25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

KIBADENI, JULIO WAISHANGAA SIMBA

 

THERESIA GASPER DAR Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MAKOCHA wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ‘King’ na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, wamewashangaa waajiri wao wa zamani kwa kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi katika kipindi hiki pamoja na kuendelea kutoa nafasi kwa makocha wageni.

Hivi karibuni uongozi wa klabu ya Simba, ulitangaza kuachana na Mayanja kwa madai kwamba kocha huyo kutingwa na majukumu yake ya matatizo ya kifamilia hali iliyofanya kusitisha mkataba wake.

Kufuatia hatua hiyo, juzi klabu hiyo ilimtambulisha kocha msaidizi mpya raia wa Burundi, Masud Djuma, aliyekuwa akiinoa Rayon Sports ya Rwanda, kuja kusaidiana na Mcameroon, Joseph Omog.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, Kibadeni alisema ni vizuri zaidi nafasi kama ya kocha msaidizi wangepewa wazawa ili waweze kupata ajira na ujuzi zaidi.

Jambo kama hili linakuwa si la kawaida endapo kocha mkuu amepewa nafasi kocha mgeni ambaye anakuwa na utaalamu mkubwa, hivyo msaidizi anaendelea kupata ujuzi na ingekuwa ni vizuri hata akiondoka wanatuachia faida.

“Mimi naweza kuwasifu Yanga kwa upande wa pili wanawatumia wachezaji wao wa zamani kwani nafasi kama ile wamempa mzawa ambaye anaendelea kuchota ujuzi, hasa mfano kwa sasa Mayanja ameondoka akiwa amepata faida na anapeleka kwao Uganda.”

“Mara nyingi klabu inavyoamua kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi wanaanza na kocha mkuu, lakini si kwa msaidizi, ila sijafahamu kwanini wameamua kufanya hivyo ngoja tusubiri ili tuone na matunda ya kocha huyu kwani ndio kwanza amefika,” alisema Kibadeni.

Upande wake Julio, alisema klabu hiyo haikufanya maamuzi sahihi kumuacha Mayanja katikati ya msimu, kwani jambo hilo litakuja kuwagharimu ukizingatia alishaitengeneza timu kwa kusaidiana na Omog.

“Kumfukuza Mayanja sijapenda kabisa, lakini jamaa ana misimamo yake niseme hizo timu za watu na walimu tupo kwa ajili ya kufukuzwa ameisaidia sana Simba lakini ndio hivyo wamemwondoa.”

Kocha huyo alisema anashangaa timu za Tanzania kuwapa nafasi makocha wa kigeni wakati wapo wazawa wenye uwezo mkubwa.

Alisema makocha wa kigeni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutokujua mazingira hivyo kujikuta wakifanya kazi katika mazingira magumu.

“Timu ikiwa inachukuliwa na walimu wazawa tunawajua kwa sababu wengine wadogo zetu, kwa hiyo tunajua jinsi ya ‘kudeal’ nao sikubaliani kabisa na hizi timu kuwapa makocha wakigeni nafasi hata katika usaidizi,” alisema.

Mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo (jina tunalo), alipoulizwa kuhusu kauli za makocha hao ambao pia waliwahi kuichezea timu hiyo kwa mafanikio alisema jambo kama hilo ni la kawaida kwani mabadiliko hayo yanaweza kuiongezea nguvu zaidi timu.

Alisema mtu ambaye ana majukumu makubwa kwenye kikosi ni kocha mkuu, ambaye bado anaendelea kuinoa timu hivyo hakuna kitu kilichobadilika.

“Kufanya mabadiliko kwenye kipindi kama hiki mbona ni kawaida, mbona Yanga walibadilisha kocha mkuu katikati ya ligi na wakachukua ubingwa wa msimu uliopita, hapa katikati timu ilivyokuwa haipati matokeo mazuri baadhi ya mashabiki walianza kuongea, mimi nawaomba tuendelee kuisapoti timu yetu,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles