24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kama CCM wanawapenda Wazanzibari waamue mgombea urais 2020 atoke Visiwani

 NA HILAL K SUED

Mwaka 2014 wakati wa mijadala ya Bunge la Katiba, tuliona pasi shaka yoyote kwamba Zanzibar ndiyo kisiki kikubwa sana kwa chama tawala – CCM katika kutetea hoja yake ya kupitisha rasimu wanayoitaka ya muundo wa muungano wa serikali mbili.

Kisiki hiki hata CCM wenyewe walikitambua na kukikiri, hata kabla ya upigaji kura – kwamba bila ya maridhiano, theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar haiwezi kupatikana.

Hilo awali lilizungumzwa na Rais Jakaya Kikwete mwenyewe alipolihutubia Bunge hilo pale aliposema bila ya maridhiano rasimu haitapita kutokana na ulazima wa theluthi mbili kuipitisha, ingawa hakugusia kwamba hili limejikita zaidi kwa wajumbe wa kutoka Zanzibar.

Naye Marehemu Kingunge Ngombale-Mwiru, siku ya kuliahirisha Bunge alisema bila maridhiano ya pande mbili hakuna rasimu. Sasa upande upi ulitakiwa ulegeze msimamo?

Bunge hilo la Katiba lilisusiwa na Ukawa  na walidhamiria kutorudi bungeni hadi mapendekezo halisi ya rasimu ya Tume ya Jaji Joseph Warioba (ya muundo wa serikali tatu) ndiyo yawe mwongozo wa majadiliano. Tusisahau kwamba umoja huo ulionekana kukubalika kwa kiasi kikubwa huko visiwani (Unguja na Pemba).

Lakini siamini iwapo viongozi wakuu wa CCM yenyewe walikuwa wanalitambua hili – kwamba chama chao ndicho kilikuwa sababu kubwa ya kuzuka kwa hali ile ya sintofahamu. Na hii ilitokana na udogo wa Zanzibar, ukilinganisha na Bara. Pamoja na Muungano wa aina hii, yaani wa serikali mbili, bado Zanzibar inaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wake – lakini si masuala yanayoweza kusababisha kujitenga – kama vile suala la serikali tatu.

Sidhani hili nalo utawala wa CCM Bara (kumbuka serikali ya CCM ya Bara imejikita katika Serikali ya Muungano) ulikuwa unalitambua kwa uhalisia wake, kwani ungekuwa unalitambua vilivyo, usingekuwa unaviburuza visiwa hivyo namna inavyotaka.

Nathubutu kutumia msamiati ‘kuburuza’ kwani sioni namna nyingine ambayo utawala wa Bara unaonesha na kukiri au hata kuonesha kuwapo kwa hali ya usawa kati ya pande mbili za muungano.

Siku zote Zanzibar imekuwa ikipiga zumari la pili (second fiddle) katika masuala ya Muungano, labda pale inapoamua kutumia ubabe – kama vile ilivyoamua kupitisha marekebisho ya Katiba yake mwaka 2010, Katiba ambayo iliutambua upande huo kama nchi na hivyo kukiuka Katiba Ya Muungano ya mwaka 1977.

Huenda waliona kuendelea kungojea utawala wa Bara ndiyo uchukue hatua kama hiyo, ingebidi wangojee muda mrefu sana.

Kikubwa kinachofanyika kutoka kwa viongozi wa utawala wa Bara ni kauli tu za mdomoni za kuutukuza Muungano na kauli hizi zilifikia kileleni wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano mwaka 2014.

Kauli hizo hasa zilielekezwa kwa ‘maadui wa muungano’ – ambao bila shaka ni watu wa ‘kufikirika’ ambao eti wanataka kuvunja muungano, bila ya kuwataja.

Kwa tafsiri yoyote ile walengwa hawa ni wale wanaotetea muundo wa serikali tatu na nia ya kauli mbiu hizi ni kuuaminisha umma, kwa njia ya upotoshaji wa kimakusudi kabisa, kwamba serikali tatu ni kuvunja Muungano.

Wanachotaka Wazanzibari walio wengi ni muungano utakaowapa usawa na mamlaka ya kuamua mambo na mustakabali wao wenyewe, kama vile Bara ilivyo ndani ya hilo ‘koti la Muungano’ ambalo imekuwa ikilivaa kwa kipindi chote cha miaka 54 sasa.

Kwa mfano katika sherehe za Muungano za 2014 wengi walishangazwa na maonesho makubwa ya zana za kijeshi kana kwamba Muungano ulikuwa wa kijeshi. Baadhi ya watu walisema lengo lilikuwa ni Ukawa – hususani msimamo wao wa kuwa na muundo wa serikali tatu. Lakini kuna baadhi wanaona kuwa kuzionesha zana za kijeshi ni kutoa onyo kwa Zanzibar-kwamba kitendo chochote cha kutaka kuuvunja muungano hakitavumiliwa na Bara.

Vinginevyo watu wanajiuliza mafanikio ya Muungano katika miaka 50 yalikuwa ni ya kijeshi tu? Hakuna mafanikio mengine ambayo yanaweza kuoneshwa katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano?

Hata Muungano wenyewe, katika miaka 54 iliyopita, ukitoa miaka 10 ya utawala wa Ali Hassan Mwinyi, miaka iliyobaki 44 ilikuwa ya utawala wa rais kutoka Bara. Lakini kama kweli watawala wa CCM wa Bara wanawapenda wenzao wa Zanzibar, kwa nini wasisitize kuwapo kwa hali ya usawa katika uongozi wa juu wa muungano – kwa maana ya Urais?

Wengi wamekuwa wanauliza kwanini serikali ya Muungano haitoi nafasi kwa Zanzibar kwa kutamka kwamba mwaka 2020 ni zamu yao kutoa mgombea wa urais kupitia chama hicho? Kuna dhamira ya dhati ya kuonesha usawa, udugu na upendo kuliko hatua kama hiyo ambayo yumkini Zanzibar wataipokea kwa mikono miwili?

Viongozi wa CCM Bara kamwe hawako tayari kujitolea kitu kama hicho kwa sababu wamejawa na unafiki na baadhi yao uchu wa madaraka. Wanawaona wenzao hawastahili usawa huu kwani daima wao wanatakiwa kupiga zumari la pili.

Kuna baadhi ya watu watasema mpango kama huu hautawezekana kwani huenda Zanzibar watakosa mgombea mwenye nguvu kuweza kumkabili mgombea wa upinzani katika kinyang’anyiro cha urais. Lakini hii ni dhana tu, kwani watoe basi hiyo nafasi tuone kama kutakosekana mgombea madhubuti kutoka Zanzibar.

Kabla ya kuwa Rais mwaka 1985 wangapi huku Bara walimjua Ali Hassan Mwinyi? Au wangapi walijua kama engeimudu nafasi hiyo ya urais wa Muungano? Na sote sasa tunakubali alifanya makubwa katika kipindi chake.

Au basi kwa nini CCM, kama chama mwasisi wa Muungano, wasiweke utaratibu ambao wa kupokezana urais. Hapa sizungumzii Katiba ya Muungano inavyosema, lakini nazungumzia utaratibu tu wa chama hicho katika kuonesha kwa vitendo yale wanayoyatamka majukwaani ya haja ya kudumisha muungano, mshikamano, udugu nakadhalika.

Haya ninayoyazungumza si ya kufikirika, yapo katika nchi nyingine ingawa kwa hali tofauti kidogo, lakini lengo ni kuondoa manun’guniko na kuongeza mshikamano katika jamii.

Nigeria ni nchi kubwa yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 100 na kama ilivyo Tanzania kuna dini kubwa mbili Ukristo na Uislamu. Katika hali ya namna hii katika jamii mshikamano wa kisiasa na kijamii bila ya kufuata misingi ya dini huwa ni mtihani mkubwa sana.

Hivyo basi katika kujaribu kuikabili changamoto hii chamacha People’s Democratic Party (PDP) ambacho kilikuwa madarakani tangu 1999 na kuondolewa mwaka 2015 kilijiwekea utaratibu unaofanana na huu ninaousema.

Waliamua kwamba mgombea wa urais kutoka chama hicho uwe wa zamu kati ya Mwislamu na Mkristo – yaani kama Mkristo ni rais, basi baada ya vipindi vyake viwili vya miaka minne minne (yaani miaka 8) basi mgombea Mwislamu anafuata.

Hata tukiachia suala la urais, tangu kuundwa kwa Muungano mwaka 1964 Zanzibar haijawahi kutoa Mkuu wa majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Polisi (IGP) na Gavana wa Benki Kuu (BoT). Na yote haya ni masuala ya Muungano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles