30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kenya kukusanya takwimu za watu wenye jinsia mbili

NAIROBI, KENYA

KENYA itakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kukusanya takwimu za watu wenye jinsia mbili  katika sensa yake ya kitaifa inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Katika sensa hiyo inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti itachukua idadi ya raia wake ambao hawajitambulishi kama ni wanaume au wanawake.

Watu wenye jinsia mbili mara kadhaa wanakabiliwa na unyanyasaji na kutengwa na jamii.

Nchini Kenya, inakadiriwa kuna watu zaidi ya 700,000  wenye jinsia mbili kati ya milioni 49.

“Kupata taarifa juu ya watu wenye jinsia mbili kwenye sensa itasaidia watu kufahamu changamoto tunazopitia,” alisema  Ryan Muiruri,  ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Intersex Persons Society of Kenya (IPSK).

“Kujumuishwa kwenye sensa ni mafanikio makubwa kwetu,” aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC.

Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kuweka wazi muingiliano wa watu wenye jinsia mbili kwenye sheria ya kupinga ubaguzi.

Hatua hiyo ya Kenya imekuja wakati ikiwa imepita takribani miaka kumi tangu mwanamke mmoja nchini humo kuamua kwenda mahakamani mwaka 2009 baada ya daktari kuweka kiulizo sehemu ya kujaza jinsia kwenye cheti cha kuzaliwa mtoto wake.

Mwanamke huyo alitaka vitu vitatu: nyaraka ya utambulisho ya mtoto wake kuwa na uwezo wa kwenda shule, sheria kuzuia upasuaji  kwa watoto waliozaliwa na jinsia mbili vinginevyo iwe muhimu kitabibu, na taarifa sahihi ikiwamo msaada wa kisaikolojia kwa wazazi.

Katika hukumu yake mwaka 2014 Mahakama Kuu iliagiza serikali itoe cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo ambaye wakati huo alikuwa na miaka mitano.

Zaidi mahakama ilimwagiza Mwanasheria Mkuu kuunda kikosi kazi ambacho kitaangalia njia za kutoa msaada sahihi kwa watoto wenye jinsia mbili.

Kikosi kazi hicho kilikabidhi mapendekezo yake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwezi Aprili.

Kilipendekeza upasuaji kutofanywa haraka hadi pale watoto wenyewe watakapojiamulia kuchagua wao wenyewe kubaki na jinsia wanayoitaka  na zaidi kupendekeza kufanyika kwa utafiti kubaini idadi yao.

Pia ilipendekezwa alama I itumike kama kitambulisho cha jinsia mbili, na itumike  kwenye nyaraka za umma.

Alama hiyo inatumika kuelezea watu ambao wamezaliwa na tofauti za kibaolojia  katika viungo vyao vya uzazi na ambao hawaeleweki kama ni wanaume au wanawake.

Kuna tofauti nyingi, zinazohusisha viungo vya uzazi, ovari na mifumo ya homoni.

Umoja wa Mataifa unasema kwa mujibu wa wataalamu, kati ya asilimia 0.05 na 1.7 ya watu wanazaliwa wakiwa na sifa ya jinsia mbili.

KISA CHA RYAN MUIRURI

Mwanzilishi huyo wa taasisi ya IPSK, Ryan anasema yeye binafsi alizaliwa akiwa na jinsia mbili, lakini alipewa utambulisho wa kike na akaitwa jina Ruth.

Ryan anasema wazazi wake hawakumkubali  na walikwenda kwa mganga wa kienyeji kwa sababu walitaka kuweka sawasawa kile ambacho watu wengi waliona kama ni mkosi.

“Watu walimcheka mama yangu kwa sababu ya mwonekano wangu, na kuna nyakati nilimwona akilia,” anasema .

Anasema aligundua yupo tofauti alipokuwa na umri wa miaka mitano.

“Siku moja nilikuwa nacheza na watoto wengine, mmoja wao aliniita mimi msichana  na mwingine akasema: “nani kakwambia Ruth  ni msichana?.”

Anasema walimsogelea na kumvua nguo.

Ryan anasema shuleni kila alipokuwa anakwenda chooni watoto wenzake walikuwa wanamfuata kumwangalia kama anasimama au ana chuchumaa.

“Ilikuwa inaniumiza sana na nilikosa raha, kitu kilichokuwa kinaniuma zaidi ni kuitwa mkosi  na wazee wa kijiji  walinishutumu kuleta ukame  ulioikumba eneo letu.

Anasema alitaka kujiondoa uhai mara tano kwa sababu alijiona mpweke na mtu anayekataliwa.

“Siku moja nilipokuwa benki nachukua fedha, mtu anayehudumia dirishani aliita polisi akinituhumu nimedanganya jinsia. Nilijaribu kuelezea hali yangu lakini hakuna aliyenielewa.

Anasema baadae aliamua kuanzisha  taasisi anayoisimamia sasa ili kusaidia watu wenye matatizo  kama yake.

Anasema kuwekwa kwenye sensa jambo hilo ni mafanikio makubwa kwao.

Mwanzilishi wa taasisi ya Intersex Persons Society of Kenya (IPSK), Ryan Muiruri.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles