30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Hata kujitoa katika uchaguzi ni demokrasia pia

Mwandishi wetu -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli amezungumzia hatua ya vyama vya upinzani kususia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, akisema ni demokrasia na kwamba maendeleo hayana chama.

Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu, vyama vikuu vya upinzani nchini vilijitoa kwa kile walichoeleza hawakutendewa haki wakati wa uchukuaji na ureshaji wa fomu za wagombea.

Kutokana na hali hiyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilinyakua vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, mitaa 4,263 sawa na asilimia 100 na vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4.

Akizungumza na wananchi wa Isaka wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga, Rais Magufuli alipongeza chama hicho tawala kwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.

“Nawashukuru sana ndugu zangu wa Isaka mmemaliza uchaguzi, nimeambiwa CCM kimepasua vizuri, hongereni sana, maendeleo ndugu zangu hayana chama na demokrasia hata kujitoa nayo ni demokrasia, kususia uchaguzi nayo ni demokrasia.

“Hivyo nawapongeza kwa ushindi mkubwa mlioupata CCM, lakini maendeleo hayana chama, ni lazima tushikamane wote kujenga taifa letu, tunachohitaji ni maendeleo, ukileta maji, wote watakunywa, uwe CCM, uwe Chadema, ukileta bandari hapa kila mmoja atafanya biashara,” alisema Rais Magufuli.

SIRI YA KUSITISHWA MIRADI YA KIMKAKATI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alifichua siri ya kusitishwa kwa baadhi ya miradi ya kimkakati, ikiwamo ujenzi wa stendi mpya ya Nzega mkoani Tabora na Nyegezi mkoani Mwanza.

Alisema fedha zilizopangwa kutekeleza miradi hiyo pamoja na mingine katika wilaya na mikoa kadhaa nchini, zimepelekwa katika miradi mingine yenye faida na masilahi zaidi.

“Si stendi ya Nzega pekee, hata ile ya Nyegezi Mwanza. Pia kule Mwanza walipanga kujenga soko kuu jipya la kisasa lenye ghorofa, sijui utauza nyanya kwenye ghorofa? Tumesitisha na kuhamishia fedha kwenye miradi mingine yenye faida na masilahi zaidi,” alisema Rais Magufuli.

MCHAKATO WA UJENZI WA RELI

Aidha Rais Magufuli alisema Tanzania na Rwanda zinakamilisha mchakato wa ujenzi wa reli itakayounganisha mataifa hayo mawili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mradi huo wa reli ambao utaunganishwa pamoja na reli ya kati ambayo itaanzia bandari kavu ya Isaka Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, tayari upembuzi yakinifu umekamilika.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli alisema kwa sasa kinachoendelea ni kutafuta fedha za utekelezaji.

“Tayari nimeshazungumza na Rais wa Rwanda (Paul Kagame) kuhusu utekelezaji wa mradi huu, upembuzi yakinifu umekamilika. Kinachofanyika sasa ni kutafuta fedha,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka wakazi wa Isaka kufanya kazi kwa bidii, hasa katika sekta ya kilimo na biashara ili kuzalisha mazao na bidhaa zitakazosafirishwa kupitia miundombinu inayojengwa na Serikali.

“Isaka msibakie kukaa mkiangalia haya malori ya mizigo yanayosafirisha mizigo inayohifadhiwa katika bandari kavu, chapeni kazi ikiwamo kutilia mkazo suala la kilimo cha mazao mbalimbali,” alisema.

WANAWAKE WALIOTOA KILIO

Rais Magufuli pia alilazimika kuwachangisha viongozi wa ngazi ya wilaya na Mkoa wa Shinyanga fedha kuwapatia wanawake wawili waliotoa kilio chao mbele yake, wakidai kutotendewa haki na mamlaka za haki licha ya kuwasilisha vilio vyao kwao.

Wanawake hao Mariam Maricha na Neema walitoa kilio chao hicho wakati Rais Magufuli aliposimama kuwasalimia wananchi hao.

Mariam alimweleza Rais Magufuli kuwa kuna mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Daudi alimpiga na kumvunja mkono, lakini mtuhumiwa aliachiwa huru na polisi.

“Mheshimiwa Rais, Daudi alinipiga akanivunja mkono, alikamatwa kupelekwa polisi, lakini nilipoenda siku inayofuata nilikuta ameachiwa, hadi sasa sijui yupo wapi,” alisema Mariam.

Baada ya kutoa kilio chake hicho, Rais Magufuli alimwita Mkuu wa Mkoa, Zainabu Telack, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kahama, Anderson Nsumba, mbunge wa jimbo hilo, Jumanne Kishimba, diwani na OCD kuchangia fedha na zikapatikana Sh 500,000 na kumkabidhi mwanamke huyo.

“Nimewachangisha fedha hizi ili viongozi mliopewa dhamana mjue kushughulikia matatizo ya wananchi hawa masikini,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Neema, alisema mumewe aligongwa na askari wa usalama barabarani akafariki dunia, lakini pamoja na kufuatilia amekuwa akizungushwa bila kupata msaada wowote.

Baada ya maelezo yake hayo, alichangiwa Sh 900,000 ili kuhudumia watoto wake wawili, huku Rais Magufuli akiagiza askari huyo asimamishwe kazi na kufuatilia kesi hiyo ili mama huyo apate haki yake.

“Haiwezekani mwananchi wa kawaida akifanya kosa anafungwa hadi miaka saba, lakini eti askari yeye hakamatwi yupo mitaani anazunguka na mnamuangalia tu, najua askari wanafanya kazi nzuri ila wapo wachache wanaoharibu,” alisema Rais Magufuli.

MKURUGENZI APATA KIGUGUMIZI

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mji wa Kahama, Nsumba, alishindwa kutoa majibu ya hoja na maswali ya wananchi mbele ya Rais Magufuli.

Majibu ya Nsumba kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha mjini Kahama, yalipata upinzani kutoka kwa Rais Magufuli baada ya kusema fedha za utekelezaji zitapatikana kupitia mkopo wa benki.

Nsumba alitoa majiobu hayo baada ya hoja ya mmoja wa wananchi kuhusu kukosekana kwa stendi ya kisasa ya mabasi mji wa Kahama wenye shughuli nyingi za kiuchumi kutokana na biashara na uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Katika jibu lake Nsumba alisema Halmashauri ya Mji Kahama yenye bajeti ya Sh bilioni 37, inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa stendi kupitia fedha za mkopo kutoka Benki ya TIB.

Jibu hilo halikumridhisha Rais Magufuli huku akihoji  inawezekanaje halmashauri yenye mapato ya zaidi ya Sh bilioni 37 ishindwe kutekeleza mradi wa ujenzi wa stendi kwa fedha zake za ndani hadi ichukue mkopo wenye riba wa benki.

“Kwanini msitumie fedha zenu hadi mkakope benki na mlipe kwa riba? Hebu kakope uone,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles