29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AZUNGUMZIA MAMBO 8 MUHIMU KWA UCHUMI

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ameeleza namna ilivyokuwa vigumu kuchukua hatua dhidi ya Kampuni ya Barrick Gold Mine na jinsi wajumbe wa Tanzania walivyotekeleza majukumu yao kwa uzalendo mkubwa, wakati wa mazungumzo na kampuni hiyo.

Rais Magufuli pia ameonya watu wanaopindua takwimu za uchumi wakisema makusanyo ya kodi yameporomoka, huku akitaka vyombo vinavyohusika kutumia sheria ya takwimu ya mwaka 2015, kuwapeleka watu hao mahakamani wakathibitishe kauli zao.

Dk. Magufuli alifichua siri hiyo Dar es Salaam jana, mara baada ya kutoa vyeti vya kutambua mchango wa wajumbe wa Tanzania waliokuwa wakifanya mazungumzo na timu ya Barrick na hatimaye kuibuka na maridhiano mbalimbali ikiwa ni pamoja na Serikali kupata asilimia 50 ya faida kutoka katika kila mgodi.

Akizungumzia suala la kupindua takwimu, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi pamoja na vyombo vya dola kuwachukulia hatua watu wanaopotosha takwimu za Serikali wakati ukweli wanaujua.

“Vita ya kupigania rasilimali za nchi ni ngumu sana, ninapata shida kubwa kutokana na kuongoza vita hii, inaniumiza sana lakini nimetumwa na Watanzania kuifanya kazi hii kwa moyo wangu wote.

“Wapo ambao kwao kubadilisha takwimu ni jambo la kawaida muwapuuze, watu wa aina hii wapo tu. Vyombo vya dola na Waziri wa Katiba muangalie watu wa aina hii.

“Nakumbuka kuna sheria ya takwimu ya mwaka 2015, anayebadilisha takwimu za Serikali anaweza kufungwa miaka miwili jela kwanini hatuvitumii hivi?

“Utakuta mtu anazungumzia makusanyo ya Serikali yameshuka, wakati anajua kabisa si kweli, watu wa namna hii wangekuwa wanapelekwa mahakamani waka justify,”alisema.

Alihoji endapo kweli mapato yanashuka, Serikali ingewezaje kusaini mkataba wa kujenga reli ya kisasa (standard gauge) wenye thamani ya Sh trilioni 7.

“Katika hesabu za kawaida tu kama mapato yanashuka utaweza kusaini mkataba wa kujenga reli wenye thamani ya Sh trilioni 7 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro mpaka Dodoma jumla zikiwa ni KM 726 na mkandarasi yupo ‘site’, sasa utapata wapi fedha kama makusanyo hayapo.

“Lakini katika Serikali ambayo haina mapato utaweza kununua ndege sita kwa mpigo? Umezinunua kwa kubadilisha na dagaa au migebuka ya Kigoma?

“Kama Serikali haina makusanyo bajeti ya afya ingepanda kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 269, utapata wapi fedha ya kupeleka umeme wa REA vijiji 4000.

“Kama huna mapato utatangazaje tenda ya meli ya Ziwa Victoria. Unaweza kutoa mifano mingi.  Sasa hivi tunatengeneza barabara kwa fedha zetu wenyewe.

“Muwapuuze wanaotaka kututoa kwenye direction (mwelekeo) kuacha kuzungumzia uchumi wetu. Mwingine mdomo unatoka mapovu anabeza juhudi zinazofanywa lengo lao likiwa ni kugombanisha wananchi na Serikali.

“Wanaopinga juhudi za Serikali za kupigania rasilimali za nchi wanatetea pesa walizoahidiwa na wezi wa rasilimali zetu, hao wasingeweza kunyamaza. Lazima wasemee matumbo yao.

“Lakini Watanzania wengi waliunga mkono juhudi hii kwa sababu wanajua ni namna gani walinyonywa kwa miaka yote,”alisema.

Jumamosi wiki hii, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliwaambia waandishi wa habari kwamba takwimu za Serikali kuhusu pato la taifa kwa robo ya pili ya mwaka zimepikwa.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali Dk. Hassan Abbas aliliambia MTANZANIA juzi kuwa Zitto hana uhalali wa kisiasa, kiuchumi wala kijamii kukosoa takwimu za Serikali kwa sababu hana vyombo vya kupima uchumi wa nchi lakini serikali inavyo.

Alisema suala la takwimu za kiuchumi hupimwa kitalaamu na si kisiasa na kwamba takwimu zilizopo zinaonesha Tanzania imekuwa ya pili kwa kuwa na takwimu bora Afrika.

Vita ya rasilimali

Akizungumzia kuhusu vita ya kupambana na uchumi, Rais Magufuli alisema kazi ya kumnyang’anya mtu mabilioni ya fedha ni mbaya na kwamba mtikisiko alioupata anaujua mwenyewe.

“Mimi mwenyewe mtikisiko niliokuwa naupata naujua mwenyewe lakini nilisema nilichaguliwa kwa ajili ya Watanzania, lolote ninalolipata ni kwa faida ya Watanzania kwa sababu walinichagua niwaongoze,”alisema Rais Magufuli.

Alisema mazungumzo waliyoyafanya na Kampuni ya Barrick ilitokana na namna walivyokuwa wanapata taarifa zote za namna nchi ilivyokuwa inaibiwa na kwamba Serikali ingeshtaki ingeshinda katika mahakama yoyote duniani.

“Tulipoanza zoezi hili tulikuwa tunajua, tunadili na watu wa aina gani, tulipata information zote na tunazo mpaka leo mawasiliano yote tunayo ya jinsi walivyokuwa wanaiba na walivyokuwa wanafungua akaunti nje.

“Na kwa sababu tunazo hizo information ndiyo iliwaleta hao watu kwenye mazungumzo kwa sababu tungeenda hata mahakama gani tungeshinda, hata iwe mahakama ya malaika tungeshinda,” alisema.

Alisema waliamua kuzungumza na kampuni hiyo ya Barrick kwa sababu ndiyo yenye hisa kubwa katika mgodi wa Bulyanhulu.

“Unapodili na issue kubwa kama hii usizungumze na wapiga kelele, zungumza na wenye mali ambao ni Barrick wenye hisa asilimia 64,” alisema.

Aliwashukuru viongozi wa vyama vya upinzani kwa kuruhusu wanachama wao kuwepo katika kamati za madini kwa sababu maendeleo hayana vyama na kwamba fedha zikiongezeka hata ruzuku za vyama itaongezeka.

Mbali na hayo, Rais Magufuli alisema kwa miaka 16 aliyokuwa waziri angeweza kuwa tajiri lakini aliwatumikia Watanzania kwa sababu anajua maisha ni mafupi.

“Maisha ni ‘too temporary’ kama ni utajiri basi na mimi ningekuwa tajiri nimekaa wizara ya ujenzi miaka16, lakini hata kama ningepata utajiri nilizaliwa uchi nitarudi uchi…nina box moja tu la kuwekewa kaburini I am nothing  (mimi ni bure) tumeumizwa mno wakati nchi yetu  ni tajiri mno,”alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles