyumbani, atatakiwa kuonesha risiti inayoonesha kuwa alinunua kutoka kwa muuzaji aliyesajiliwa.  

Pia atakayebainika kuuza mazao ya misitu kama vile magogo, mbao, miti au mkaa katika maeneo yasiyosajiliwa atawajibika kulipa faini Sh milioni 5 hadi Sh milioni 10 au kifungo miezi sita hadi 10.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, mtu yeyote ambaye anataka kukata miti kwa ajili ya magogo au uzalishaji wa mkaa kutoka shamba binafsi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani atatakiwa kupata kibali kutoka kijiji au kwa Ofisa Mtendaji wa Mtaa.

Mtu yeyote ambaye anataka kukata miti kwa ajili ya maandalizi au matumizi mengine ya ardhi atatakiwa kupata kibali kutoka kwa Meneja wa Misitu wa Wilaya baada ya idhini ya Kamati ya Wilaya ya Mavuno ya Mazao ya Misitu.

Mtu yeyote anayevunja kanuni hiyo katika kesi ya shamba la kuanzia ekari moja hadi ekari 50 atawajibika kulipa faini Sh milioni 3 hadi Sh milioni 5 au kifungo mwaka mmoja hadi miaka miwili au adhabu zote kwa pamoja.

Ikiwa ni shamba la zaidi ya ekari 50 muhusika atawajibika kulipa faini Sh milioni 10 hadi Sh milioni 12 au kifungo miaka miwili hadi miaka mitano au adhabu zote kwa pamoja.

Uuzaji wa mkaa nje bila kuwa na kibali halali kilichotolewa na waziri atawajibika kulipa faini Sh milioni 5 hadi Sh milioni 10 au kifungo mwaka mmoja hadi miaka mitano.

Usafirishaji wa mazao ya misitu kama vile magogo, mbao, miti na mkaa kwa madhumuni ya kibiashara utafanyika kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni kwa njia zilizoainishwa katika kibali cha usafirishaji.

MATUMIZI YA MKAA

Ripoti ya mazingira ya mwaka 2014 inaonesha Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa matumizi ya nishati ya mkaa ambapo hutumia tani 500,000 kwa mwaka.

Ripoti hiyo pia inaonyesha hekta 372,000 za misitu hukatwa nchini kwa mwaka na asilimia 70 ya nishati hiyo unatumika Dar es Salaam tofauti na vijijini ambako wengi wanatumia kuni zilizokauka na kuanguka zenyewe.

Pia ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha zaidi ya asilimia 73 sawa na familia nane kati ya 10 wanatumia mkaa kama chanzo cha nishati kwa ajili ya kupikia.

Juni mwaka jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, alisema zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa na kati ya asilimia 70 hadi 80 ya miti hukatwa kwa ajili hiyo.

Alisema kama hazitafanyika jitihada za makusudi baada ya miaka 20 hata mkaa ulioko sasa hautakuwepo na nishati ya kupikia inaweza kuwa ghali zaidi kuliko vyakula.

Kwa mujibu wa waziri huyo, asilimia 61 ya nchi imeathiriwa na jangwa kutokana na ukataji miti na hali ni mbaya huku akisema kuwa mkaa hatutaushinda kwa virungu au amri bali kwa kuweka mazingira ya nishati mbadala itakayopatikana kirahisi na kwa gharama nafuu.

Hata hivyo Waziri Makamba alisema wako kwenye mchakato wa kuandaa kanuni ambazo zitapiga marufuku matumizi ya mkaa na kuni kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 300.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles