31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

kibano kampeni Uchaguzi Serikali za Mitaa

Faraja Masinde -Dar es salaam

HUKU vyama vikiendelea na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, huenda wagombea wakajikuta kwenye hatarini wakati kampeni zikiendelea.

Hatua hiyo inatokana na kanuni zinazoendesha uchaguzi huo kuweka vifungu ambavyo mgombea au mwakilishi wake ambaye atatumia jukwaa la siasa kukashifu mgombea mwingine, atachukuliwa hatua za kisheria na msimamizi wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, kifungu cha 27(4) kinatoa mamlaka na sauti ya mwisho  kwa msimamizi wa uchaguzi iwapo vyama vitashindwa kuridhiana kwenye uwanja wa kampeni.

 “Endapo vyama vya siasa vitashindwa kuridhiana wakati wa uunganishaji wa ratiba za mikutano ya kampeni, Msimamizi wa Uchaguzi ataunganisha ratiba ya mikutano ya kampeni na uamuzi wake utakuwa wa mwisho,” kinaeleza kifungu hicho.

Mbali na hilo, kanuni hizo pia zimebainisha masharti ya kufanya kampeni kwa mgombea au chama, huku zikipiga marufuku kampeni za ubaguzi, matusi na zile zinazoweza kuchochea vurugu.

“30 (2) Mgombea au mwakilishi wa mgombea au Chama cha Siasa chenye mgombea hakitaruhusiwa kuendesha kampeni za uchaguzi kwa: (a) kutumia rushwa, (b) kutoa maneno ya kashfa au lugha za matusi, (c) kufanya ubaguzi wa jinsia, maumbile, ulemavu, dini, rangi, kabila au ubaguzi mwingine wa aina yoyote au (d) kutoa maeneo ambayo yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kusababisha vurugu,” ilieleza kanuni hiyo.

Hata hivyo suala hilo linakwenda kuwekewa mkazo na sura ya 11 ya makosa ya adhabu kwa mgombea ambapo kifungu 47 (2) kinasema kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa kosa lolote chini ya kanuni ndogo ya (1) atahukumiwa adhabu ya faini isiyozidi Sh 300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja, yaani faini na kifungo.

Pamoja na hali hiyo kanuni hiyo pia inaeleza masharti ya kupiga kura huku kifungu 35(6) kikipiga marufuku mtu yeyote kutoruhusiwa kubaki eneo la kituo cha kupigia kura baada ya kupiga kura.

SABABU ZISIZOBADILI MATOKEO

Kanuni hizo zimefafanua masuala ambayo kwa namna yoyote hayawezi kubadilisha matokeo ya uchaguzi. Katika kanuni ya 42 imetaja; “(a) Kutokuwapo kwa mgombea au wakala wa mgombea wakati wa kupiga kura, kuhesabu kura au kutangaza matokeo au (b) mgombea au wakala wa mgombea kukataa kusaini fomu ya matokeo.”

Kuhusu makosa ya uchaguzi, kanuni ya 47 inaeleza kuwa mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi endapo, (a) ataharibu orodha ya wapigakura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi, (b) atatoa taarifa za uongo ili aweze kupiga kura au kugombea nafasi ya uenyekiti wa mtaa au ujumbe wa kamati ya mtaa, (c) atajiandikisha au kupiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja.

Hata hivyo baada ya kupiga kura watu wanatakiwa kusimama mita 200 kutoka eneo la kituo ambapo kifungu kinasema; “(f) ataonyesha ishara au kuvaa mavazi yanaoashiria kumtambulisha mgombea au chama cha siasa katika eneo la mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura.

Aprili mwaka huu, wakati wa kikao cha kujadili kanuni na viongozi wa vyama vya siasa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanatoa maoni yenye tija ili kutengeneza kanuni zilizo bora, zitakazosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema Tanzania inaongozwa kwa utaratibu wa demokrasia, hivyo Serikali iliona ulazima wa kutengeneza jukwaa la kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo vyama vya siasa ili kuwa na kanuni bora zitakazoendesha uchaguzi kwa amani na utulivu.

Jafo alisema kutokana na umuhimu wa vyama vya siasa katika uundwaji wa kanuni za uchaguzi, ofisi yake ilipeleka rasimu hiyo mapema kwa wadau ili kuweza kupata muda wa kupitia na kuja na maoni yaliyo bora.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda, alisema watahakikisha wanatengeneza kanuni zitakazojenga taswira nzuri ya nchi kitaifa na kimataifa. Aliomba katika kikao hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa atoe uwianishaji wa kanuni hizo na sheria mpya ya vyama vya siasa ili isijeleta msuguano wakati wa uchaguzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles