27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, KENYATTA WAAMUA MAMBO MANNE

Na MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, wamewaagiza mawaziri wa nchi hizo mbili kutatua tofauti ndogo ndogo zinazojitokeza katika biashara.

Marais hao kwa pamoja walitoa agizo hilo jana asubuhi walipokutana na kufanya mazungumzo katika Hoteli ya Munyonyo, Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, imewakariri viongozi hao wawili wakisema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.

Kauli hizo zimekuja wakati ambako Juni mwaka jana Serikali ya Kenya ilipiga marufuku bidhaa za Tanzania kama unga wa ngano na gesi kuingizwa nchini humo pasipo kutozwa ushuru jambo ambalo ni kinyume na makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kuna mambo madogo madogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote mawaziri wa Kenya na mawaziri wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogo madogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa,” alisema Rais Magufuli na kuungwa mkono na Rais Kenyatta.

Kwa msingi huo maagizo yaliwalenga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya, Peter Munya.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.

Katika mazungumzo yao Rais Dk. Magufuli, alisema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki, inaguswa na hali ya Sudan Kusini hivyo alitoa wito kwa pande zinazopingana kumaliza tofauti zao ili wananchi wa Taifa hilo wajikite kujenga nchi yao.

“Nimemhakikishia Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudan Kusini na tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudan Kusini, hata chakula kama wanahitaji tutawauzia,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Kwa upande wake Rais Salva Kiir, alisema Tanzania na Sudan Kusini zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake lakini Rais Dk. Magufuli, amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaendelezwa na kukuzwa zaidi.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli, alikutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, Gaston Sindimwo.

Sindimwo alimfikishia ujumbe wa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, kuwa hali ya Burundi ni shwari na Rais Dk. Magufuli alisema anafurahi kuona wakimbizi wa Burundi waliokuwa wamepata hifadhi Tanzania wameanza kurudi nchini kwao.

Pia Rais Dk. Magufuli, alifanya  mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ambaye ni mratibu wa mazungumzo ya amani ya mgogoro wa Burundi aliyealikwa kuhudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles