23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya kina Zitto, wenzake kumnusuru CAG yakwama

KULWA MZEE  -DAR ES SALAAM

NAIBU Msajili wa Mahakama Kuu, S.S. Sarwatt,  amekataa kusajili maombi ya kesi iliyotaka kufunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalando),  dhidi ya Spika wa Bunge Job Ndugai,  akipinga uamuzi wake wa kumuita Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad kuhojiwa katika Kamati ya Bunge.

Maombi hayo yaliyowasilishwa Jumatatu wiki hii yalikataliwa jana kwa barua iliyopelekwa kwa Wakili wa muombaji, Fatma Karume.

Barua hiyo iliandikwa na kusainiwa na Naibu Msajili, Sarwatt na sababu za kukataa kusajili maombi hayo ni kwamba kiapo cha Zitto hakikuambatanishwa na wito uliotoka kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kwenda kwa CAG.

Pia hakukuwapo kiapo cha CAG kinachounga mkono maombi hayo na waombaji wengine walitakiwa kuwa na viapo lakini waliondelewa na kubakia mwombaji mmoja, Zitto.

Akizungumzia hilo, Wakili Fatma Karume,  alisema msajili kazi yake ni  kupokea kesi na kupeleka kwa majaji na si kuhoji ushahidi wa kesi kwa sababu  viapo anavyohoji ni ushahidi.

“Akili yangu imevurugika kabisa kwa jambo hili, msajili anataka ushahidi kabla kesi haijafika kwa jaji.

“Kiapo cha Zitto lazima kijibiwe na Spika, anataka wito aliuona wapi, nani kamwambia kuna wito, yupo anayejua kuna wito ndiyo maana anataka uambatanishwe,” alisema.

Akizungumzia hilo,  Zitto  alisema wito ni siri, kutaka kiapo cha CAG ni ujanjaujanja unaotumika kumuingiza CAG kwa jambo lisilomuhusu.

“Tumepeleka malalamiko kwa Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma, kasema yatashughulikiwa, tunatumia Mahakama kupata haki, tunapanda ngazi naamini tutapata uamuzi.

“Kuna njama inafanywa… hili likifanikiwa nchi itaibiwa sana na tutapata hasara wananchi,” alisema Zitto.

Kwa mujibu wa Wakili Fatma,  Jaji Mkuu ameelekeza malalamiko yao yakashughikiwe na Jaji Kiongozi.

Hata hivyo Zitto alisema juzi waliambiwa jalada liko kwa Jaji Kiongozi lakini inashangaza kwa jalada hupelekwa huko baada ya kusajiliwa na si kabla ya kusajiliwa kama ilivyokuwa kwa maombi yao.

Wakati Zitto na wenzake wakitua mahakamani, mnyukano huo umezidi kuchukua sura mpya ambako juzi Spika Ndugai, alitangaza kuwa amewatawanya wajumbe wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Tawala za Mikoa na Mitaa (LAAC).

Ndugai alisema  kwa sasa wajumbe wa kamati hizo  wanafanya kazi kwenye kamati nyingine.

Hatua ya usitishaji huo inatokana na kauli  ya CAG Profesa Assad  aliyoitoa Desemba mwaka jana  kwenye mahojiano na Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda.

Mtangazaji huyo  alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

Katika majibu yake CAG alisema: “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha panapoonekana kuna matatizo hatua zinachukuliwa.

Januari 7, mwaka huu Spika Job Ndugai, alitoka hadharani na kutangaza kusikitishwa na kauli hiyo huku akiagiza CAG Assad afike mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge Januari 21, mwaka huu kujieleza kutokana na kauli hiyo.

Ndugai alidai CAG amedhalilisha Bunge kwa kauli hiyo.

Alimtaka afike siku hiyo kwa hiari yake  akahojiwe vinginevyo atafikishwa mbele ya kamati hiyo kwa pingu.

Licha ya CAG, pia Spika Ndugai, alisema Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 22, mwaka huu.

Alisema CAG Assad, akiwa nje ya Tanzania wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili Redio ya Umoja wa Mataifa (UN), alisema Bunge la Tanzania ni dhaifu.

“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji,  huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi,  na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles