27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kafulila: IPTL acheni kuweweseka

David Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila

Na Fredy Azzah

MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amesema ataendelea kupiga kelele mpaka fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Escrow zirudishwe.

Alisema kitendo cha Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kufungua kesi mahakamani ili imnyamazishe kinaonyesha wazi ni kuweweseka.

Kauli ya Kafulila inakuja wakati IPTL imewasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakitaka itoe zuio la muda kwa Kafulila asiendelee kuikashifu kampuni hiyo.

Maombi hayo yaliwasilishwa mwishoni mwa wiki iliyopita chini ya hati ya kiapo cha dharura na yameungwa mkono na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Harbinder Sign Seth.

Wadai katika hati hiyo, wanaiomba mahakama hiyo kutoa zuio hilo hadi shauri la msingi walilofungua mahakamani hapo dhidi ya mbunge huyo kwa kuwatuhumu kuiba fedha katika Akaunti ya Escrow isivyo halali litakaposikilizwa.

IPTL kwa kushirikiana na Kampuni ya Pan African Power Solution (T) Limited (PAP) na mtendaji mkuu wa kampuni hizo, Harbinder Sing Seth, ndio waliowasilisha maombi hayo mahakamani.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kafulila alisema haijamjulisha kuhusu kesi hiyo na kwamba hajatoa kashfa yoyote zaidi ya kueleza ukweli halisi wa jambo hilo.

Alisema suala hilo kwa sasa linashughulikiwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa azimio la Bunge, hivyo haliwezi kujadiliwa mahakamani.

“Ninachosisitiza ni kwamba, IPTL ni kampuni ya kifisadi na ina uzoefu kufisadi tangu ianze mpaka sasa. Fedha za escrow Sh bilioni 200 zilitolewa kwa njama za kifisadi. Ndiyo maana makubaliano kati ya IPTL na Wizara ya Nishati na Madini kuhusu fedha hizo walikubaliana iwe siri.

“Huyo PAP na Singh Seth wanahangaika tu, Watanzania wameamka. Hii nchi siyo ya Mfalme Juha, ambayo watakuja na kuvuna mabilioni kitapeli, wasubiri uchunguzi kisha waone Bunge litakavyoamua, waache kuweweseka,” alisema Kafulila.

Alisema anaendelea na kampeni ya kutaka fedha hizo zirudishwe na kuwa jana walitarajia kuendelea na kampeni hiyo iliyopewa jina la Bring Back Our Money (Rudisheni fedha zetu), kwenye Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Alisema lengo la kampeni hiyo ni kueleza wananchi namna ambavyo fedha hizo zilichotwa kwenye Akaunti ya Escrow, wakati wanafunzi wakiwa hawana madawati na wagonjwa wakiwa hawana vitanda vya kutosha wala dawa.

“Nasikia Seth kasema hana vita na Kafulila ana vita na Wazungu, hata mimi sina vita naye nina vita na Serikali iliyopora kwa mgongo wake. Mimi kama Mbunge sina kazi ya kuisimamia IPTL kazi yangu ni kuisimamia Serikali, hoja yangu ni kwanini Serikali iliruhusu wizi huu kwa mgongo wa IPTL?” Alihoji Kafulila.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. Kafulila, kazana tu kama unauhakika na jambo hili, hakika Mungu atakusimamia tu, na Watanzania wenye mapenzi mema watakuwa nyuma yako. Mungu akulinde na waovu wote katika jitihada za kutetea mali za Watanzania.Ubarikiwe sana.

  2. Kafulila anayoyasema Fr Mapunda yakitie nguvu na ujasiri usiona lifani kutupigania kodi zetu watanzania ambazo zinatafunwa na mafisadi bila kujali hata haki za msingi za raia yeyote duniani.

  3. Mh. Kafulila kanena ukweli usiopingika kwani nchi hii imeoza na janga la ufisadi kwa hili nampa pongez mbuge wangu kafulila kwa uhodali wake wa kutoboa ukweli bila woga ni wazi kuwa ufisadi huu unaiweka nchi katika hali mby huku wananchi tukizid kukumbwa na matatz mblmbl.. NB. tunahitaji wabunge wenye ujasir kama wa mh. kafulila ili kuunganisha nguvu ya pmj tuweze kuutokomeza ufisadi uliokithiri hapa nchin.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles