27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kalemani ateua wajumbe wa Bodi Tanesco

Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameteua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yenye wajumbe nane.

Dk. Kalemani amefanya uteuzi leo Jumatano Novemba 13, unatokana na Rais John Magufuli kumteua Dk. Alexander Kyaruzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa kipindi kingine cha pili.

Rais Magufuli alimteua Dk. Kyaruzi Novemba 9, mwaka huu baada ya kuwa ameshika wadhifa huo kuanzia Mei 2016 hadi Mei 2019.

Dk. Kalemani amesema wajumbe hao wapya watakaa madarakani kuanzia Novemba 13, mwaka huu hadi Novemba 12, 2022.

Amewataja wajumbe hao kuwa ni Balozi Dk. James Nzagi (alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco iliyomaliza muda wake) na Dk. John Kihamba (Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Saam – DUCE).

Wengine ni Dk. Lugano Wilson (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi na Mkuu wa Teknolojia za Nishati – Tirdo), John Kulwa (Mkuu wa Idara ya Ukaguzi Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi – MUHAS) na Denis Munumbu (Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – Takukuru).

Wengine ni Dk. Gemma Modu (Mkurugenzi Nacte), Mathew Kirama (Mkurugenzi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Gilay Shamika (Mjumbe katika bodi iliyopita).

Dk. Kalemani alimpongeza Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua tena Dk. Alexander Kyaruzi kuisimamia Bodi hiyo.

Alimtaka Mwenyekiti huyo kulitumikia Shirika kwa Kasi, weledi na nidhamu ili kuwahudumia watanzania kwa kuondoa kero ndogo na kuifanya heshima ya Watanzania kwa Tanesco iendelee.

“Ni matumaini yetu mtakuja na ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya katika kutekeleza azma ya Hapa Kazi Tu ili kulipa nguvu Shirika letu,” amesema Dk. Kalemani.

Kwa wajumbe wote, aliwataka wachape kazi ili kuhakikisha wadau wa Tanesco wanafaidi huduma nzuri na kuhakikisha Umeme unawafikia watanzania wote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Dk. Kyaruzi amemshukuru Rais Magufuli kwa heshima kubwa kwake kwa kumteua tena kulisimamia shirika hilo.

Amesema Tanesco miradi mingi ya kimkakati ukiwamo Mradi wa Kufua Umeme wa Maporomoko ya Maji wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 na wa Rusumo mkoani Kagera.

Amesema miradi hiyo na mingine wataisimamia kikamilifu kwa kuweka mikono yao humo kwa kufuata miongozo mbalimbali wanayopewa na viongozi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles