24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

KANUNI MPYA ZA USAFIRISHAJI ZITAPUNGUZA AJALI BARABARANI?

Ajali ya barabarani

 

 

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MATUKIO ya ajali za barabarani yamekuwa na athari nyingi hapa nchini kiuchumi na kijamii kwani yamewasababishia wananchi madhara makubwa yakiwamo kupoteza maisha, majeraha, ulemavu wa kudumu, mali kuharibika na kuacha familia nyingi zikiwa tegemezi baada ya kuondokewa na watu wanaowategemea

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO), ajali za barabarani zinaendelea kupoteza maisha ya watu wengi ambapo watu milioni 1.25 hufariki kila mwaka huku sehemu kubwa ya vifo na madhara ya ajali hizo zikitokea Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Hali ya Usalama Barabarani Duniani iliyotolewa na WHO mwaka juzi, inaonyesha ajali za barabarani ndizo zinaongoza katika vifo vya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 29.

Pia inaonyesha asilimia 90 ya vifo vya ajali za barabarani vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na kati, japokuwa wana asilimia 54 ya magari duniani.

Mkuu wa kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza WHO, Etienne Krug, anasema kiwango cha juu kabisa cha vifo vya ajali za barabarani kipo barani Afrika, ikifuatiwa na Mashariki ya Kati.

Afrika ina asilimia mbili pekee ya magari duniani lakini ina kiwango cha juu cha vifo vya barabarani.

Ripoti hiyo inaonyesha ajali za waendesha baiskeli na watembea kwa miguu zinafikia asilimia 26 ya vifo vyote vitokanavyo na ajali za barabarani, ambapo idadi hii inafikia asilimia 33 barani Afrika.

Hali ilivyo nchini

Takwimu za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani zinaonyesha kuanzia mwaka 2013 hadi Desemba 2015, zilitokea ajali 46,536 huku kundi lililoongoza kwa kuathirika na matukio ya ajali likiwa ni la abiria.

Katika kipindi hicho watu 3,444 walipoteza maisha huku majeruhi wakiwa ni 20,181. Kundi la watembea kwa miguu linafuatia kwa kusababishiwa vifo vya watu 3,328 na majeruhi 8,256 kutokana na ajali za barabarani.

Wapanda pikipiki ni kundi la tatu likiwa na vifo vya watu 2,493 na majeruhi 10,702. Kwa upande wa baiskeli vifo vilivyotokea ni 1,071 huku majeruhi wakiwa ni 2,060. Madereva waliofariki ni 813, majeruhi ni 3,157.

Wasukuma mikokoteni 81 walifariki katika kipindi hicho huku waliojeruhiwa wakiwa ni 246.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, anasema: “Taifa linasikitishwa na matukio ya ajali zinazotokea kila mara, ajali nyingi husababishwa na uzembe wa madereva.”  

Chanzo cha ajali

Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi nchini, ajali nyingi zinatokea kwa sababu ya makosa ya kibinadamu hasa uzembe wa madereva kutotii sheria na kanuni za barabarani, mwendokasi, matumizi ya vilevi, ubovu wa barabara na ubovu wa vyombo vya moto.

Takwimu hizo zinaonyesha asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na uzembe wa madereva, asilimia nane husababishwa na ubovu wa barabara wakati ubovu wa vyombo vya moto husababisha ajali kwa asilimia 16.  

Mikakati ya Serikali

Kwa kiasi kikubwa ajali nyingi zinaepukika kama madereva na watumiaji wengine wa barabara watatii sheria na kanuni za usalama barabarani.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, nchi 17 zimekuwa na mafanikio kwa kuweka sheria za usalama barabarani.

Baadhi ya nchi kama vile Sweden, Uingereza, Uholanzi na nyingine wameweza kupunguza viwango vya vifo vya barabarani kwa zaidi ya asilimia 80 kwa kutekeleza hatua kadhaa zinazoeleweka vyema.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imekuwa na mikakati mbalimbali ya kupunguza ama kutokomeza kabisa ajali za barabarani ambapo imetengeneza kanuni na taratibu ambazo zinalenga kuinua ubora wa huduma, usalama na nidhamu katika utoaji huduma na kuainisha adhabu kulingana na makosa husika.

Kanuni hizo zimetungwa baada ya Sheria namba tisa ya mwaka 2001 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Sheria namba moja ya mwaka 1973 inayohusu leseni za usafirishaji kufanyiwa marekebisho mwaka jana.

Miongoni mwa kanuni hizo ni Kanuni ya Usafirishaji Magari ya Abiria ambayo imezua mjadala mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa usafirishaji wakiwamo wamiliki wa mabasi.

Hivi karibuni Sumatra iliitisha mkutano wa wadau kujadili rasimu za kanuni hizo kwa kina na kutoa maoni kwa lengo la kuziboresha kabla ya kuanza kutumika rasmi.

Mkurugenzi wa Sheria Sumatra, Leo Ngowi, anasema kanuni hizo zinahusu utaratibu utakaotumika kufanya maombi ya leseni, masharti ya leseni za usafirishaji, kufutwa ama kusitisha leseni pindi msafirishaji akikiuka masharti, utoaji tiketi kwa abiria, utoaji risiti kwa mzigo wa abiria na vifungu vya sheria.

“Kanuni zimejikita katika kutoa huduma kwa makampuni zaidi, magari ni lazima yawe na vidhibiti mwendo na gari likipata itilafu usafiri mbadala upatikane ndani ya saa mbili. Msafirishaji anatakiwa atoze nauli iliyoidhinishwa na kuanzia sasa abiria anaweza kukata tiketi mwaka mmoja kabla ya safari,” anasema Ngowi.

Baadhi ya maboresho yaliyoainishwa katika kanuni hizo ni umri wa madereva ambapo dereva wa mabasi ya mjini atatakiwa kuwa na umri kati ya miaka 25 – 60, mabasi ya shule (30 – 60), masafa marefu (30 – 60) na anayeendesha umbali wa zaidi ya saa nane atatakiwa kuwa na wasaidizi.

Viwango vya adhabu vimepandishwa kutoka Sh 50,000 na Sh 100,000 za zamani kwa kosa moja, hadi Sh 200,000 na Sh 500,000 kwa kosa.

Kifungu namba 37 kinachozungumzia makosa na faini kinaonyesha msafirishaji akitiwa hatiani anaweza kulipa faini kati ya Sh 200,000 hadi Sh 500,000 ama kifungo kati ya mwaka mmoja hadi miwili au adhabu zote kwa pamoja.

“Kuna kipengele kinachompa uhuru msafirishaji kwenda mahakamani lakini kama ukikiri kosa unalipa nusu ya faini kama ni 200,000 basi utalipa Sh 100,000. Abiria anaruhusiwa kusafiri na mzigo wa kilo 20 na kama ukizidi msafirishaji anatakiwa kuwa na mzani wa kupima na kutoza uzito uliozidi. Atatakiwa kutoa risiti na kadi ya kufunga mzigo,” anasema.

Kanuni hizo pia zimebainisha kuwa safari yoyote itakayochukua zaidi ya saa 12 lazima kuwe na madereva wawili wa kupokezana ili kuongeza umakini kudhibiti ajali zinazotokana na uchovu wa madereva.  

Maoni ya wadau

Hata hivyo, wadau wa sekta ya usafirishaji nchini wanapinga kanuni hizo kwa madai kuwa zinawakandamiza kwani hazijaainisha makosa ya dereva na mmiliki wa chombo cha usafiri.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (Taboa), Enea Mrutu, anasema kuelekeza adhabu zote kwa mmiliki hakutasaidia kupunguza ajali na kupendekeza kanuni zitenganishe makosa kati ya mmiliki na dereva.

“Kama makosa hayakutenganishwa tutakwenda mahakamani na ikishindikana tutaondoa mabasi barabarani. Huu ni uonevu kanuni za namna hii hazitekelezeki,” anasema Mrutu.

Naye Mjumbe wa chama hicho, Ibrahim Awadhi, anasema mambo mengi yaliyopo katika maboresho ya kanuni hizo si mapya, isipokuwa ongezeko la viwango vya faini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, anasema makosa mengi husababishwa na madereva na makondakta hivyo waainishiwe makosa yao na kulipa faini zinazowahusu.

Wadau hao wanapendekeza umri wa madereva uanzie miaka 20 ili kutoa fursa za ajira kwa vijana kwani wakifunzwa vizuri wana uwezo hata wa kuendesha masafa marefu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC), Oscar Kikoyo, anashauri kanuni ndogo ziongezwe hasa zinazowahusu watu wenye ulemavu kwani wamesahauliwa katika rasimu hiyo.

“Mtu mwenye ulemavu anaweza kupanda kwenye basi akaambiwa alipie kiti chake lakini kile ndiyo kama miguu yake sasa kwenye kanuni hizi kama hilo halipo anaweza kujikuta akilipia,” anasema Kikoyo.

Kwa ujumla kanuni nyingi zilizokuwapo awali zimepitwa na wakati na kumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani kutokana na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na wasafirishaji wasiozingatia maadili ya kazi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles