KESI YA KINA MBOWE YAZUA UTATA

0
422

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM


KESI inayowakabili vigogo tisa wa CHADEMA akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, imechukua sura mpya baada ya wakili anayewatetea, Jeremiah Mtobesya, kujitoa akidai kuwa akiendelea na kesi hiyo haki haitatendeka.

Mtobesya alifikia uamuzi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada ya mahakama kuamuru kesi ianze kusikilizwa wakati awali ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kusikiliza uamuzi.

Kabla ya kuanza kubishania kuwa kesi hiyo ianze kusikilizwa ama iahirishwe, mahakama hiyo ilitoa uamuzi wa kuyatupilia mbali maombi ya kina Mbowe ya kutaka kesi inayowakabili iahirishwe mahakamani hapo hadi rufaa iliyopo Mahakama ya Rufaa itakapotolewa uamuzi na maombi ya kusitisha usikilizwaji wa kesi kwenye Mahakama ya Kisutu yatakapotolewa uamuzi.

Akitoa uamuzi wa kuyatupa maombi hayo, Hakimu Mashauri alisema katika kifungu namba 225 (1) (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, hakuna mahali popote ambapo kunaupa nguvu upande wa utetezi kufungua maombi ya kuahirisha kesi hiyo.

Alisema masuala yote yanayohusu Mahakama ya Rufaa yanakuwa chini ya mahakama hiyo.

“Hakuna hoja za msingi zilizowasilishwa, wanakusanya mambo yoyote kwa lengo la kuchelewesha kesi, Mahakama Kuu ilipoyatupa maombi yao ya marejeo haikutoa maelekezo yoyote, haikuzungumzia chochote kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.

“Mahakama Kuu haikutoa changamoto zozote kuhusu uamuzi wa mahakama hii, hivyo mahakama hii haiwezi kula matapishi yake, maombi ya kuahirisha kesi yamekataliwa, safari hii mahakama inayatupilia mbali kabisa ,”alisema Hakimu.

Baada ya hakimu kusema hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai kwamba kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kusikiliza uamuzi.

“Uamuzi tuliokuwa tunasubiri umeshatolewa, shauri hili lilitakiwa kuingia katika hatua ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali, tunaomba kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali sasa hivi, “alisema Nchimbi.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Mtobesya aliyekuwa akiwatete kina Mbowe, alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa hivyo maombi ya upande wa Jamhuri ya kusoma maelezo ya awali hakubaliani nayo.

Akitolea uamuzi wa mabishano hayo, Hakimu Mashauri alikubaliana na upande wa Jamhuri na kuamuru maelezo ya awali yasomwe muda huo.

Alipomaliza kusema hayo, Wakili Mtobesya aliifahamisha mahakama kwamba anajiondoa katika kesi hiyo kwasababu wamekuwa wakiendeshwa na Jamhuri, hivyo akiendelea kuwawakilisha washtakiwa, haki haitatendeka.

Wakili Nchimbi akijibu alidai hawana pingamizi kwa wakili huyo kujitoa, mahakama ilikubali na kuamuru maelezo ya awali yasomwe Agosti 27.

Awali maombi ya kina Mbowe, yalitaka kuahirisha kesi hiyo hadi hapo Mahakama ya Rufani itakaposikiliza na kutolea uamuzi rufani watayowasilisha  kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam wa  kutupilia mbali maombi yao ya marejeo.

Pia, vigogo hao wamewasilisha maombi Mahakama ya Rufani wakiomba kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi hiyo mpaka rufani yao itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Mbowe atoa lawama nzito

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Mbowe alisema hawaogopi kufungwa lakini wanataka wafungwe kwa haki na si kwa kubambikiziwa kesi.

“Mimi nasema wazi kabisa bila woga wowote, kuna dhamira ya kutubambikia kesi ambayo haituhusu, waliomuua Akwilina (Akwilina Akwilini, aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji Dar es Salaam – NIT) wapo na wanajulikana lakini tumesikia maofisa wa polisi kuwa hawana hatia.

“Sasa walioua hawana hatia lakini walioonewa ndiyo wana hatia, sisi hatuogopi jela wala kufungwa lakini tunataka tufungwe kwa haki, waue wengine, wapige risasi wengine wale walioonewa ndiyo wanashutumiwa.

“Tumejitahidi kutafuta haki kupitia njia mbalimbali ndani ya ngazi mbalimbali za kimahakama bado kunaonekana kuna shinikizo ngazi ya Mahakama ya Kisutu.

“Naomba tukubaliane kuwa Chadema tunaheshimu mahakama zetu na hatujawahi kudharau mahakama, lakini kwa namna ambavyo suala letu linapelekwa matamko anayoyatoa hakimu mahakamani, hata mwili na sura yake vyote vinaashiria pengine anafanya kazi kwa shinikizo na maelekezo maalumu.

“Kwa sababu tunaona kabisa jambo hili linapelekwa kasi bila kuthamini kwamba sisi ni viongozi waandamizi wa chama, sisi ni wabunge na Bunge zima la bajeti tulishindwa kwenda kwa miezi mitatu kwa sababu tunakuwa mahakamani.

“Sasa hivi Kamati za Bunge zinakutana hatujaweza kwenda majimboni miezi sita sasa kwa sababu tunakimbilia mahakamni kila siku, saa nyingine inasikilizwa hadi usiku.

“Jambo hili sasa limewachosha mawakili wetu kwa sababu utetezi wao wa kitaaluma unapuuzwa wazi wazi na mahakama na ndiyo imesababisha sasa wakili wetu mmoja kujitoa.

“Ilikuwa kesi inakuja kwa ajili ya kutolewa maamuzi kwamba Mahakama ya Kisutu isiendelee na shauri hili hadi pale ombi letu la kwenda Mahakama ya Rufaa ambayo imeshapangiwa namba isikilizwe lakini hakimu amekataa jambo hili tena kwa maneno ya kubeza.

“Tunalizungumza hili ili Watanzania waelewe, wapigakura wetu waelewe, ubabe unaotumiwa na Serikali na vyombo vya dola kwa wagombea wetu katika chaguzi za marudio.

“Watu wetu wanaumizwa na wanabambikiziwa kesi, madiwani wetu wanalazimishwa kujiuzulu, watu wanapigwa mchana kweupe katika uchaguzi na Serikali inaona, Tume ya Uchaguzi (NEC) inabariki haya, polisi wanasaidia mambo haya.

“Viongozi wakuu wa nchi wanakaa kimya, halafu mnaishangaa Chadema tunakuwa wapole,  sisi tunakuwa wapole kwa sababu tunaipenda amani ya nchi yetu, sitamani kuiona Chadema vijana wanaingia mitaani wanaanza kupigana na kuumizana,”alisema Mbowe.

Aliwataka viongozi wa dini, viongozi wastaafu wa Serikali, wazee na wasomi, waone chuki inavyopandikizwa dhidi ya viongozi wa upinzani.

“Haiwezekani kwa miezi sita haki yetu inanyimwa, hatutaki kusema kuwa hatuna imani na mahakama bali hatuna imani na majaji, hakimu mmoja mmoja ndani ya mahakama.

“Dunia na Watanzania waelewe kuwa hatuoni haki ikitendeka na anavyozidi kuipeleka tunaona kabisa kuna maelekezo na mikakati wafungwe hawa viongozi wa Chadema kwa lengo la kuua demokrasia.

“Awali polisi walisema walioua (Akwilina) ni polisi na wanashikiliwa na baadaye wakaachwa bila kupelekwa mahakama yoyote, lazima tuseme ukweli.

“Upole wa Watanzania na wanasiasa kwamba hawa watu ni wadhaifu kila siku tunawatuliza watu wetu, wanatutaka tususie uchaguzi, tusishiriki na tufanye maandamano lakini tumewaambiwa hapana hiki si chama cha mapambano,” alisema.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine kwenye kesi ya msingi ni  Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee,  Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here