27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KAULI YA MWALIMU NYERERE KUHUSU UONGOZI, KATIBA

 

HUU ni mwendelezo wa mahojiano ya Mwalimu Julius Nyerere na waandishi wa habari yaliyofanyika Agosti 16, 1993 nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.

Alitumia fursa hiyo kufafanua hotuba aliyoitoa kwa wabunge mwishoni mwa juma lililokuwa limepita (wakati huo) kuhusu
masuala mbalimbali ya Katiba ya Muungano na uongozi.

Endelea kufuatilia mazungumzo haya.

 

SWALI: Lakini kama unavyosikia watu wanapigapiga kelele. Kwa mfano kama watu watasema Rais Mwinyi ajiuzulu. Nini maoni yako?

JIBU: Rais Mwinyi, mtu yeyote akisema anataka ajiuzulu atataja sababu zake. Atasema sababu hii, sababu hii, sababu hii na raia wote sasa wata-argue (watajadili) kuona kama sababu hizo zina msimamo au sivyo. Mimi nazungumza habari ya Katiba ya nchi yetu. Usifikiri watu sasa … kama wangekuwa wanataka Rais Mwinyi ajiuzulu … mimi nafikiri hawakuelewa hivyo. Mimi nasema tuendeshe nchi yetu kwa mujibu wa Katiba.

Nchi hii iongozwe kwa mujibu wa Katiba. Kama watu wanaiendesha bila mujibu wa Katiba wanadhibitiwa. Tunajitahidi kuwadhibiti. Lakini kusema kweli hili wengi tunalikwepa. Tunataka ku-side (jitenga) pembeni tu. Jambo la msingi ni kujitahidi kuwaambia viongozi wetu kwamba mtaiendesha nchi kwa mujibu wa Katiba. Na mnapoivunja tunawadhibiti. Huu ni msingi wa kuendesha nchi ya watu huru.

SWALI: Kwanini Mwalimu tusiwaambie wenzetu wa Zanzibar kwamba kama ni Muungano basi tufanye Muungano wa serikali moja kuliko kukazania kuwa hawa wanamezwa?

JIBU: Mimi siwezi kusema zaidi ya nilivyokwishasema, nasema mtu mwenye nia njema na Tanzania, tunayo Katiba. Mimi naamini kwamba haina tatizo. Tatizo ni kwamba haitekelezwi. Kama Katiba hii ikitekelezwa kama ilivyokusudiwa, mimi nadhani itatosheleza hali ya kwamba hii ni nchi ya nchi ambazo zilikuwa mbili zikaungana. Inatosheleza kabisa ikitekelezwa.

Mtu mwenye nia nzuri na nchi yetu akisema Katiba hii haitoshi, atasema tuzungumze kwenda kwenye serikali moja. Hazungumzi kwenda kwenye serikali tatu hata kidogo. Serikali tatu itavunja nchi. Lakini nasema serikali moja, kwa sababu nia ya serikali moja ilikuwa ni lazima kukubaliana na Zanzibar. Serikali moja haiwezi kupitishwa tu, sisi tunataka serikali moja.

Kwa sisi ndivyo tunavyotaka Bara. Kwa sababu matokeo yake ni yale yale kama vile serikali tatu zitakavyovunja Muungano. Madai ya serikali moja by (na) Bara peke yake yatavunja Muungano. Kwa sababu sasa mtafanya Zanzibar kuwa koloni. Hamwezi kufanya. Kwa hiyo kama mnataka kwenda kwenye serikali moja, mtaona wote Watanzania kwamba ya nini. Hii kung’ang’ania hapa serikali tatu zinaleta gharama, zinaleta misunderstanding (kutoelewana).

Wabunge hawa, wakati mwingine Bara wanadai kuwa na serikali yao. Kwa nini? Kwa nini tusiungane tukafanya serikali moja? Nimesema hivyo katika Bunge. Lakini hata mkikubaliana bado nawaambia watu wenye nia nzuri watasema, lakini kweli Wazanzibari tutawafanya kama Lindi. Wana watu laki tano.

Lindi nayo ina watu laki tano. Hivi kweli nchi yenye watu laki tano, hata kama mkikubaliana kwa nia njema tu na Wazanzibari, nasema watu wenye busara watasema msiifanye Zanzibar kama Lindi. Na Zanzibar bado representation (uwakilishi) yake kwenye Bunge itakuwa tofauti na representation ya Lindi. Watu watakuja kuuliza baadaye mbona hawa Wazanzibari wako watu laki saba, wana watu wengi katika Bunge hili kuliko Lindi. Maelezo yatakuwa ni historical (ya kihistoria). Na ndivyo ilivyo duniani kote.

Wataambiwa kuwa huko nyuma nchi hizi zilikuwa mbili—Zanzibar na Bara. Haya ni matokeo ya hayo yaliyoziunganisha nchi hizo mbili. Wataelezwa hivyo. Kama tunavyoelezwa sasa Zanzibar kuwa na serikali yake pamoja na Zanzibar sasa hivi ndani ya Bunge ina representation ya peke yake. Ni tofauti kabisa na wengine. Hivyo bado hata kama mki-move kwenye serikali moja bado mtasema Zanzibar bado haina budi itendewe tofauti na Lindi. Lakini jambo mnalizungumza kama watu wazima wanavyoendesha nyumba yao, siyo kama bwana mkubwa mmoja anasema tumechoka na watu hao sasa tuwameze hasa. Haiwezekani. Haiwezekani hata kidogo.

SWALI: Mwalimu umesisitiza sana suala la kufuata Katiba. Lakini mimi naona ukija kwenye suala hili utaona kwamba ni vigumu sana kudhibiti kama Rais akiamua kuwa dikteta. Kwa mfano, pale bungeni wabunge wanaweza kudadisi suala kwa undani linachukuliwa kijanjajanja. Na kunachukuliwa uamuzi wa kupiga kura na mle kuna mawaziri, wakuu wa mikoa na wabunge wa Taifa. Kwa hiyo unakuta mara zote serikali inashinda tu—kama hili suala la OIC kule Dodoma. Ingawa wabunge walidadisi sana, lakini serikali hatimaye ilishinda na ikawaacha wabunge na malalamiko yao. Sasa ni vipi utawadhibiti madikteta?

JIBU: Mimi nasema hivi bwana, tunazungumza hapa sasa hivi, lakini msifikiri kwamba mambo haya mimi kuyazungumza ni rahisi sana kuyasema kama hivi. Rais Mwinyi ni successor wangu (kachukua madaraka kutoka kwangu). Na nilipokuwa natoka niliwaelezeni sifa zake. Anazo sifa nyingi. Moja nilisema ni mpole sana. Sidhani kama nilisema ni mpole mno, nilisema ni mpole sana.

Na hiyo nasema mpaka sasa ni mpole sana. Na mambo ya nchi hayapendi upole sana. Siku nyingine lazima uwe rough (madhubuti) na watu—hasa wahalifu. Rais ni mpole. Rais Mwinyi kwa vyovyote vile hawezi kuwa—huwezi kum-accuse (shutumu) kwa dictatorship (udikteta). Unaweza kum-accuse kwa kitu kingine. Udikteta hata kidogo. Hakuna mtu anayemjua yeye, akasema sasa niko mbele ya dikteta. Actually (kwa kweli) mimi, mtu angeweza kusema huyu … Mimi wangenionea, lakini wangeweza kufanya hivyo. Lakini Rais Mwinyi hapana.

Ila nawaambieni. Nawaambieni kuwa njia kubwa ya kuzuia udikteta ni kuongozwa na sheria. Na hamwezi kuongozwa na sheria kama hilo linakuwa siyo wito wa Taifa. Taifa zima linaelewa. Ni taifa la watu huru, na kwamba wote ndivyo wanavyosema. Na wale viongozi wanapokiuka, wanakemewa na taifa bila woga. Na mimi sidhani kama jitihada zangu zote hizi ilikuwa ni kujenga Taifa la watu waoga sana. Haikuwa nia yangu. Kama inatokea hivyo, basi nasema Mwenyezi Mungu anisamehe.

Sasa kwa hiyo msingi wa kwanza kabisa ni kuona kwamba viongozi wetu wanatutawala, wanatuongoza kwa kufuata sheria. Sheria zinawabana hivyo. La pili ni kuona kwamba viongozi wetu wanatuongoza kutokana na maamuzi ya vikao. Ndiyo maana ya demokrasi. Maamuzi ya demokrasi yanatokana na vikao.

Ziko tabia mbili sasa hivi. Moja, ni kujaribu kukwepa vikao. Sasa kwa mfano, jambo la kuamua suala la OIC lisizungumzwe kwenye vikao. Mimi najua Rais alishauriwa hivyo na watu wasiopenda mazungumzo haya (ya vikao). Sasa tabia hii isizoewe ya kuzuia vikao kuzungumza. Ndiyo maana hata katika Bunge, wakati tunazungumza, na kwamba Mwalimu pengine ingekuwa vyema ungekuja katika Bunge. Lakini hata kidogo. Isiwe kwamba ni mbinu za ujanjaujanja mimi nizuie wabunge kusema mambo haya. Hata kidogo. Tuzungumze tu mambo haya.

Mambo ya nchi lazima yazungumzwe waziwazi katika vikao rasmi vilivyowekwa. Hivyo, lazima jitihada kwamba tunasimamia tusimamie. Nchi yetu inaendeshwa na Katiba. Maamuzi makubwa ya nchi yanatokana na vikao. Central Committee (Kamati Kuu) kwenye Chama, National Executive (Halmashauri Kuu ya Taifa) maana Chama hiki ndicho kinachotawala. Na mpaka sasa kila nikitazama sioni kingine, ni hicho hicho.

Basi chama hicho kiendelee kuwa na tabia ya kuwa maamuzi yake yanafahamika katika vikao. Kwani kwa sasa hivi maamuzi ya chama hicho bado ni kitu kizito sana. Sasa Central Committee inazungumza mambo, National Executive inazungumza mambo, lakini kuna ujanja wa kuepusha mazungumzo. La Makamu (wa Rais) liliepushwa. La OIC nadhani halikufikishwa kabisa. Nadhani halikufika kabisa kabisa.

Na Bunge lilipotaka kuzungumza ikawepo janjajanja ya kuwatoa pale. Hizi ndizo dalili za dictatorship. Na lazima zikemewe. Hapana kuwa na uamuzi wa janjajanja hivi. Nchi haiongozwi kwa ujanja hata kidogo. Nchi inaongozwa kwa msimamo. Inaongozwa kwa taratibu zinazojulikana kabisa kabisa. Watu wanakutana katika Central Committee wanaelewana, wanatenda jambo. Na kama kuhitilafiana, wanahitilafiana saaana katika jambo la msingi. Wengine wana-resign (jiuzulu). Ndiyo. Waziwazi kabisa na wanaeleza kwa nini wana-resign.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles