30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kiapo ndoa ya Pilipili chatikisa, mwenyewe afurahia tuzo

SWAGGAZ RIPOTA

KITENDO cha mchekeshaji nyota Bongo, Emmanuel Mathias ‘Mc Pilipili’, kubadilisha kiapo cha ndoa aliyoifunga hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kimepokewa kwa mitazamo tofauti kiasi cha kuwagawa watu ambao wanaosema amepatia na wengine wakisema amekosea.

Pilipili na mke wake Philomena, walifunga ndoa Juni 29, mwaka huu katika kanisa la Mbezi Chapel of Baptist kisha hafla kubwa ikafanyika katika ukumbi wa Mlimani City.

Katika kiapo alichoapa Mc Pilipili na mke wake kilikwenda kinyume na vile ambavyo imezoeleka kwamba wanandoa huwa wanaapa kuwa pamoja kwenye nyakati zote za maisha yao hata pale wanapopitia changamoto mbalimbali.

Lakini kwa wawili hao ilikuwa tofauti, katika kiapo chao walikataa kabisa shida, magonjwa, matatizo na mateso na wakaapa kuwa pamoja kwenye nyakati za baraka, uzima na furaha.

Jambo hilo liliwashtua wengi, akiwamo Askofu William Mwamalanga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya Maadili ya dini za Tanzania aliyepinga kiapo hicho kilichofanya ndoa ya Pilipili iwe batili kwa kuwa kipo kinyume taratibu za kuapa.

“Anayewakilisha kiapo cha Mungu atatoa kile kiapo wao hawapokei, utaona siyo kwa mwanamke au kwa mwanamume, ubatili ni mkubwa kwa maana ya ndoa ya Mungu ila kimwili wanaendelea,

“Biblia inasema ndoa na iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumu adhabu, usilete mambo ya uasherati ndani ya nyumba ya Mungu ile ni mizaha, Biblia inasema usiweke mizaha,” anasema Askofu William.

Swaggaz, tukamtafuta Nabii Richard Godwin ambaye  alikuwa msimamizi wa ndoa ya Mc Pilipili, atolee ufafanuzi kwanini mchekeshaji huyo hakuapa kama vile ambavyo imezoeleka.

“Kwanza nirekebishe hili, Mc Pilipili hajabadilisha kiapo, kile kiapo alichoopa kilikuwa sawa kabisa kulingana na utaratibu na imani yake, duniani tuna imani nyingi, sasa usitake kile unachofanya wewe kwenye imani yako kiwe utaratibu kwenye imani yangu,

“Pilipili alikuwa anaamini yeye kwasababu amefunga ndoa siyo mgonjwa, amefunga ndoa siyo masikini, hada shida na matatizo, ni kijana ambaye ndiyo anaibukia kwenye mafanikio sasa kwanini akiri magonjwa na umasikini madhabauni wakati ndiyo anaanza kuwa tajiri?,” anahoji Nabii Richard ambaye ni mwanzilishi wa huduma ya Jehovah Mercy International Ministry.

Aliongeza kwa kusema: “Watu wengi wamekuwa wakiharibikiwa ndoa zao kwa kukiri magonjwa, shida na umasikini kupitia kiapo hiki cha zamani kwa kuwa kile ambacho unakiapa ndiyo ambacho kitatokea kwenye maisha yako, hiki kitu kaka hakifai,

“Usiape umasikini wakati wewe siyo masikini, usiape ugonjwa wakati wewe siyo mgonjwa, Mungu anasema mimi ni Mungu ninayewawazia mema nyakati zenu za mwisho, Mungu hajawahi kumpa mtu umasikini,

“Mimi ni baba yake wa ndoa kwahiyo naomba kusema kuwa ndoa ya Mc Pilipili iwe fundisho kwa mwanadoa wengine, kabla hujaoa nenda kakague kile kiapo kwanza, usiombe matatizo wakati una furaha. Ile ndoa imeandaliwa miezi mitatu kanisani, imefungishwa na watu wenye akili, waliofunga safari kutoka Nairobi kwaajili hiyo”

Wakati hayo ya kiendelea, Mc Pilipili na mke wake wanakula fungate lao visiwani Zanzibar huku akifurahia kutajwa kuwania tuzo kubwa Afrika Kusini za Savanna Comics Choice.

Akiziongelea tuzo hizo Mc Pilipili alisema : Nashukuru ndoa imekuja na baraka, naomba sana muendelee kunipigia kura katika tuzo hizi kubwa za Wachekeshaji Afrika, namna ya kunipigia kura ni kwenda kwenye ukurasa wao wa Instagram @comicschoice na kugusa link utakayoikuta hapo itakuwezesha kunipigia kura.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles