23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KAULI NNE TATA MWANAFUNZI UDSM ALIYETOWEKA

MWANDISHI WETU


IKIWA zimepita siku saba tangu kutolewa taarifa za kutoweka kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kabla ya kupatikana Mafinga wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa, kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa umma na watu wengine zimeongeza utata wa mazingira ya tukio hilo.

Mpaka sasa, baadhi ya watu waliotoa kauli kuhusu tukio hilo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Pamoja na viongozi hao, wengine waliotoa kauli na matamko ni mtandao wa TSNP pamoja na baba mdogo wa Nondo.

TSNP waliitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumza kupotea kwa mwenzao huyo ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limeeleza kuwa limemrejesha Nondo Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi lakini bado hajafikishwa mahakamani, wala yeye mwenyewe kutoka hadharani kueleza ni nini hasa kilichomsibu.

Kauli tata

Juzi, Waziri Mwigulu, akiwa mkoani Singida alitoa kauli iliyoonyesha kuwa ana wasiwasi juu ya mazingira ya kupotea kwa Nondo.

Waziri Mwigulu alikuwa akizungumza katika hafla ya kuzindua Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Dk. John Magufuli.

“… Ndiyo maana tunaona vinyago vinyago vingi, ..kama hivi juzi anatokea kijana mdogo anasema ametekwa, eti ametekwa akapata na muda wa kutafuta pa kula na nguo za kubadilisha kule anapokwenda.

“Unatoa wapi muda wa kujiandaa? ni vitu vya kiajabu ajabu, watu wanatafuta namna ya kuchafua taswira ya nchi yetu,” alisema Waziri Mwigulu.

Kabla ya kauli hiyo ya Waziri Mwigulu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Bwire alikaririwa na vyombo vya hahari akieleza kuwa Nondo alipatikana Mafinga wilayani Mufindi.

“Baada ya kumhoji Nondo alisema alitekwa na watu wasiojulikana ambao walimtekeleza Wilaya yi Mufindi.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi kama ametoa taarifa za uongo kwa nia ovu kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake kuleta uvunjifu wa amani nchini, tutamshughulikia kama wahalifu wengine na kama kweli atakuwa ametekwa tutawasaka wahalifu,” alikaririwa Kamanda Bwire.

Taarifa ya awali kuhusu kupotea kwa Nondo ilitolewa na Ofisa Habari wa TSNP, Hellen Sisya katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Sisya alisema walianza kupata shaka kuwa Nondo amekubwa na tatizo baada ya kuona anajitoa kwenye makundi mbalimbali ya mtandao wa kijamii wa whatsapp.

Alisema Nondo alianza kujitoa kwenye makundi hayo Machi 7 mwaka huu kati ya saa 6:00 na 8:00 usiku hali iliyozua taharuki miongoni mwao hivyo kulazimika kutaka kufahamu kilichomsibu.

“Tulivyojaribu kumtafuta kwa namba yake ya simu ilikuwa inaita bila kupokewa. Ilipofika saa 9 usiku alituma ujumbe mfupi kwa Mkurugenzi wetu wa Idara ya Sheria, Paul Kisabo, ujumbe ulisomeka ‘Am at risk.’

“Jitihada za kumpigia simu ziliendelea bila mafanikio hadi muda huu. Tulichukua jukumu la kutafuta mawasiliano ya watu wa karibu chuoni alipokuwa akikaa ambapo walitutaarifu kuwa tangu alipoondoka saa saba mchana hajaonekana tena na aliaga anakwenda kwao Madale,” alisema Sisya katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Kauli nyingine ni iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kutangaza kupatikana kwa Nondo.

Makonda alisema amesikia taarifa za kutekwa kwa kijana huyo na kuwataka polisi Mkoa wa Iringa wakimaliza taratibu zao za kumuhoji wamlete Dar es Salaam.

Alisema taarifa za kijana huyo kutoweka ziliibuka wakati chuo kimefungwa wanafunzi wakiwa wanarudi nyumbani.

“Juzi nilisikia kuna mtu mmoja eti ametekwa, nafikiri Iringa wakimalizana naye wamlete Dar es Salaam, asitake kutuchafulia sifa ya mkoa wetu. Halafu waandishi wa habari wanaandika tu bila kuwa na uhakika.

“Shule zilikuwa ndiyo zimefungwa na wanafunzi wanarudi nyumbani, kwa hiyo hata mtandao ukikosekana tu kidogo mtu amepotea au ametekwa? Halafu mnaitisha waandishi wa habari kutoa tamko?” alieleza kwa mshangao Makonda.

Aliwataka waandishi wa habari kuchuja taarifa za kuufukishia umma, zile ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika ziwekwe pembeni kwa sababu zinaweza kuibua taharuki isiyokuwa na msingi.

Taarifa nyingine zilizoongeza utata zilitolewa  kwenye mitandao ya kijamii za mtu aliyedai kusafiri na Nondo wakitumia gari la Kampuni ya Newforce.

Hata hivyo mawakala wa gari hilo mkoani Iringa walilieleza Mtanzania kuwa basi la mwisho la kampuni hiyo hupita Iringa saa 9 alasiri.

Mmoja wa mawakala hao alisema, “muda  ambao inasemekana mwanafunzi  huyo alijikuta yupo Mafinga katekelezwa ni saa  moja asubuhi. Basi letu kutoka Mbeya hata Makambako linakuwa halijapita na yale ya Ubungo hupita huku alasiri,” alisewa wakala huyo ambaye jina lake tumelihifadhi.

Utata wa kauli hizi ni pamoja na namna mwanafunzi huyo alivyojikuta akiwa Mafinga, majira ya saa moja jioni huku siku iliyopita alikuwa Dar es Saalam kama walivyodai wenzake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles