27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AZUIA ZABUNI KAMPUNI BINAFSI TPA

AGATHA CHARLES na FLORENCE SANAWA, DAR ES SALAAM/ MTWARA

RAIS Dk. John Magufuli ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuachana na utaratibu wa kutoa zabuni za uendeshaji wa bandari kwa kampuni binafsi ambazo huingia mikataba isiyo na manufaa kwa nchi na kusababisha mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Agizo hilo alilitoa mjini Mtwara jana muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati namba mbili la Bandari ya Mtwara unaotarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 kuanzia sasa.

“Kwa sababu mmeamua kuichimba bandari hii ili kuongeza kina hadi mita 15 kwa kutumia fedha zetu, sitarajii TPA na wizara kuingia tena mkataba na wawekezaji wengine, kwa sababu imekuwa ni kawaida hapa Tanzania, tunatumia fedha zetu halafu wanakuja watu wengine kufanya biashara na fedha zetu kana kwamba nchi hii haina wasomi, na wanaokuja kuendesha kweli wanaiba,” alisema.

Aliwataka wakandarasi waliosaini mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo – Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd, kuanza kazi mara moja. Pia alisema mkandarasi anayejenga Barabara ya Masasi hana sifa.

Aliwataka wakandarasi hao kufanya kazi usiku na mchana na katika ubora ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

“Wakandarasi hakikisheni mnamaliza kazi kwa wakati, na kama inawezekana malizeni kabla ya muda, vizuri kufanya kazi usiku na mchana, nataka kuona mwisho wa mradi huu,” alisema.

Pia alisema ujenzi wa gati hiyo wenye urefu wa mita 350 umegharimu Sh bilioni 137.5 na utasaidia kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo mkoani Mtwara na nchi jirani zitakazokuwa zikisafirisha mizigo, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Masasi, alisema hana uhakika iwapo mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo anafaa kwa kuwa awali hakufanya kazi vyema.

“Nataka nimweleze hapa hapa, hakufanya kazi vizuri barabara ya kwenda Same- Mkumbara, kandarasi mwenzake aliyekuwa amepewa eneo kubwa alimaliza mapema, huyu hakumaliza, lakini nashangaa mmempa huku, sasa tufahamu kama amejirekebisha au kabla ya kumpa (zabuni) aliwapa nini kwanza. Ningekuwa mimi nisingempa kazi. Mimi nasema tu, sifahamu kama mlijiridhisha vizuri na huyu mkandarasi, au amejirekebisha,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles