30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KACHERO WA POLISI AUAWA NA MAJAMBAZI

Na TUNU NASSOR-PWANI

WATU watatu akiwamo OCCID wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Peter Kubezya wamefariki dunia kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Jaribu mkoani hapa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamu Kifu alisema watu sita wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto walikivamia kizuizi cha kukusanyia ushuru kijijini hapo jana na kuwafyatulia risasi.

Kwa mujibu wa shuhudia wa tukio hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema watu hao walifika katika kizuizi cha Maliasili kilichopo kijijini hapo na kukichoma moto.

Shuhuda huyo alisema baada ya kuchomwa moto kwa kizuizi hicho ndipo majibizano ya risasi yalianza kati ya majambazi hao na askari polisi waliokuwa doria.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni ya Mchukwi, Zacharia Lukeba alithibitisha kupokea mwili wa Kubezya na maiti nyingine mbili ambazo majina yake hayakutambuliwa mara moja.

Alipotafutwa kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Bonaventura Mushongi, simu yake ilipokewa na msaidizi wake na kusema Kamanda alikuwa kwenye kikao na hivyo hawezi kuzungumza na simu.

Mauaji hayo ni mwendelezo tangu mwaka jana ambapo eneo la Kimanzichana ambalo ni jirani na Wilaya ya Kibiti watu zaidi ya 10 wakiwamo viongozi wa vijiji walifariki dunia na wawili kujeruhiwa kwa risasi na kuviacha baadhi ya vijiji bila uongozi.

Mapema mwaka jana karani wa Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga aliyefahamika kwa jina moja la Pazi na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kimanzichana, Rajab Sinkole walidaiwa kuuawa kwa kuchinjwa.

Julai 17, mwaka jana, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimanzichana, Ramadhani Mkagile anadaiwa kwamba aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake jirani na kituo cha polisi kijijini hapo.

Mauaji mengine yanadaiwa yalifanyika Agosti 12, mwaka jana ambapo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mkuruwili, Salum Kiswamba ambaye pia alikuwa imamu wa msikiti alipigwa risasi na watu waliokuwa wamefunika nyuso zao.

Oktoba 6, mwaka jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kijiji cha Kimanzichana, Bakari Sinkole aliuawa akiwa ofisini kwake huku mtendaji wa kijiji hicho, Omar Mfilisi akijeruhiwa begani kwa risasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles