26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KAULI ZAWAPONZA MWIGULU, IGP SIRRO

Na ASHA BANI

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika utawala  wa Serikali ya Awamu ya Nne, Lawrance Masha, amemshangaa Waziri anayeiongoza wizara hiyo sasa, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro,  kwa kushindwa kuyafanyia kazi matukio ya kutisha yanayoendelea kutokea nchini.

Matukio hayo ni pamoja na mauaji, utekaji na vitisho ambavyo alisema ni mambo mapya kwa Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Masha aliyasema hayo jana mbele ya vyombo vya habari, katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema, akiwa ameongozana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano Uenezi na Mambo ya Nje  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema na Mkurugenzi wa Mafunzo Oganaizesheni wa chama hicho, Benson Kigaila.

Masha, ambaye alikuwa akizungumzia matukio hayo  akilinganisha na uzoefu wake ndani ya Wizara hiyo,  alisema yeye binafsi tayari angekuwa amekwishayapa uzito wa namba moja  matukio hayo na kuanza kuyashughulikia kikamilifu.

“Mimi nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo kulikuwa na tatizo huko Rorya, watu walikuwa wakipigana na kuuana, lakini niliweka kambi huko kubaini tatizo na likapungua kama si kwisha kabisa.

“Ningekuwa leo Waziri hili ndio lingekuwa namba ‘one’ la kulifanyia kazi, kwani wakati huo sisi tuliacha kazi  ofisini na kwenda kusimamia mambo hayo kule Rorya na tulifanikiwa, sasa sijui yeye kwanini amekuwa na ukimya anashindwa kuchukua hatua,’’ alihoji Masha.

Kwa sababu hiyo, Masha amemwomba Rais  Dk. John Magufuli,  kutosita kuwaelekeza watendaji wake katika Jeshi kuomba msaada  wa kimataifa kuja kuchunguza waliomshambulia kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kwani kwa kufanya hivyo si dhambi wala fedheha.

Ili kuthibitisha hoja yake hiyo kama kuomba msaada isichukuliwe ni jambo la aibu, Masha ambaye pia ni msomi wa sheria, akiwahi kuiongoza wizara hiyo kati ya mwaka 2008 hadi  2010,  alihoji mbona makamanda wengi nchini wapo Marekani wakisoma, kwanini waogope kupokea msaada wa uchunguzi wakati si dhambi?

“Ningeomba Rais Magufuli kuwaagiza makamanda wake kuomba msaada ili Watanzania wasiendelee kuishi kwa hofu, si kawaida sisi Watanzania kukuta sehemu moja ndani ya wiki mbili au tatu, maiti 17 zinakutwa zikielea katika Bahari ya Coco Beach,” alieleza Masha, huku akionyesha kukerwa.

Masha ambaye katika vuguvugu la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 alitangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia  Chadema,  alitumia fursa hiyo kumtaka waziri mwenye dhamana kwa sasa, Mwigulu na Jeshi lake kujifunza na kuelewa kwamba ndani ya Jeshi kunatakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuweka pembeni masuala ya itikadi za siasa na dini.

Alisema wakati yeye akiwa Waziri katika wizara hiyo,  mambo ya migogoro ya kidini na siasa kwa hayakusumbua nchi kama sasa  na ilikuwa hata nchi nyingine zikiwaonea wivu Watanzania.

Akielezea athari ya matukio hayo kuachwa hivi hivi, Masha alisema hayaathiri  Watanzania  peke yao, bali hata mataifa ya nje kwa kuwa tayari  mataifa mbalimbali wameanza kuulizana kulikoni Tanzania iko hivi kwa sasa?

“Mtaani huko watu wanaogopa  hata kutoka nje, kutembea usiku na hata kuongea, wanajiuliza ule uhuru tuliouzoea kama Watanzania uko wapi, mbona kuna sintofahamu inaendelea nchini na kwanini.’’

Alisema polisi pia wanatakiwa kuelewa kuwa kazi yao kuu ni kulinda raia na mali zao bila kuangalia itikadi.

Akizungumza kabla ya Masha, kwa upande wa Mrema, alisema anashangazwa na hatua za Jeshi la Polisi kushindwa kuyafanyia upelelezi matukio mbalimbali ya mauaji, utekaji yanayoendelea nchini.

Alisema hadi sasa tayari zimepita siku 695 tangu kuuawa kwa kiongozi wao wa Chadema huko Geita, Alphonce Mawazo, siku 329 kupotea kwa mlinzi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane  na siku 30 za kupigwa risasi kwa Lissu na watu wasiojulikana.

Alisema matukio hayo yote hadi sasa  Jeshi la Polisi hawajaeleza chochote zaidi ya kushikiliwa  kwa gari aina ya Nissan nane zikiwa hazina dereva ambazo zimehifadhiwa kusikojulikana  na madereva wake wasiojulikana.

Alisema matukio hayo yakiwa yanaendelea  viongozi na wabunge wa Chadema wameendelea kutishwa na watu wasiojulikana, akiwamo kiongozi wa Kanda ya Ziwa, Ansbert Ngurumo, Mbunge wa Bunda,  Ester Bulaya, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.

Hivi karibuni, Ngurumo aliandika ujumbe ambao ulisambaa katika mitandao ya kijamii akieleza maisha yake jinsi yalivyo hatarini kutokana  na kazi zake za uandishi wa ukosoaji.

Bulaya inaelezwa alifuatwa nyumbani kwake Bunda na mara kadhaa amelalamika akifuatiliwa na watu ambao hajawafahamu.

“Haya ni matukio ya kuogofya kwa kuwa hata Saanane alitishiwa na kutoa taarifa, Tundu Lissu naye alitoa taarifa kwa zaidi ya wiki tatu pindi akiwa anafuatiliwa na hatimaye akashambuliwa sasa na haya yametolewa taarifa, Jeshi la Polisi kazi yao kufuatilia lakini kimya.

“Aliyekuwa Waziri, Nape Nnauye,  alitishiwa bastola  na baadaye matamko ya Waziri na IGP wanasema ni mtu asiyejulikana wakati alionekana, Lissu risasi hadharani  hakuna kilichofuatiliwa, hivi wako ‘serious’ kweli hawa?” alihoji Mrema.

Kwa upande wake, Kigaila, ambaye alizungumza baada ya Mrema, alilinyooshea kidole Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuwakamata watu wanaoandika mitandaoni na kutoa vitisho.

Aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na mtu mmoja anayejiita Jerry Muro, aliyekuwa mwandishi wa habari, ambaye ameandika ujumbe kupitia mitandao ya kijamii, ambao katika moja ya vipengele vyake vinasomeka … angekuwa yeye ndio Jeshi la Polisi kwa utoto wanaofanya Lema na Nassari angewapoteza.

Kutokana na hilo, alisema  andiko hilo la Jerry litakuwa ni ushahidi tosha kwao endapo wabunge hao watakuja kudhurika mbele ya safari.

Mbali na Jerry, mwingine waliyemtaja  ni Suleiman Othman,  ambaye naye aliandika  kupitia mitandao ya kijamii akimlenga Lissu  kwamba: “Hiyo ni dawa kwa watu wenye siasa kama zake waache mara moja,” akaandika tena: “Naomba ruhusa ya kumuua Lissu, waliompiga Lissu walikosea kwa kuwa hajafa.”

Kigaila hakuishia hapo, alisema kuwa, mtu huyo ambaye wamekuwa wakifuatilia maandiko yake hivi karibuni ameandika vibaya zaidi kuwa, kwanini aliyempiga Lissu amemuacha hai alitegemea asikie amekufa na kwamba, akifika Tanzania mara hii hatafanya makosa.

Alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kuwaacha watu hao pasipo kuwachukulia hatua yoyote kinawatia shaka na kuwafanya wajenge hisia kwamba Serikali huenda ikawa inahusika.

Alisema watu hao wangeandika ujumbe hasi dhidi ya Serikali tayari wangekuwa wameshatiwa hatiani kwa ajili ya kulisaidia Jeshi la Polisi.

“Huyu mtu awe yeye halisi asiwe yeye, lakini tulitegemea kuwa mikononi mwa polisi kwa sasa, ina maana IGP haoni?’’ alihoji.

Alisema kuwa, kuna watu walitupia picha za askari kupigwa risasi Mbagala, lakini waliofanya vile walikuwa Mahenge, hivyo walichukuliwa kutoka Mahenge hadi Dar es Salaam kuisaidia Polisi Makao Makuu.

Pia alishangazwa na tamko la Mwigulu la kusema kuwa gari lililotajwa na Lissu lipo Arusha na wala halijawahi kuletwa Dar es Salaam.

“Jeshi la Polisi halina kifaa cha kugundua magari yanayotembea, hawana kamera za usalama za nchi nzima, sasa Waziri amejuaje au amekuwa wakili wa watuhumiwa?” alihoji.

Kigaila pia alilikumbusha Jeshi la Polisi kuanza upelelezi na walinzi wa wawili wa Kampuni ya Suma JKT waliokuwa wakilinda nyumbani kwa Lissu, kuliko kumtaka dereva ambaye anatibiwa kisaikolojia kwa sasa.

Kwa upande wake,  Lema alimweleza IGP Sirro kuwa nafasi yake haijengwi na kuwa na ghala kubwa la silaha, bali kwa kusema kweli mbele ya bosi wake.

Alisema kutokana na matukio yanayotokea sasa nchini, kama kweli serikali ingekuwa inafuata na kuzingatia utawala wa sheria na Katiba, basi Mwigulu na IGP Sirro wasingekuwa bado wako ofisini.

Alisema juzi walipeleka ushahidi kwa  IGP Sirro wa aliyemtishia bastola  aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,  lakini wanashangaa Jeshi la Polisi kudai kwamba hajulikani.

Alisema kijana huyo amekuwa akionekana mara kadhaa akimlinda Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, lakini baada ya kumwonyesha bado IGP amekaa kimya pia.

“Sasa  sijui Mwigulu na IGP wanafanya nini ofisini hadi leo, anaulizwa anajibu watu wasiojulikana sasa kama hawajulikani na yeye Waziri hajulikani atoke ofisini,’’ alieleza Lema.

Alisema kwa sasa wanaishi kama wakimbizi katika nchi yao, akitolea mfano wa yeye binafsi kwamba  ametishiwa kuuawa na hivi karibuni saa saba usiku alikimbia na kumwacha mkewe akiwa kwenye gari  baada ya kuona wanafuatiliwa na watu wasiojulikana.

Alisema hayo mambo yana mwisho na kama Jeshi linashindwa kufanya kazi yake, basi jamii mwisho wa siku itafanya yenyewe.

“Sisi tuna mwili na tuna damu na ndugu, kama Rais Magufuli, Serikali yake haijui nani anafanya mambo haya, basi yeye mwenyewe hayuko salama pia na nchi haiko salama.’’

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles