24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JWTZ yajitosa mauaji Tanga

wanajeshi
Askari wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ).

 

*Jenerali Mwamunyange atangaza msako usiku,mchana

na waandishi wetu,

SERIKALI imetuma kikosi maalumu cha ulinzi, kikiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuwasaka watu wanaodaiwa kuwa majambazi ambao wanaendesha mauaji ya kinyama mkoani Tanga.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya watu wanane kuuawa kinyama kwa kuchinjwa juzi usiku katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata jana, zinasema tayari vikosi hivyo vimeanza operesheni kali katika mapango ya Amboni ambayo yanadaiwa kuwa maficho ya watu hao.

Akitoa salamu za rambirambi wakati wa mazishi ya marehemu wanne kati ya wanane waliozikwa Kibatini jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema vyombo vya dola vitahakikisha watu wote waliohusika katika mauaji hayo wanatiwa mbaroni.

“Ndugu zangu nawapeni pole kutokana na kuondokewa na wapendwa wetu… naomba kuwahakikisha sisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola tutahakikisha tunawatia nguvuni watu wote waliohusika na mauaji haya,” alisema Jenerali Mwamunyange.

Alisema tukio la mauaji hayo ni la kusikitisha mno kutokana na Tanzania kusifika kuwa nchi ya amani duniani.

“Tanzania inasifika kuwa na amani duniani kote, lazima hatua za kiusalama zichukuliwe haraka ili kunusuru amani yetu isichezewe.

“Ni tukio la ajabu ambalo limegusa watu wengi wasio na hatia, tutasaidiana na wenzetu kuhakikisha wahalifu hawa wanapatikana,” alisema Jenerali Mwamunyange.

 WAZIRI MASAUNI

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Hamad Masauni, alisema Serikali inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kuwakamata wahusika ndani ya kipindi kifupi.

Aliwahakikisha wananchi kuwa ulinzi unaimarishwa na kwamba matukio hayo hayatajirudia tena.

“Vyombo vya ulinzi vitafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha tunawatia nguvuni haraka watu waliohusika na mauaji hayo,” alisema Masauni.

Aliwaomba ndugu na jamaa ambao wamefiwa na ndugu zao kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu alisema wataendelea kuimarisha ulinzi na usalama maeneo yote.

 WANANCHI

Katika hatua nyingine, wakazi wa mitaa mitatu ya Mleni Kati, Mleni Mashariki na Kibatini katika Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga, wameanza kukimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao baada ya mauaji hayo.

Mauaji hayo yalitokea juzi usiku ambapo watu wanaoaminika kuwa majambazi walivamia nyumba tatu katika eneo hilo, wakiwa wamelala usiku, kisha kuwateka na kuwapeleka msituni kabla ya kuwachinja.

Wakazi hao wanaounda zaidi ya kaya 30, walisema wameamua kuyakimbia makazi yao kwa kutokuwa na imani ya usalama wao katika eneo hilo, baada ya wale wanaoitwa majamabzi kuvamia makazi yao kwa mara ya pili kwa staili ya kutisha.

Kabla ya tukio hilo la juzi, watu wasiofahamika walivamia makazi yao na kuchinja kuku 40, mbuzi wanne na ng’ombe mmoja na kukimbilia mapango ya Amboni na hawajawahi kukamatwa.

MTANZANIA jana lilishuhudia wanawake na watoto wakiwa na mizigo mithili ya wakimbizi wakiondoka katika eneo hilo huku wanaume wakibaki kwa ajili ya kuzika ndugu, jamaa na marafiki zao waliouawa katika tukio hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Juma Issa, alisema wamelazimika kuwahamisha wanawake na watoto kwa kuhofia wanaweza kuvamiwa tena kwa mara ya pili.

Nae Lucas Muhina alisema kuwa anashindwa kuhama katika eneo hilo kutokana na kuwa na mifugo, hivyo anashindwa kujua mahali salama pa kuihifadhi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibatini, Shabani Mwamini, alithibitisha baadhi ya wananchi wa mitaa mitatu kuhama katika eneo hilo.

“Nyumba nyingi zimebaki na wanaume pekee yake kwani wanawake na watoto wote wamehama kwa sasa,” alisema.

Wakati huohuo, maiti nne kati ya nane zimezikwa jana huku nyingine nne zikisafirishwa nje ya mkoa huo.

Mwamini aliwataja waliozikwa kuwa ni Issa Husein, Mkola Husein, Issa Hamis

na Salim Adam.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella alisema kuwa vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.

 SIMULIZI ZA MAUAJI

Mtoto wa marehemu Mkola Hussein
anayeitwa Salimu Mkola (16) alisababisha vilio na simanzi kwa waombolezaji baada ya kusimulia namna watu hao walivyomchukua baba yake na kwenda kumchinja mbele ya nyumba yake.

Akisimulia tukio hilo huku akibubujikwa machozi, mtoto huyo alisema watu hao walifika nyumbani kwao wakagonga mlango saa sita usiku na kumuamrisha baba yao atoke na fedha.

“Nilipoona hivyo nilijaribu kupiga kelele
kuomba msaada kwa majirani, lakini mmoja wa wauaji aliingia ndani na kunitoa nje ya nyumba yetu, huku akiniuliza wakati wale vijana saba
wanachukuliwa na polisi mimi nilikuwa wapi.

“Waliendelea kuniuliza kama nina habari ninayoijua, huku wakiwa wameshika mapanga na bunduki, ndipo waliponiambia wapo kwa ajili ya kutetea dini yetu.
“Baadaye waliniruhusu niingie ndani na kulala, lakini niliendelea kusikia vishindo vya kipigo na watu wakikoroma ambayo ilikuwa ni ishara ya kuwa baba yangu alikuwa anakata roho pamoja na watu wengine,” alisema.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Abuu Mkola, alisema vijana saba ambao sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi awali walionekana katika Kitongoji cha Kibatini wakiwa wanakimbia kusikojulikana.

Alisema baada ya hali hiyo baba yake ambaye ni marehemu, Mkola Hussein
akishirikiana na wananchi wa mtaa huo walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walikuja na kuwakamata vijana hao lakini mmoja wao alifanikiwa kukimbia.
Abuu alisema kuwa katika tukio la juzi, wauaji hao wakati wanamchukua baba yake walisema wanawahitaji vijana wao saba waliokamatwa na polisi, lakini aliposema hajui ndipo walimuunganisha na watu wengine kwa ajili ya kumchinja.

BUNGENI

Ofisi ya Bunge imeiagiza Serikali kutoa taarifa rasmi kuhusu mauaji yanayoendelea nchini ili kuwatoa hofu wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali.

Akitoa maagizo hayo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni anapaswa kuzungumza na Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yote ambayo yametokea mauaji ili aweze kutoa taarifa ndani ya Bunge.

“Waziri atuletee taarifa kwa sababu Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) yupo hapa na waziri anayehusika na mambo ya Bunge yupo, naomba watuletee taarifa kwa sababu mauaji yamekuwa yakitokea mara nyingi na tumekuwa tukiwasihi Serikali ituletee taarifa na si mtakuwa mnazitafuta,” alisema Dk. Tulia.

Baada ya maelezo hayo Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alisimama na kuomba mwongozo chini ya kanuni 68 (7).

“Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na haya uliyoyatolea maelezo juu ya mauaji yanayotokea katika nchi yetu, nimelazimika kuomba mwongozo huu kwa sababu matukio yaliyoanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali na maeneo mengine mambo haya tuliwahi kuyauliza Serikali na kuahidi watayatolea ufafanuzi.

“Sasa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani  amekwenda kuangalia na atazungumzia jambo hilo wakati mambo haya wabunge tulishaiomba Serikali itoe ufafanuzi ni jinsi gani inajipanga kukabiliana nayo,” alisema Lugola.

Alisema kitendo cha Serikali kusema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amekwenda kushughulikia jambo hilo wakati huo huo mambo ambayo yametokea Mwanza na maeneo mengine yalishaombewa ufafanuzi lakini hakuna majibu si kizuri.

 CUF WATAKA UKWELI

Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani mauaji hayo.

Katika taarifa iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari na kusainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Abdul Kambaya, ilisema vitendo hivyo katika Jiji la Tanga si mara ya kwanza kutokea.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CUF imelitaka Jeshi la Polisi kuwaeleza Watanzania ukweli wa tukio hilo na mengine kama hayo kabla taasisi na mashirika mengine binafsi hayajatoa ukweli wa suala hilo.

 

Habari hii imeandaliwa na Oscar Assenga, Amina Omary (Tanga) na Aziza Masoud (Dodoma)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles