25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kamusoko, Niyonzima ngoma nzito Yanga

harunaaNA MICHAEL MAURUS, ZANZIBAR

THABAN Kamusoko na Haruna Niyonzima, wamezidi kuwagawa mashabiki wa Yanga kutokana na aina ya uchezaji wao, madhara yao kwa timu pinzani na mchango wao kwa ujumla kwa timu bila kujali ugumu na urahisi wa mechi.

Kwa siku za hivi karibuni, Kamusoko ametokea kuwateka wapenzi wengi wa Yanga kutokana na aina ya uchezaji wake, akiwa na nguvu, akili ya mpira, mbinu na pia ni mfungaji mzuri.

Katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, Kamusoko alitokea kuwa mkombozi wa Yanga kwa kufunga mabao muhimu, lakini pia kutoa pasi maridadi za mabao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya mashabiki wa Yanga waliamini kuwa kiungo huyo kutoka Zimbabwe ‘anatosha’, kwamba hawakuwa na haja ya kuwa na Niyonzima anayedaiwa kupenda ‘kucheza na jukwaa’ hata pale timu inapotafuta ushindi, tofauti na mwenzake huyo anayeelezwa kuwa si wa kuremba awapo uwanjani.

Imani hiyo ipo kwa wapenzi wa Yanga na hata viongozi wao, pale Niyonzima alipochelewa kuripoti kambini alipokuwa amekwenda kwao Rwanda kwa ajili ya mapumziko wakati ligi iliposimama kupisha mechi za kimataifa kwa timu ya Taifa, kiungo huyo alisimamishwa na mwisho wa siku kutangazwa kutimuliwa Jangwani.

Sambamba na hilo, uongozi wa Yanga ulimtaka Mnyarwanda huyo kuilipa klabu hiyo kwa kukiuka makubaliano yao ya kimkataba, akiwa kama mwajiriwa na Wanajangwani hao.

Kitendo cha Niyonzima kusimamishwa na baadaye kufungiwa, kilipokewa kwa hisia tofauti, baadhi ya watu wa Yanga wakisapoti, huku wengine wakipinga.

Wanaosapoti wamekuwa wakidai kuwa kiungo huyo ni msumbufu akiwa na kawaida ya kuidengulia klabu yao lakini pia kwa uwepo wa Kamusoko, wasingekuwa na shida ya kumvumilia.

Kwa wale wanaoendelea kumtaka Niyonzima awepo Jangwani, wanaamini kiungo huyo ana vitu adimu ambavyo timu yao ingevikosa kwa kuondoka kwake.

Wakati hayo yakiendelea, kumeibuka mjadala mpya juu ya viungo hao wawili.

Mjadala huo ulianzia katika mechi ya Kombe la Mapinduzi kati ya Yanga na Mtibwa kwenye Uwanja wa Amaan, ikidaiwa kuwa Kamusoko hakucheza vizuri na kujikuta akifunikwa na viungo wa wapinzani wao hao japo walishinda kwa mabao 2-1.

Pia, ilidaiwa kuwa Mzimbabwe huyo hakung’ara walipoivaa Azam kwenye michuano hiyo katika sare ya bao 1-1 kama ilivyokuwa Jumapili iliyopita dhidi ya URA.

Mwisho wa siku, baadhi ya mashabiki wa Yanga wamekuja na jibu la kwamba Kamusoko inaonekana ni mchezaji wa mechi ndogo, wakitolea mfano jinsi alivyowasumbua Mafunzo, lakini akishindwa kufanya hivyo dhidi ya Mtibwa, Azam na URA.

Hatimaye baada ya kutolewa kwa Yanga na URA kwenye Kombe la Mapinduzi, baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wameanza kuutaka uongozi wao kumrejesha kikosini Niyonzima ambaye huwa anang’ara katika mchezo wowote bila kujali kama ni dhidi ya timu ngumu au la.

Mashabiki hao wanaamini Kamusoko na Niyonzima wanaweza kucheza pamoja kwa mafanikio makubwa, mmoja akiwa katikati kama kiungo namba nane na mwingine akitokea pembeni hasa upande wa kushoto

Tayari imedaiwa kuwa Yanga ipo katika mchakato wa kumrejesha kundini Niyonzima, ambaye imeelezwa ameanza mazoezi kivyakevyake kujiweka fiti baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

MTANZANIA liliwasiliana na Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha kuzungumzia hatima ya Niyonzima ambapo alisema: “Tatizo halipo kwetu bali ni kwa mchezaji mwenyewe ambaye anaonekana hajitambui.

“Akiwa kama mwajiriwa wa klabu ya Yanga, alitakiwa kuheshimu mkataba na kuzingatia taratibu za mwajiri wake, lakini pamoja na hatua zilizochukuliwa na klabu, hadi sasa hajaomba radhi. Sasa hatuwezi kulea mambo kama haya, kila mchezaji bila kujali nafasi yake katika timu, anatakiwa kufuata taratibu na kutovunja makubaliano yaliyo katika mkataba,” alisema.

Alipoulizwa iwapo wana mpango wa kumrejesha kundini, Tiboroha alishindwa kulithibitisha au kukana juu ya suala hilo, akisisitiza kuwa hawawezi kuwalea wachezaji wasiojitambua na wasumbufu hata kama watapata shinikizo kutoka kwa mtu yeyote yule.

MTANZANIA lilimtafuta Niyonzima kwa simu jana asubuhi kuzungumzia suala hilo, lakini kwa muda wote simu yake iliita bila kupokewa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles