25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Kamwele awafukuza Wachina kwa kukiuka mkataba

Na Mwandishi Wetu, Chunya

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amewafukuza kazi na kuwataka kuondoka nchini mara moja wafanyakazi wawili wa Kampuni ya China New Railway 15 Bureau Group Corporation inayojenga  barabara ya kilomita 39 kwa kiwango cha lami kutoka Chunya hadi Makongolosi kwa kukiuka mkataba na kuwadhalilisha wafanyakazi.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Matundasi, Kamwelwe ambaye yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, aliwataja wafanyakazi hao ni Meneja mradi huo, Pen Pong na Meneja Rasilimali Watu, Liun Migun.

Alisema mameneja hao licha ya kukiuka vipengele vya mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo, pia wanatuhumiwa kuwapiga na kuwafukuza kazi wafanyakazi wazawa kwa uonevu.

“Haiwezekani Serikali ikamvumilia mkandarasi asiyezingatia mkataba na anayedhalilisha wananchi ambao ndio walipakodi zinazotumika kumlipa, nawaonya wakandarasi wote nchini kuzingatia mikataba na kutenda haki kwa wafanyakazi wao,” alisema.

Kamwelwe alisema mkandarasi huyo amekiuka mkataba kwa kuwa alitakiwa awe na mitambo 75 kwa ajili ya ujenzi, lakini hadi sasa ni 34 tu inayofanya kazi.

Pia alisema alipaswa kuwa na wataalamu saba, lakini hadi sasa ni watatu tu ndio wanaofanya kazi licha ya kulipwa asilimia 15 ya malipo ya awali.

“Natoa miezi mitatu kwa kampuni hii kujirekebisha na kuzingatia mkataba kabla hatua nyingine za kisheria hazijachukuliwa,” alisema.

Kamwelwe alisema ujenzi wa barabara hiyo ulitakiwa kuanza Oktoba 30, mwaka jana na kukamilika Januari 2020, lakini hadi sasa imejengwa kwa asilimia 13 badala ya 20 zilizokubaliwa katika mkataba.

Katika hatua nyingine, alitoa mwezi mmoja kwa Kampuni ya China Civil Engineering Corporation (CCECC) inayojenga barabara ya kilomita 74.1 kutoka Mafinga hadi Nyigo na ile ya kilomita 63.8 kutoka  Nyigo hadi Igawa kukamilisha ujenzi huo  kwa mujibu wa mkataba.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Iringa, Daniel Kindole, amemuhakikishia Kamwelwe kuwa ujenzi huo uko katika hatua za mwisho na utakamilika kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles