23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, mamia wamwaga chozi wakimuaga Mengi

NA NORA DAMIANI

DAR ES SALAAM

RAIS John Magufuli ni mmoja wa maelfu ya Watanzania waliomwaga chozi jana wakati wa kuaga mwili wa  aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Rais Magufuli ambaye alifuatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali, alitoa heshima za mwisho jana wakati wa shughuli za kuaga mwili huo  katika ukumbi wa Karimjee.

Baada ya kuaga mwili huo  wakati akianza kutoka ukumbuni, Rais Magufuli alionekana kuvua miwani yake na kutoa kitambaa mfukoni kisha kufuta machozi.

Mbali na watu waliokuwa ndani ya ukumbi, mamia ya wengine walikuwa nje eneo la wazi huku baadhi yao wakilia kwa uchungu.

Pia kulikuwa na watu wengi wenye ulemavu waliofika hapo, kundi ambalo wakati wa uhai wake marehemu alikuwa akilisaidia kwa kiasi kikubwa.

Ingawa Rais Magufuli hakizungumza katika shughuli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Paramagamba Kabudi, alitoa salamu za Serikali akisema kifo cha Mengi kimekuwa cha ghafla.

“Serikali imehuzunishwa   na kifo chake, nchi imeondokewa na mtu mnyenyekevu, mpole na mwenye upendo kwa watu wote.

“Alishiriki moja kwa moja kujenga uchumi wa nchi yetu na kutoa ajira. Kwa namna ya pekee uzalendo wake uliwavutia wawekezaji wengi kuja nchini.

“Alishauri juu ya sera za  uchumi za nchi yetu na alikuwa mzawa na mzalendo wa kweli aliyeishi Sera ya Uchumi wa Viwanda na kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema maisha ya Mengi ambaye mwili wake leo unatarajiwa kupelekwa mkoani Kilimanjaro utakapozikwa kesho Machame Wilaya ya Hai, yana fundisho kubwa kwa sababu  alitumikia taifa kwa uzalendo, weledi, uthubutu na kujituma.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema Mengi alijenga himaya kubwa katika sekta ya habari iliyotoa mchango mkubwa nchini.

“Huwezi kuongelea sekta ya habari na sanaa Tanzania bila kugusa mchango mkubwa wa Dk. Mengi nchini, kazi za sanaa zilipata nafasi ya kurushwa katika vyombo vyake.

“Timu ya Serengeti Boys  iliposhindwa hakukata tamaa aliniambia nikitoka Dodoma tujadiliane kuhusu timu ya taifa, nasikitika kifo chake kimeninyima fursa hiyo,” alisema Dk. Mwakyembe.

VYAMA VYA SIASA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, alisema Mengi alikuwa miongoni mwa matajiri wazalendo na waliotumia utajiri wao kusaidia watu wengine.

“Kila palipokuwa na mkwamo kabla mambo hayajaharibika Mzee Mengi alikuwa kiungo kati ya chama na sekta binafsi.

“Tunayo bahati na tunajivuna kwamba alikuwa bilionea na mjamaa aliyeishi imani ya chama chetu, usawa wa binadamu, utu wa binadamu, ujamaa na kujitegemea.

“Katika mafanikio ya chama chetu kuanzia mwaka 2015 ushauri wa Mengi tumeuzingatia na kuutumia sana,” alisema Polepole.

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), James Mbatia, alisema Mengi alihimiza maridhiano kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao kuepusha umwagaji damu.

“Machi 20 mwaka huu aliniita ofisini kwake na alisisitiza namna gani tutaimarisha maridhiano katika uchaguzi mkuu ujao.

“Alisema maisha yako kwenye ulimu wa binadamu na alisisitiza tukitumia vizuri ndimi zetu hasa sisi wanasiasa Tanzania itakuwa sehemu salama na nzuri zaidi ya kuishi.

“Tuondoe kila aina ya jeuri na kuwa wanyenyekevu kama alivyokuwa Reginald Mengi,” alisema Mbatia.

Mbatia ambaye ni Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, pia alitoa rai kwa Serikali na sekta binafsi kumuenzi Mengi kwa kuwajali watu wenye ulemavu.

“Serikali na sekta binafsi mratibu siku ya kukutana  tuimarishe taasisi hii kwani ndiyo namna bora ya kumuenzi Dk. Mengi,” alisema.

Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe  ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA, alisema mara nyingi alizungumza na kubishana na Mengi kuhusu siasa, maisha na biashara lakini mfanyabiashara huyo aliwaogopa wanasiasa.

“Alijua kutafuta utajiri lakini hakuruhusu kuwa mtumwa wa utajiri. Ulikuwa wa  pekee sana ‘uncle’ Mengi Tanzania itakukumbuka na alama yako itaendelea kubaki,” alisema Mbowe katika salamu zilizosomwa kwa niaba yake na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema).

  Kubenea   alisema Mengi alikuwa kama mzazi aliyembeba mithili ya mtoto wa kumzaa.

“Mwaka 2008 nilipopatwa na majanga mbalimbali, Mengi alijitolea kunifariji na kugharamia matibabu yangu nje ya nchi.

“Bila mzee Mengi na baadhi ya watu wengine waliopo hapa mimi pengine leo ningekuwa kipofu,” alisema Kubenea.

Alisema licha ya Mengi kuwa mwanachama wa CCM lakini itikadi   kwake halikuwa jambo muhimu na kwamba alithamini utu wa mtu kuliko itikadi za vyama.

VIONGOZI WA DINI

Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, alisema kifo cha Mengi kimegusa wengi kwa sababu aligusa jamii katika huduma zake.

Alisema watamkumbuka Mengi daima kwa kuwa ameacha alama hai kwa kujenga shule ya watu wenye mahitaji maalumu.

 “Mbali ya matendo mema aliyoyaishi mwanadamu anakabiliana na nguvu ya uovu hivyo ni vema tukashirikiana kumuombea kwani Mungu hapendi mtu aangamie bali aishi kwa sura na mfano wake,”alisema Dk. Kitima.

 Askofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Nelson Kisare, alisema Mengi ameishi maisha ya aina yake, hivyo viongozi wa dini wana kila sababu ya kutumia changamoto kuwa fursa   kuisaidia jamii.

“Nafikiria angeweza kusema aliyoyatenda, kuyaishi, aliyoyapenda, yaliyo ya kweli tuyatafakari hayo,”alisema Askofu Kisare.

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Manfold Kijalo, alisema maisha yanapaswa kuwa furaha, baraka na amani kwa wanaokuzunguka na si kufurahisha tu nafsi yako.

Alisema Mengi amekuwa mfano bora wa kujitoa kwa wengine na hata kufanya toba.

“Hili ni funzo kwetu   tunapokosa tujifunze kufanya toba kwa kuwashirikisha viongozi wetu wa dini kwani mwenzetu hili alifanikiwa na ni imani amefurahia kifo chake,”alisema Mchungaji Kijalo.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema Mengi alikuwa mpenda amani na kwamba wataendelea kumkosa katika eneo hilo lakini watamuenzi kwa mazuri yake.

“Wamekufa watu lakini mema yao yanaishi na wengine wapo wanaishi kama wafu kwa sababu ya matendo yao,”alisema Alhad Salum.

SHIVYAWATA

Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (Shivyawata), Ummy Ndeliananga, alisema ni zaidi ya robo karne imepita Mengi akiitetea   watu wenye ulemavu.

“Siku zote aliamini katika utu na upendo kwa watu wenye ulemavu. Hakika kwetu alikuwa ni baba, rafiki, mshauri na mtetezi wetu.

“Wito kwa Serikali na wadau wengine tunaomba tusiishie kulia na kutoa machozi bali twende mbali zaidi kwa kuendeleza maono yake ya kusaidia watu wenye ulemavu,” alisema Ummy.

Alisema Shivyawata wataienzi Mei 2   kila mwaka kwa kutafakari maono ya Mengi.

TPSF, MOAT, CTI

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte, alisema Mengi alikuwa na mchango mkubwa katika sekta binafsi na maendeleo ya uchumi wa taifa.

“Alikuwa muumini wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma na aliamini kila binadamu ameumbwa kuwa namba moja na kinachowatofautisha ni uwezo wa kuona fursa na kuthubutu.

“Alikuwa anatamani kuona nchi ina mamilionea wengi kumzidi yeye, tuwajenge watoto na vijana kuwa wajasiriamali na tuweke mazingira bora yatakayowavutia Watanzania wengi kuthubutu na kuziona fursa,” alisema Shamte.

Mwakilishi wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Joseph Kusaga, alisema MOAT ni kama imepigwa radi kwa kifo cha Mengi.

“Tumekaa naye akituongoza kwa zaidi ya miaka 20, tumejifunza mengi kutoka kwake, hakuwa mchoyo wa mawazo na fikra za maendeleo.

“Mtu ana chombo cha habari lakini anakupa mawazo ya kufungua chombo cha habari.

“Tumepoteza mtu ambaye katika taifa hili atabaki katika fikra zetu…kufanya ‘replacement’ yake itabidi tufanye kazi ya ziada,” alisema Kusaga.

Mwakilishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Shubash Patel, alisema elimu aliyowaachia ni kubwa kuliko fedha alizokuwa nazo Mengi.

“Tumempoteza mshauri mkubwa, alitumikia CTI kwa miaka minne, elimu aliyotupa ya kuishi katika dunia hii ni kubwa kuliko fedha alizokuwa nazo.

“Tumeumia lakini tujifunze kuwa na roho ya kutoa na kusaidia kama alivyokuwa yeye,” alisema Patel.

MWAKILISHI WA FAMILIA

Balozi Mstaafu Juma Mwapachu, alisema maombolezo si nafasi ya kumuelezea Mengi kwa kuwa ameyaishi maisha ya kupendeza na kuwa kielelezo cha  biashara ndani na nje ya nchi.

Alisema alimfahamu zaidi ya miaka 30 ambako walifanya wote shughuli mbalimbali za  biashara.

“Ipo siku Mungu akipenda nitaandika kitabu nilivyomfahamu Dk. Mengi,”alisema Balozi Mwapachu.

Alisema kama rafiki na familia watamkumbuka katika maeneo saba ambayo ni pamoja na kuwa na imani ya kufanya kila jambo lililopo mbele yake na kuukataa umaskini hasa upande wa afya na elimu.

Mwapachu alisema alisaidia watu wenye ulemavu, fikra ya kuwa mjasiriamali, kuwekeza nguvu kubwa kwa vijana wanaohitimu vyuo kujikita kwenye ujasiriamali, hakujihusisha na siasa na aliguswa na mazingira ambako alianzisha kampeni ya kupanda miti Mlima Kilimanjaro.

“Kitabu chake ni urithi kwetu, Rais Magufuli aliomba kiandikwe kwa Kiswahili na tayari kazi hiyo marehemu ameikamilisha hivyo ni vema tukakitumia kama tunu kwetu,”alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema Mengi ni sikio la waliokata tamaa na mwamba wa watu wa kaskazini.

“Sikuwahi kutegemea hata siku moja kuona mchaga anampa fedha yatima au mlemavu, si jambo rahisi. Naitaendelea kufanya jambo jema la kuwashika mkono watu wenye ulemavu kama alivyofanya Mengi,” alisema Makonda.

KUAGA

Mwili wa Mengi uliingia katika viwanja vya Karimjee saa 9:45 asubuhi na  watoto wa marehemu kwa kushirikiana na familia waliingiza mwili huo ndani ya ukumbi.

Baada ya mwili huo kuingia viwanjani hapo watu wengi walionekana kuwa na nyuso za huzuni na wengine walishindwa kujizuia na kuangua vilio. 

Baada ya kumalizika  shughuli za kuaga, mwili wa Mengi ulipelekwa nyumbani kwake Kinondoni na leo utasafirishwa kwenda Machame wilayani Hai, Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles