31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kamanda Shana: Wapinzani si watu wa vurugu, ni watu wazuri

BENJAMIN MASESE Na FATUMA SAID-MWANZA

ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Jonathan Shanna, amesema wapinzani ni watu wazuri ndiyo maana katika muda wote aliokuwa bosi wa polisi kwenye mkoa huo, hawakuwahi kurushiwa mabomu na jeshi hilo.

Kamanda Shana ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Operesheni, aliyasema hayo jana wakati akimkabidhi ofisi Jumanne Muliro ambaye ndiyo RPC mpya wa Mkoa wa Mwanza.

Alisema  kati ya vitu anavyojivunia  katika uongozi wake ni kutolalamikiwa ama yeye kuwalalamikia  viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari ambao kwa pamoja walimpa ushirikiano wa karibu na kupata taarifa nyeti.

Shanna alisema viongozi wa siasa hasa wapinzani, wanachukuliwa ni watu wa vurugu lakini alisisitiza ni watu wazuri unaposhirikishana jambo na kukubaliana.

Alisema hakuna haja ya kurushiana mabomu kwa sababu  yeye tangu aingie  Mkoa wa Mwanza  haijawahi kutokea bomu likarushwa kwa wanasiasa, bodaboda, machinga wala watu wengine.

“Kutoka moyoni  kwangu na nayasema maneno hayo kwa dhati bila unafiki, viongozi wa vyama vya siasa na waandishi wa habari mkoa huu ni watu ambao wamenipa ushirikiano mkubwa sana, kama ni taarifa nimezipata huko na nilipokuwa nazifuatilia nakuta zina ukweli.

“Kama ni waandishi wanaoandika habari za kweli  zilizojitosheleza kwa kila upande ‘balanced’ ni hapa Mwanza, natamani wengine waje kujifunza.

“Kwanza ukiwaita muda wowote wanafika na tunakwenda wote kwenye mapango, vile vile viongozi wa dini nao hawako nyuma wamesaidia mkoa kuwa na amani.

“Nimeondoka hapa nikiwa salama sijaondolewa hata cheo kimoja kama mnavyoona  hapa begani, hii inatokana na ushirikiano na  maofisa wenzangu wa polisi na kamati za ulinzi.

“Tangu nije  Mwanza haijawahi kutokea tunapiga mabomu bodaboda, machinga, madereva wa daladala  au wananchi kwa sababu ya maandamanao au vurugu, hawa watu ni kukaa nao na kukubaliana nao,”alisema.

Hata hivyo alisema moja ya tukio ambalo hawezi kulisahahu ni ajali ya kivuko cha MV Nyerere  kilichokuwa kikifanya safari zake kati ya Bugorola na Ukara  Wilayani Ukerewe   ambacho kilipinduka Septemba 20, mwaka jana  na kusababisha abiria  230 na wengine 41 kuokolewa.

Alisema katika ajali hiyo aliweza kupata changamoto kadhaa ambako alishirikiana na kamati ya ulinzi ya mkoa kuhakikisha watu wanaokolewa  wakiwa hai ingawa baadhi yao walifariki dunia.

Muliro na majambazi

Kwa upande wake Muliro, aliwataka majambazi wanaofanya uhalifu kwa kutumia silaha, kuandika wosia kabla ya kuingia mitaani.

Alisema miongoni mwa watu  atakaowashughulikia kwa nguvu zote ni majambazi wanaotumia silaha  kwa   kupambana na polisi au kuhatarisha usalama wa watu.

 “Kipaumbele  changu ni kusimamia kuzuia uhalifu hasa wale wanaotumia silaha za moto,  anayejua hiyo ndiyo shughuli yake (ujambazi) ni heri akabadili mtazamo wake.

“Sitakubali kuona askari wangu anazuiwa na mtu anayejiita jambazi, huyo atabadilika jina lake kwanza, pia silaha yake inachukuliwa na pengine ndiyo itakayomshughulikia.

“ Nitatunza siri kwa watu wanaotoa siri na nitajenga misingi  inayoongoza jeshi la polisi  askari wafanye kazi kwa weledi, kama mtu yupo hapa anashirikiana na wahalifu ni vema wakashauriane kuacha biashara hiyo.

“Tangu nifike nimedokezwa na Shanna kwamba waandishi wa habari walimsaidia   kupata taarifa nyeti, hivyo nami nitawatumia  kufanikisha lengo langu,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles