23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: WANAFUNZI WANAOPATA MIMBA MARUFUKU KURUDI SHULENI

ELIZABETH HOMBO, Dar Na GUSTAPHU HAULE, Kibaha


RAIS Dk. John Magufuli amesema ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi atakayepata mimba na kuruhusiwa kurudi shuleni.

Amezitaka taasisi zinazotetea utaratibu wa wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni, kufungua shule zao za wazazi lakini si kuilazimisha Serikali kufanya hivyo.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo   siku chache baada ya Taasisi ya HakiElimu kuitaka Serikali kuharakisha kupitia na kupitisha  miongozo  watoto wa kike waliojifungua warejee shuleni na kuendelea na masomo.

Mbali na HakiElimu, pia wadau mbalimbali na baadhi ya wabunge wamekuwa wakitetea utaratibu wa wanafunzi wanaopata mimba kurudi shuleni wakitoa sababu mbalimbali za watoto wa kike kubeba mimba.

Akizungumza jana akiwa katika ziara yake mkoani Pwani ambako pia alizindua viwanda saba, Rais alisema katu katika utawala wake hataruhusu utaratibu huo huku akizitaka taasisi binafsi zinazotetea wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni wafungue shule zao za wazazi.

“Yaani anapata mimba amezaa mtoto iwe kwa makusudi,  kwa bahati mbaya au kwa raha yake, yaani aende shuleni ameshazaa! Si atawafundisha hawa wengine ambao hawajazaa!

“Halafu akipata mimba tena ya pili anaenda nyumbani akizaa anarudi shuleni anapata wa tatu tena hivyo hivyo, yaani tusomeshe wazazi?

“Nataka niwaambie na hizi Ngo’s na wote mnaonisikia ndani ya utawala wangu kama rais, hakuna mwenye mimba atakayerudi shuleni.

“Nataka niwaeleze tukienda kwa mzaha wa namna hiyo na tukisikiliza hizi Ngo’s wanakotupeleka wanalimaliza taifa letu,” alisema Rais Dk Magufuli.

Alisema Serikali yake ilitenga Sh bilioni 18 kwa ajili ya elimu bure  kwa sababu wapo watoto wa masikini ambao wanapata shida, lakini wanapokuwapo wachache wanaotetea hayo taifa litafika pabaya.

Alisema hivi sasa ukifanywa uchunguzi watu ambao wanatetea hayo ndiyo hao hao ambao nao walipata mimba wakiwa shuleni.

“Sasa narudia tena, hakuna mwenye mtoto katika elimu ya darasa la kwanza hadi sekondari kurudi shuleni kwa sababu amechagua maisha hayo ya mtoto akalee vizuri mtoto wake.

“Lakini hata kama amepata mimba kwa bahati mbaya, yako mambo mengi ya kufanya ambayo yanaruhusu mtu aliyejifungua kufanya anaweza kwenda VETA, akajifunza kushona cherehani, akakopa kulima kilimo cha kisasa.

“Labda ukazalie chuo kikuu huko wanaruhusiwa uwe mwaka wa kwanza, wa pili wewe zaa tu.

“Lakini sekondari uzae halafu urudi tunapoteza maadili yetu, watazaa mno, itafika baada ya miaka kadhaa mtakuta darasa la kwanza wote wana watoto, wanawahi kwenda kunyonyesha kwa sababu mchezo huo ni mzuri na kila mmoja angependa aufanye,” alisema.

Hata hivyo alivitaka vyombo vya dola kuhakikisha wale ambao wanawapa mimba wanafunzi sheria ifuatwe.

“Nitoe wito kwa vyombo vya dola kwa sababu watakuja watu watasema, je wanaowapatia mimba itakuwaje? Sasa, je mimi niwabadilishe maumbile yao?   Wanaowapa mimba sheria ipo atakwenda kutumikia miaka 30.

“Watu wa ajabu sana, hatuwezi kupeleka taifa hili katika maadili hayo. Kama wanaowatetea ni wazazi hawazuiliwi na hizi Ngo’s si wakafungue shule za wazazi kwa sababu wanakula tu fedha za bure za wafadhili lakini siyo waiamrishe Serikali kutekeleza hayo.

“Nakupongeza Mama Salma Kikwete (Mbunge wa Kuteuliwa), ulisimama bungeni ukipinga haya endelea hivyo hivyo.

“Sisi wote tuna watoto hata kama nina mtoto wangu wa kile apate mimba halafu arudi shuleni, wafanye halafu waone kama nitawarudisha shuleni.

“Wametuletea watu kubakana wanaume kwa wanaume, wanawake kwa wanawake, wakati hata mbuzi au ng’ombe hafanyi huo mchezo… umeshawahi kuona mbuzi anakosea au ng’ombe?” alisema.

PEMBEJEO HEWA

Rais Dk. Magufuli alizungumzia suala la pembejeo hewa za kilimo ambako watu waliofariki dunia miaka zaidi ya 30 iliyopita wameandikiwa pembejeo kwenye vitabu.

“Kuna watumishi hewa, vyeti hewa, wanafunzi hewa,   hivi sasa pia kuna pembejeo hewa. Wamepewa pembejeo na wameandikishwa wakati wamekufa zaidi ya miaka 30 sasa walikuwa wanatoka makaburini kuja kulima? Hata yanatokea Tanzania tu,” alisema.

Aliwataka wakurugenzi wote nchini kabla ya Juni 30 mwaka huu, wawe wamekwenda kwenye kiwanda cha dawa za kuua mbu  kuchukua dawa hizo kwa ajili ya kuzisambaza.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli, alimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kurudisha serikalini viwanda vyote vinavyomilikiwa na wawekezaji walioshindwa kuviendeleza.

Alisema kama wawekezaji hao watakuwa wabishi ni vema wakamatwe na ikiwezekana wapelekwe mahakamani ili iwe fundisho kwa wawekezaji wengine ambao watakuwa wanamiliki wa viwanda bila kuviendeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles