31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JWTZ walivyouawa DRC Kongo

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeeleza jinsi askari wake wawili wanauonda Kikosi cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO) kinacholinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), walivyouawa na wengine 16 kujeruhiwa na waasi wanaodhaniwa ni wa Allied Democratic Force (ADC).
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jana kuwa askari wawili ambao mwanzo walidaiwa kutoweka msafara wao uliposhambuliwa sasa wamekwisha kuungana na wenzao.
Alisema tukio hilo lilitokea Mei 5 saa 12:30 jioni.
“Awali kikundi cha wanajeshi 46 ambao ni walinzi wa amani kilisafiri kwa helkopta kutoka mji wa Abialose kwenda mji wa Mavivi. Baada ya kufika Mavivi msafara huo ulielekea mji wa Mayimoya kwa barabara wakitumia magari ya jeshi.
Wakiwa njiani ndipo msafara wao ulipovamiwa na kikundi kinachodhaniwa kuwa cha waasi wa ADF na magari waliyokuwa wakisafiria yalishambuliwa kwa silaha za kivita ambako gari moja liliteketezwa na kusababisha vifo vya askari wawili papo hapo na wengine 16 kujeruhiwa,” alisema Meja Masanja.
Alisema hadi sasa askari wanne wa Tanzania wamekwisha kuuawa Kongo.
Alisema kwenye eneo la mapigano jambo lolote linaweza kutokea hivyo ni vigumu kueleza moja kwa moja sababu ya shambulio hilo.
Kuhusu majina ya marehemu, alisema kwa sasa taratibu za kuwaarifu wafiwa zinaendelea na jeshi hilo litaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.
Juu ya walipokuwa askari ambao awali iliripotiwa kwamba hawajulikani walipo, Meja Masanja alisema katika hali ya kujiokoa, askari hao walipoteana na wenzao kwa muda lakini walikwisha kuungana na walinda amani wengine wa Tanzania.
Kuhusu taarifa za shambulio hilo kuchochewa na Tanzania kumkamata mmoja wa viongozi wa waasi hao, Meja Masanja alisema huo ni uzushi na hakuna kiongozi yeyote wa waasi aliyekamatwa na Tanzania.
Taarifa iliyotolewa juzi na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia msemaji wa MONUSCO, Kanali Felix Basse, ilisema mbali ya waliouawa, wanajeshi wengine 13 walijeruhiwa na wanne walikuwa hawajulikani waliko.
Nalo Shirika la Habari la Ujerumani (Deutsche-Welle) katika matangazo yake ya saa 7.00 mchana juzi, lilisema waasi hao walitekeleza shambulio hilo kwa madai ya kulipa kisasi cha kiongozi wao kukamatwa na vyombo vya dola vya Tanzania.
Mmoja wa watu walihojiwa alisema: “Waasi walinipiga risasi wakanivunja mguu, mimi ni dereva wa teksi… sababu kubwa ya kufanya mashambulio haya wanadai ni kukamatwa kiongozi wao na Tanzania.
“Walikuwa wamefunga eneo lote la barabara, wana silaha nzito… sijui hata abiria niliokuwa nao wako hai ama la,” alisema mtu huyo.
Shambulio hilo ni la pili dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN) baada ya helikopta ya MONUSCO kushambuliwa na watu wasiojulikana Jumatatu.
Mkuu wa operesheni za MONUSCO, Martin Kobler, alilaani shambulio hilo dhidi ya kikosi cha wanajeshi wa Tanzania kinacholinda amani katika kijiji hicho.
Jeshi la DRC lilizindua ‘Operesheni Sukola’ dhidi ya ADF mwaka jana baada ya kundi hilo kutuhumiwa kuua wanakijiji 300 karibu na mji wa Beni kati ya Oktoba na Desemba mwaka juzi.
Umoja wa Mataifa upo katika harakati za kuvunja makundi kadhaa ya waasi mashariki mwa DRC baada ya miongo miwili ya mgogoro ambao sehemu kubwa unachochewa na utajiri wa madini wa nchi hiyo.
Agosti mwaka jana, askari wa Tanzania, Luteni Rajabu Ahmed Mlima aliuawa huku wengine watano raia wa Afrika Kusini wakijeruhiwa katika mapigano na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa DRC.
Mapigano hayo yalitokea karibu na Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini.
Jeshi la DRC linapata msaada wa kikosi cha askari 3,000 wa Umoja wa Mataifa ambao wana idhini maalumu ya kupigana ana kwa ana na makundi ya waasi wenye silaha katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini. Kikosi hicho kinajumuisha wanajeshi wa Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles