24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi viongozi Chadema yasubiri rufaa ya kina Mbowe

Na PATRICIA KIMELEMETA – Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema inasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani kuhusu dhamana ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, ndipo ipange hakimu mwingine katika kesi ya msingi ya uchochezi inayowakabili viongozi hao na wengine saba wa chama hicho.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.

Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai mahakamani hapo jana kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanasubiri maamuzi ya Mahakama ya Rufaa.

Wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari alidai hawana pingamizi na kwamba rufani iliyokatwa na upande wa mashtaka katika Mahakama ya Rufaa itasikilizwa Februari 18, mwaka huu.

Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina alisema kuwa hadi sasa bado hawajampangia hakimu yeyote kusikiliza kesi hiyo hadi watakapopata majalada ya maamuzi kutoka Mahakama ya Rufaa.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Novemba 23, mwaka jana Jaji Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, alifuta dhamana kwa Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Baada ya maamuzi hayo, washtakiwa hao wakiwakilishwa na wakili Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga maamuzi ya mahakama hiyo ya kufuta dhamana.

Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote, iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na kuiomba mahakama hiyo kuacha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo kwa sababu haina mamlaka.

Baada ya upande wa Serikali kuwasilisha rufaa yao,  kuliibuka malumbano ya kisheria baina ya mawakili wa pande zote, huku mawakili wa kina Mbowe wakiongozwa na Kibatala walipinga uhalali wa taarifa ya Serikali ya kusudio la kukata rufaa kwa madai hawajafahamishwa na Msajili wa Mahakama Kuu kuhusu kuwepo kwa taarifa hiyo.

Jaji Rumanyika alisema kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa na kwamba kunapokuwepo taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.

Jaji Rumanyika alisema mahakama yake imefungwa mikono, hivyo anasitisha usikilizwaji wa rufani hiyo hadi hapo itakapotolewa uamuzi katika Mahakama ya Rufani.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles