25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Hata mimi huwa nashangaa tumewezaje

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amesema anajivunia kununua ndege tangu alipoingia madarakani Novemba mwaka 2015.

Alitoa kauli hiyo jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), muda mfupi baaada ya kupokea ndege aina ya Boeing 787-800 Dreamliner iliyowasili ikitokea nchini Marekani.

Rais Magufuli ambaye aliongoza mamia ya Watanzania kupokea ndege hiyo iliyowasili jana saa 8:36 mchana, alisema ndege hiyo ni ya saba kati ya 11 zinazotarajiwa kununuliwa na Serikali ifikapo mwaka 2022.

“Ninajisikia vizuri kuwa kiongozi wa Tanzania, lakini zaidi ninajisikia vizuri kuwa mwenyekiti wa CCM kwa sababu haya yalizungumzwa kwenye ilani ya uchaguzi na sisi ni watekelezaji.

“Yaani hata nashangaa… Mungu anatupenda Tanzania. Wewe ndege kama hii inashuka hapa lazima tujiulize kwanini haikushuka zamani? Huo ndiyo ukweli bila kuficha. Kwanini ndege kama hii isubiri Magufuli ndio ishuke,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ambaye alikuwa akirudiarudia kumshukuru Mungu katika hotuba yake, alisema mkakati wa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ni uhakika kulingana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015.

“Tulipoanza wengine walidhani tuna-beep, waswahili husema ukitaka kwenda safari ndefu lazima uende na hatua fupi, lakini tulipoanza kuifufua ATCL wengine walianza kupiga kejeli za chini chini,” alisema.

Alisema ndege nyingine nne zinatarajiwa kuwasili nchini kwa nyakati tofauti, huku moja ya masafa mafupi itawasili Novemba, nyingine itawasili Juni mwakani na nyingine mbili zinatarajiwa kuwasili kati ya Juni na Julai 2021.

AIONYA ATCL LUGHA MBAYA KWA WATEJA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliitaka menejimenti ya ATCL na watumishi wake kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi.

Alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wateja kuhusu maofisa wa shirika hilo kuwatolea lugha mbaya.

Katika hilo, aliwataka watumishi wa shirika hilo kuacha tabia hizo na badala yake wawahudumie wateja kama wafalme kwa kuwa wao ndio waajiri wao.

“Nitoe wito kwa menejimeti na watumishi wa ATCL tekelezeni majukumu yenu kwa ufanisi na weledi, ninafahamu kuna malalamiko mengi yanayotolewa na baadhi ya wateja kuhusu ucheleweshwaji wa safari na kuambiwa ndege imejaa ilihali bado kuna viti viko wazi.

“Pia wakati mwingine lugha zinazotolewa na maofisa sio nzuri, hivyo ninaomba mjirekebishe, nisingependa kusikia malalamiko hayo tena kwani wateja ndio waajiri wenu, hivyo ni lazima muwahudumie kama wafalme.

“Endeleeni na mkakati wenu wa kupanua mtandao wa safari zenu ndani na nje ya nchi, na kwenye hili sina tatizo, na muendelee kushirikiana na Bodi ya Utalii na mashirika mengine kwa ajili ya kutangaza kazi nzuri na maeneo mazuri ya utalii katika nchi yetu,” alisema Rais Magufuli.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho akielezea mkakati wa miaka mitano wa ATCL, alisema shirika hilo linatarajia kuwa na ndege mpya tisa zikiwemo nne za  Bombardier Q400, za masafa ya kati za Airbus A220-300 tatu na mbili kubwa za masafa marefu ambazo ni Boeing 787 Dreamliner.

MAKONDA ARUSHA KOMBORA KWA WABUNGE WA CHADEMA

Aidha, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo kutafuta Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam.

Alitoa agizo hilo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumwomba ampatie kiasi hicho cha fedha kwa hospitali hiyo kwa sababu wabunge wa eneo hilo wamekuwa hawawajibiki kwa wananchi.

“Kwanza nimefurahi sana Makonda umeomba Hospitali ya Wilaya ya Ubungo na umeomba Sh bilioni 1.5, nitazitoa ujenge hospitali. Hatuwezi kuacha wananchi wa Ubungo wateseke wakitaka kutibiwa waende mpaka wilaya nyingine, hapana, tutajenga hospitali nyingine,” alisema.

Awali, Makonda aliwataja wabunge wa upinzani Dar es Salaam; John Mnyika (Kibamba), Saed Kubenea (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe), akisema wamekuwa hawashiriki shughuli za maendeleo, hivyo akamwomba Rais Magufuli kumsaidia kiasi hicho cha fedha kwa ujenzi wa hospitali hiyo.

“Wananchi wa Dar es Salaam kuna majimbo matatu ambayo tulikosea; Jimbo la Kibamba, Ubungo na Kawe, wabunge wa majimbo haya sio tu kwamba sio watumishi wa wananchi, lakini ni wezi wanaokula posho bungeni bila kufanya kazi.

“Wilaya ya Ubungo ni mpya na ina wabunge wawili na ina meya wa upinzani, lakini hawawezi kuja kwenye shughuli yoyote ya maendeleo, wangeweza kufika hata kwenye shughuli ya leo wakawa sauti ya wakazi wa wana-Ubungo, mheshimiwa Rais ikikupendeza usikie kilio chao.

“Ubungo ni wilaya ambayo haina hospitali ya wilaya na wananchi wake wanalazimika kuja kupata huduma kwenye hospitali ya Wilaya ya Kinondoni wakati wabunge wao hawajawahi kutoa shilingi, wala kujenga hoja bungeni. “Wananchi wa Ubungo afya zao ziko matatani wabunge wao wameingi mitini, hivyo ombi langu kwako mheshimiwa Rais ninaomba unisaidie Sh bilioni 1.5 niwajengee hospitali ya Wilaya,” alisema Makonda.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles