26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: NITAFUNGA MIGODI YOTE

Na WAANDISHI WETU-

KIGOMA, DAR ES SALAAM

WAKATI mazungumzo kati ya Kampuni ya Barrick Gold Corporation inayomiliki zaidi ya asilimia 60 za hisa katika Kampuni ya Acacia Mining Plc na Serikali yakisubiriwa, Rais Dk. John Magufuli, amesema endapo wawekezaji hao watachelewa kuja, ataifunga migodi yote.

Juni 14, mwaka huu, Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Barrick, Profesa John Thornton, kisha Kurugenzi ya Mawasiliano-Ikulu ikatoa taarifa kwa umma kwamba kampuni hiyo ilisema ipo tayari kufanya mazungumzo ya kurekebisha mikataba ili pamoja na mambo mengine, pande zote mbili (Serikali na Barrick) zifaidike katika madini wanayoyachimba katika migodi hiyo, baada ya Acacia kufanya udanganyifu katika uendeshaji wa shughuli zake hapa nchini.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini, Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi.

Viongozi hao walikutana baada ya kusomwa kwa ripoti ya kamati ya pili ya uchunguzi wa mchanga wa dhahabu (makinikia), iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osoro.

Akisoma ripoti ya kamati yake, Profesa Osoro alisema takwimu walizokusanya kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mwaka 1998 hadi Machi, mwaka huu, makadirio ya chini yanaonyesha makontena yaliyosafirishwa nje ya nchi ni 44,277, huku kwa makadirio ya juu yakiwa ni 61,320.

“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 44,077 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh trilioni 132.56, sawa na Dola bilioni 60.25 za Marekani, au Sh trilioni 229.9, sawa na Dola bilioni 104.5 za Marekani kwa kiwango cha juu.

 

“Thamani ya madini yote katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya mwaka 1998 na 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani ni shilingi trilioni 183.597, sawa na Dola bilioni 83.45 za Marekani, kwa kiwango cha juu ni sawa na shilingi trilioni 380.499, ambazo ni Dola bilioni 144.77 za Marekani,” alisema Profesa Osoro.

Akizungumza mkoani Kigoma jana, alipokwenda kuzindua ujenzi wa Barabara ya Kibondo-Nyakanzi, Magufuli alisema na kuongeza: “Nitasimamia haki siku zote katika maisha yangu na niliwaambia nimeanzisha vita hii ya kiuchumi, vita ya kiuchumi ni mbaya sana, wakubwa wale huwa hawafurahi, kuna viongozi wengi tu mliona yaliyowapata ni kwa sababu nchi zao zilikuwa na mali.

“Lakini wale wakubwa wakataka kuchezea hizo mali, kwa manufaa yao na si kwa manufaa ya wananchi wa pale, walitumia mbinu nyingi za kila aina, lakini Mungu wangu ni mwema na Watanzania ni wema, watasimama kwa ajili ya taifa hili.

“Ninayoongea nayajua ni matrilioni ya fedha, ambayo yameibiwa, na kwa sasa hivi tumewaita waje wafanye mazungumzo, wamekubali, lakini wakichelewa chelewa  nitafunga migodi yote.

“Ni mara 10 migodi hii tukagawana Watanzania wachimbe, wawe wanauza tuwe tunapata kodi, kuliko kuchimbwa na watu wanaojiita wawekezaji halafu hawalipi kodi. Walikuwa wanazungumza mle wanachimba dhahabu, madini machache tu, matatu. Tumegundua mle kuna madini mengi.

“Tanzania hii ni nchi tajiri, lakini imekuwa ikiibiwa mno, tumechezewa sana, mimi nipo serikalini na mimi ndiye najua siri za serikalini, tumechezewa sana kwa kuibiwa sana mali zetu, kwenye dhahabu huku tumeibiwa mno, ukiyajua yale yaliyokuwa yanafanyike mle unaweza ukalia.

“Unaweza ukatamani kwamba usiishi, mtu anachimba anapokea, anapeleka na anashirikiana na baadhi ya watu tuliowaamini kwenda kulisimamia hili.

“Anasema hapa tunasafirisha mchanga na Watanzania wote tunaamini tunasafirisha mchanga, mbona hawajaja Kibondo kuchukua mchanga wa hapa, mbona na penyewe tunao?

“Lakini tunaamini, wanaupeleka kwenye makontena wanapeleka Ulaya na wakishaenda kuusafisha kule ule mchanga unaobaki wala hawaurudishi, ulikuwa ni utapeli wa ajabu, na ni aibu kubwa kuona utapeli huu unafanywa na watu ambao ni wakubwa.

“Ni dhambi kubwa na ni dharau kubwa kwa Taifa la masikini kama Tanzania, wananchi wake wanakosa dawa wanakufa, wanakosa maji, wanakosa barabara, watu wanakufa kwa kipindupindu, wanakosa elimu bora, wanakosa umeme, mali tuliyopewa na Mungu inakuja kusombwa na watu bila kujali utu wa Watanzania.

“Ndiyo maana niliwaambia ndugu zangu mimi nimezaliwa kwa ajili ya Watanzania, kama kuna baya lolote linanitokea linitokee kwa sababu ya Watanzania.”

 

MAPATO ACACIA YAPOROMOKA

Jana Acacia ilitoa taarifa ya ripoti yake ya nusu mwaka (miezi sita) huku ikionyesha kushuka kwa mzunguko wake wa fedha kutoka Dola milioni 318 za Marekani (Sh bilioni 709.115) hadi Dola milioni 176 (karibu Sh bilioni 392.46).

Ripoti hiyo iliyoishia Juni 30, mwaka huu, imeonyesha kuwa, Acacia imepoteza mapato ya hadi kufikia Dola milioni 176 za Marekani (karibu Sh bilioni 390.236) katika kipindi hicho cha miezi sita kutokana na kile ilichokiita kama ni kipindi kigumu, hasa kutokana na Serikali kuamuru kusitishwa kwa usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

Katika ripoti hiyo yenye maneno 28,605, Acacia ilisema katika nusu ya mwaka 2017, ililipa jumla ya Dola milioni 53 za Marekani kama kodi na mirabaha.

“Nusu ya kwanza ya mwaka huu imekuwa na changamoto kubwa katika uendeshaji wa migodi yetu hapa Tanzania, baada ya zuio la usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Nimefurahishwa na jinsi tulivyojitahidi kufanya vizuri pamoja na changamoto nilizotaja huko juu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo, iliyomtaja Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya hisa za Acacia ilishuka kwa asilimia 31 kulinganisha na Desemba, mwaka jana.

Taarifa hiyo ilisema pia kuwa, gawio la mwaka jana la dola senti 8.4 kwa hisa lililipwa kwa wanahisa Mei 25, mwaka huu.

Kutokana na changamoto zilizojitokeza, Bodi ya Wakurugenzi ya Acacia bado haijapendekeza gawio la mwaka huu.

Ripoti hiyo pia imedai kuwa, pamoja na changamoto zilizojitokeza katika kipindi husika, Acacia ilikuwa na uzalishaji mkubwa zaidi katika historia ya kampuni hiyo. Uzalishaji wa dhahabu ulikuwa wakia 428,203, ambao ni ongezeko la asilimia nne.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ingawa mauzo ya dhahabu yalikuwa Dola 893 za Marekani kwa wakia moja, mauzo hayo yalikuwa chini kwa asilimia tano ukilinganisha na yale ya mwaka jana.

Pia Acacia ilisema katika ripoti hiyo kuwa, Serikali isingesitisha usafirishaji wa makinikia Machi, mwaka huu, basi mauzo yangekuwa Dola 800 za Marekani kwa wakia moja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, athari mojawapo ya kukataza kusafirisha makinikia ni pamoja na sasa imewalazimu Acacia waweke viwango vidogo vya malengo yao ya uzalishaji ambayo ni kati ya wakia 850 hadi 900,000 kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kusitishwa kwa usafirishaji wa makinikia nje ya nchi kumeiathiri migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi, ambayo huzalisha dhahabu halisi na makinikia, huku Mgodi wa North Mara unadaiwa kutoathirika kutokana na ukweli kwamba, mgodi huo unazalisha dhahabu halisi.

Katika ripoti yake, Acacia imeendelea kukanusha taarifa zilizotolewa na kamati mbili zilizochunguza sekta ya madini nchini hivi karibuni.

Acacia imeendelea kukataa taarifa kwamba kampuni hiyo imekuwa ikidanganya kuhusu kiwango kilichopaswa kulipwa kama kodi.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilisema itaendelea kutoa ushirikiano katika uchunguzi unaoendelea na ilishatoa nyaraka zote kusaidia uchunguzi huo.

Acacia inarudia kueleza kwamba, imekuwa ikitoa taarifa zake za biashara kulingana na thamani ya wakati husika na imekuwa ikilipa mirabaha yote na kodi tangu ianze kazi zake nchini Tanzania.

Pia ilisema inaendelea kuangalia kwa makini athari za sheria mpya za madini zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni.

Wakati huo huo, Acacia ilisema maofisa wake wawili waandamizi walikamatwa na kuhojiwa na mamlaka za Tanzania kuhusiana na uendeshaji wa migodi yake hapa nchini.

“Watumishi wetu wengi waandamizi walihojiwa na mamlaka za Tanzania,” zilidai taarifa zilizomhoji Gordon kutoka London na kuongeza: “Tutaendelea kuwaruhusu watumishi wetu kuhojiwa.”

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Makamu Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Deo Mwanyika, ni miongoni mwa maofisa walioitwa na kuhojiwa.

Alex Lugendo, ambaye ni mshauri kuhusu masuala ya ushirikiano na Serikali, naye inadaiwa alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuhojiwa alipowasili akitokea  nchini Australia.

TMAA YAFUTWA

Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza kufuta rasmi Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kuunda Tume ya Madini, itakayokuwa na majukumu ya kusimamia shughuli zote zilizokuwa zinafanywa na TMAA.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, alisema uamuzi huo umetokana na sheria ya madini ya mwaka 2010 kufanyiwa mabadiliko hivi karibuni na kuanza kutumika Julai 7, mwaka huu.

Alisema watumishi wa TMAA waliokuwa na tuhuma na kusimamishwa kazi wataendelea kuchunguzwa kwa mujibu wa sheria na waliobaki wamerudishwa wizarani na kuendelea na majukumu yao katika ofisi ya Kamishna wa Madini.

“Baadhi ya watumishi waliokuwa TMAA ambao wamerudishwa wizarani wataripoti kwenye ofisi ya Kamishna wa Madini kwa ajili ya kuendelea na majukumu yao kwa sababu ni watumishi wa wizara,” alisema.

Pia alisema wamesimamisha shughuli za utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini hadi watakapomaliza kuandaa muundo mpya wa Tume ya Madini.

Alisema shughuli zote za madini kwa sasa zitasimamiwa na Kamishna wa Madini hadi muundo wa tume hiyo mpya utakapokamilika na kuanza kujipanga kufanya shughuli zake.

“Watumishi hawa hawatakuwa na mhuri wa TMAA, bali watakuwa wanatumia mhuri wa Kamishna wa Madini, hivyo basi tunaomba wawape ushirikiano ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo,” alisema.

Pia alisema kuanzia sasa, baada ya Serikali kufanya marekebisho ya sheria ya fedha na sheria ya kodi, mtu au kampuni itakayotaka kusafirisha madini nje yatakaguliwa na kuthaminishwa na atalipa ada ya ukaguzi ambayo ni asilimia moja ya thamani ya madini anayosafirisha.

Alisema mchimbaji mdogo anayeuza madini kwa wakala au mnada atakatwa asilimia tano ya thamani ya madini kama kodi na kupelekwa TRA.

Habari hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta, Augustino Lachuo (Tudarco), Tobias Nsungwe, Fredy Azzah (Dar es Salaam) na Editha Karlo (Kigoma).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles