31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

kibanio kipya NGO’S

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

Serikali imetoa maagizo nane kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) ambapo imesema ndani ya siku 30 yasipotekelezwa, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuyafutia usajili.

Maagizo hayo yalitolewa jana jijini hapa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Dk. Ndugulile, alisema agizo la kwanza ni NGOs kuwasilisha kwa msajili taarifa za fedha (Audited financial statements) za miaka miwili iliyopita (2016 na 2017), wakati ikijiandaa kutoa taarifa ya mwaka 2018.

Agizo jingine ni mashirika hayo kuwasilisha taarifa za vyanzo vya fedha, matumizi yake na miradi iliyotekelezwa na inayotarajia kutekelezwa kwa kipindi husika.

“Kuwasilisha mikataba au hati za makubaliano ya ufadhili wao kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi sasa, mashirika yote yasiyo ya kiserikali yahakikishe kuwa miradi wanayoitekeleza inazingatia vipaumbele, mipango na mikakati ya Serikali katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya ili kutoa mchango katika kufikia maendeleo endelevu kwa manufaa ya jamii na taifa.

“Mashirika yasiyo ya kiserikali yahakikishe kuwa kabla ya kutekeleza miradi yao ni sharti kuwasiliana na Ofisi ya Msajili wa mashirika ysiyo ya kiserikali ambaye yuko Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto sanjari na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kupata kibali ili kufanikisha jukumu la uratibu, ushirikishwaji na ufuatiliaji wa kazi za NGOs katika ngazi mbalimbali.

Agizo la sita alisema ni NGOs za kimataifa kuzingatia ushiriki wa wananchi na mashirika ya ndani katika miradi zinazotekeleza kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli za NGOs nchini.

Dk. Ndugulile alisema agizo la saba ni NGOs zilizosajiliwa chini ya sheria nyingine, ikiwamo Sheria ya Makampuni Na.12 ya mwaka 2002, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Sheria ya Usajili wa Vyama vya Kijamii, Sura ya 337 ya mwaka 2002 ziombe kupata cheti cha ukubalifu kwa mujibu wa kifungu 11 cha sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2005.

“Kufanya kazi pasipo kusajili chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni kosa kwa mujibu wa sheria,” alisema Dk. Ndugulile.

Agizo la mwisho alisema ni mashirika yasiyo ya kiserikali kutuma taarifa zao za fedha na miradi za kila mwaka kwenye Ofisi ya Msajili wa NGOs.

Akitoa sababu za kutoa maagizo hayo, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku.

“Misingi ya utawala bora pamoja na mambo mengine inasisitiza uzingatiaji wa masuala ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa kila siku, jambo ambalo Serikali imekuwa ikilihimiza na kulitekeleza ipasavyo.

“Tunapenda kufahamisha umma kuwa Serikali inayatambua mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuwa wabia muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa. Kutokana na umuhimu huo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imekuwa ikisajili, kuratibu na kufuatilia mashirika hayo ili kuweka mazingira wezeshi kwa mashirika hayo kutoa mchango katika maendeleo ya jamii na Taifa letu,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001, inasisitiza misingi ya uwazi na uwajibikaji kwa mashirika hayo.

Pia alisema Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Na. 24 ya mwaka 2002 ikisomeka pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2005 katika kifungu cha 29 (a) na (b), mashirika hayo yana wajibu wa kuwasilisha taarifa za kazi na fedha kila mwaka kwa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kwa umma.

“Hata hivyo, takwa hili la kisheria limekuwa halizingatiwi ipasavyo. Vile vile, kanuni za maadili za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Code of Conduct, GN. No. 363, 2008) ambazo zimeundwa kwa mujibu wa kifungu namba 27, zinasisitiza uzingatiaji wa misingi ya uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi, usimamizi wa masuala ya fedha na utawala.

“Hali kadhalika, wanufaika wa miradi hiyo, sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa wanamofanyia kazi na vyombo vya habari wanayo haki ya kupata taarifa za shughuli zao.

“Aidha, NGOs zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sera na vipaumbele vya nchi katika maeneo wanayofanyia kazi.

“Hata hivyo, baadhi ya haya yamekuwa hayazingatii wajibu wao wa kisheria. Hali hii imekuwa ikizusha malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi na baadhi ya wabia wetu wa maendeleo wanaotoa fedha zao kuchangia juhudi za nchi na wananchi kujiletea maendeleo,” alisema Dk. Ndugulile.

 

Machi 29 mwaka 2016, Msajili wa NGOs alitangaza kufuta mashirika yasiyo ya kiserikali 109 kwa kuendesha shughuli zao kinyume cha sheria ya NGOs .

Alisema mashirika hayo ni yale ambayo hayajawasilisha taarifa za mwaka kwa kipindi cha miaka miwili.

Oktoba 2017, Wizara ya Afya, ilitangaza  kukamilika kwa uhakiki kwa NGOs ambao ulianza Agosti mwaka 2017.

Wizara hiyo ilisema jukumu lake ni kusajili na kuratibu shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali kwa mujibu wa sera ya kitaifa ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya mwaka 2001.

Katika uhakiki huo, mashirika yasiyo ya kiserikali 3,186 kati ya mashirika 8,500 yaliyotarajiwa, yalihakikiwa.

Mashirika yasiyo ya kiserikali 2,655 yalisajiliwa chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005 na mashirika 518 yamesajiliwa chini ya sheria nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles